Wareno wamfuata Bacca AFCON | Mwanaspoti

LEO timu ya taifa (Taifa Stars), itakuwa uwanjani ikicheza mechi ya pili ya Kundi C ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, lakini kabla ya mechi hiyo kuna simu kadhaa zimepigwa katika kambi ya Stars zikimuulizia beki wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Si uliona kiwango alichoonyesha beki huyo wa Yanga katika mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Nigeria, alipomtuliza straika wa Super Eagles anayekipiga Galatasaray ya Uturuki, Victor Osimhen? Basi kiwango hicho kimezifanya timu tatu tofauti za Ulaya zikiwemo mbili za Ureno kumsaka.

Katika mechi ya Tanzania na Nigeria, Bacca alikula sahani moja na Osimhen anayesifika kwa kufunga mabao na kabla ya jana timu hiyo kurudi uwanjani, kuna simu kadhaa zimepigwa kambini zikiulizia taarifa zaidi za beki huyo wa kati Mzanzibari.

Taarifa za simu hizo kutoka kwa maskauti wa timu tatu za Ulaya wakiongozwa na Wareno zimefichuliwa na mabosi wa TFF waliozipokea wakitafuta taarifa zaidi juu ya beki huyo.

Timu hizo ambazo moja inashiriki Ligi Kuu Ureno na nyingine Daraja la kwanza zimetuma maskauti Morocco kunakoendelea  mechi za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025, ikielezwa zimevutiwa na ubora na kiwango cha Bacca.

Maskauti hao wameonyesha kukomaa na Bacca kutokana na pia kwamba hazitapata shida kumnasa beki huyo kwa kuwa bado anacheza ligi ya ndani Tanzania.

Maskauti hao walitaka kupata taarifa za mawasiliano ya beki huyo na wasimamizi wake kabla ya kuvamia klabuni kwake, wakitaka huduma ya afande huyo wa Jeshi la KMKM.

“Yanga wanatakiwa kujiandaa kwani huyu Bacca wakati wowote anaweza kuuzwa maana kuna klabu mbili. Tangu tumecheza na Nigeria zinatafuta sana taarifa za beki huyu,” amesema bosi mmoja wa juu ndani ya TFF aliyepo Morocco.

“Wanataka kujua anasimamiwa na nani. Wanataka kujua mkataba na klabu yake. Mwisho wamekuwa wanatafuta mawasiliano ya wasimamizi wake,” alifichua kigogo huyo wa TFF na kuongeza:

“Wanasema mabeki wanaofanya vizuri wako wengi hapa Morocco, lakini wengi wanatoka ligi tofauti Ulaya, ila Bacca kwa kiwango chake na bado anacheza soka ndani ya Afrika hivyo itakuwa rahisi kumpata.”

Mbali na klabu hizo, pia Bacca amekuwa akihusishwa na timu ya Ligi Kuu England, Fulham na hii sio mara ya kwanza kwake kutolewa macho kwani hata katika fainali za msimu uliopita zilizofanyikia Ivory Coast, beki huyo alidaiwa kumezewa mate japo dili zake ziliishia hewani na kusalia Yanga.

Akiwa na Yanga, Bacca ametengeneza ukuta mgumu katika Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa akiwa sambamba ma Dickson Job, Bakar Mwamnyeto na Frank Assinki, kwani katika mechi sita za Ligi Kuu kwa msimu huu timu hiyo imeruhusu bao moja  lililotokana na ushindi wa 4-1 dhidi ya KMC na kwa mechi za CAF imeruhusu moja ilipolala 1-0 kwa Silver Strikers ya Malawi katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa ipo makundi.