Wabeba tumaini la Zanzibar Mapinduzi Cup 2026

ULE msimu wa raha kutoka visiwa vya marashi ya karafuu sasa umefika, mashabiki, wapenzi na wadau wa soka ndani na nje ya Zanzibar wamekaa mkao wa kula wakisubiria kushuhudia burudani kutoka kwa timu zitakazoshiriki Kombe la Mapinduzi 2026.

Kivumbi cha Kombe la Mapinduzi kitanza Desemba 28, 2025 kwenye uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja na mshindi ataondoka na kitita cha Sh150 milioni katika fainali itakayochezwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

Katika mashindano ya msimu huu, jumla ya timu 10 zitachuana zikiwa na makundi matatu, Kundi A likiwa na timu ya Mlandege, Azam, URA na Singida Black Stars. Kundi B kuna Simba, Mwembe Makumbi na Fufuni, wakati Kundi C zipo Yanga, KVZ na TRA United.

Huu ni msimu wa 20 tangu yalipoanzishwa mashindano hayo mwaka 2007 ikihusisha timu za Zanzibar na nje ya visiwani humo na timu nne zimechaguliwa kuipeperusha bendera ya Zanzibar.

Miongoni mwa timu zilizopata nafasi hiyo mbili zikiwa na uzoefu wa michuano hiyo ikiwemo Mlandege na KVZ, huku Mwembe Makumbi na Fufuni ni wageni.

Timu hizo za Zanzibar zina kazi ya kumaliza utawala wa Tanzania Bara kwani ndiyo zinaongoza kwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo. Azam ikichukua mara tano, Simba (3), Mtibwa Sugar (2) na Yanga (2).

Mbali na timu hizo za Tanzania Bara, pia URA inayokwenda kushiriki ikiwa ni timu pekee kutoka nje ya Tanzania, imewahi kubeba ubingwa mwaka 2016 ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika fainali.

WAWAK 04

Hii ni mara ya tatu kushiriki tangu mwaka 2022 na imefanikiwa kutwa ubingwa wa kombe hilo mara mbili mfululizo mwaka 2023 na 2024. 

Kwasasa klabu hiyo ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa imefunga mabao 20 na kuvuna alama 24 kati ya michezo 15.

WAWAK 01

Hii ni mara ya tatu kushiriki Kombe la Mapinduzi baada ya mwaka 2023 na 2024. Timu hiyo ina historia ya kufika hatua ya robo fainali katika miaka yote iliyoshiriki.

KVZ ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 23 ikicheza mechi 14.

WAWAK 02

Timu hii imepata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza ikitokea kisiwani Pemba. Fufuni imepanda daraja kushiriki Ligi Kuu Zanzibar msimu huu wa 2025-2026 huku ikionyesha ushindani mkubwa ikiongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 30 kabla ya Zimamoto kushuka dimbani kwani ikishinda inaweza kuishusha.

Ubora na kiwango kizuri cha timu hiyo ikiwa uwanjani kwa kuwa na uwezo wa kuwafunga magwiji wa Ligi hiyo, ndio imeipa hadhi na fursa ya kukiwakilisha kisiwa cha Pemba huku ikiiacha Chipukizi ambayo haina afya kwa sasa katika Ligi Kuu Zanzibar.

WAWAK 03

Licha ya kutofanya vizuri sana kwenye Ligi ya Zanzibar msimu huu imepata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar kwenye michuano hiyo, huku ikibebwa na nguvu ya pamoja kwa mashabiki wake wenye hamasa nzuri wakiwa uwanjani.

Mwembe Makumbi ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ZPL, imecheza mechi 14, imevuna alama 22 na kufunga mabao 14.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti wakiwa kisiwani hapa, viongozi wa timu hizo wakiwemo makocha na maofisa habari, walisema licha ya timu za Tanzania Bara kuwa na uzoefu wa mashindano makubwa kama hayo bado haijawa sababu ya kushindwa kuonesha ubora wao mbele ya klabu kubwa ikiwemo Simba na Yanga. 

Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohamed ‘Man Gamera’ alisema hadi sasa hajakiona kitu cha kumshtua kwa wapinzani wake isipokuwa Simba kwa sababu ina uzoefu wa mashindano makubwa na kuwa na wwachezaji wa kimataifa.

Alisema mchezo wa mpira ni wa wazi na kitu ambacho anapaswa kukizungumzia kwasasa ni udogo wa timu hiyo kushiriki mashindano hayo ingawaje sio sababu ya kushindwa kwani wamejiandaa vizuri.

Alisema Fufuni bado ni timu ndogo ambayo haina uzoefu hata kwenye Ligi Kuu Zanzibar lakini imeonesha ushindani wa hali ya juu kwa kuwafunga magwiji wa Ligi hiyo.

Hivyo, alisema lengo lake ni kuiona timu hiyo ikifika fainali na kuchukua kombe kwenye ardhi ya nyumbani (Pemba) na imani kubwa kwa timu hiyo wala hana wasiwasi na Simba.

Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China amesema timu hiyo imejipanga kutetea ubingwa wake na hawawezi kuruhusu kuchukuliwa.

Alisema maboresho ya kikosi hicho ni kufanya mazoezi kwa ari na nguvu zote jambo ambalo litawafanya kuwa imara wakati wote.

Naye, Ofisa Habari wa KVZ, Aljalil Mohamed aliliambia Mwanaspoti ujio wa kocha mkuu mpya, Malale Hamsini ni miongoni mwa maboresho ya kikosi hicho katika kujiandaa kuingia kwenye mashindano ya Mapinduzi 2026.

Alisema kama walifanikiwa kuvuka hatua ya robo faina awali, mwaka huu lengo lao ni kufika fainali ambayo itachezwa kisiwani Pemba.

Ameeleza kuwa, sababu ya kumchukua Malale kwenye benchi hilo la ufundi wanaona anaweza kuivusha timu hiyo ikiwa salama kutokana na uzoefu wake.

Pia, amesema wamefanya maboresho kwa upande wa wachezaji ambapo hili litabainika katika mchezo wa kwanza kati yao na TRA, pia kwao hakuna wapinzani wagumu hadi sasa.

Ofisa Habari wa Mwembe Makumbi, Hemed Suleiman ‘London Boy’ amesema timu hiyo itahakikisha inatoboa kwenye kundi lao haijalishi nani kapangwa naye.

Amesema, katika kuona hilo linafanikiwa wamefanya maboresho maeneo kadhaa ikiwemo eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa pasua kichwa upande wao na aliyesajiliwa ataonekana kwenye mchezo wao kwanza.