Kibaha. Umoja wa Makanisa Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani umetangaza mpango wa kuanzia mwaka 2026 kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za kiroho na kijamii kwa wafungwa magerezani.
Umesema hatua hiyo inalenga kuwajenga kimaadili na kiroho, ili kupunguza vitendo vya uhalifu wanaporejea uraiani, sambamba na kuimarisha upendo, amani na mshikamano nchini.
Kupitia mpango huo, imeelezwa umoja huo utajikita katika kuwahubiria wafungwa neno la Mungu na kuwapatia mahitaji muhimu yasiyo katika bajeti ya Serikali, kama vile nguo, miswaki na sabuni kwa lengo la kuwafariji na kuwajengea moyo wa utu na matumaini mapya ya maisha bora baada ya vifungo.
Akizungumza leo Jumamosi, Desemba 27, 2025, wakati wa ibada ya Umoja wa Makanisa iliyofanyika Kibaha kwa lengo la kuliombea Taifa, Mwenyekiti wa umoja huo, Julius Shemkai amesema mpango huo unatokana na vitendo vya baadhi ya wafungwa wanaomaliza vifungo kurejea tena gerezani kwa makosa ya wizi na uporaji.
Waumini wakiwa katika bada ya Umoja wa Makanisa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani leo Jumamosi Desemba 27, 2025. Picha na Sanjito Msafiri
Amesema hiyo inasababishwa na baadhi yao kukosa maadili na hofu ya Mungu, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwaandaa wafungwa kiroho na kimaadili wakiwa bado gerezani.
“Tumebaini baadhi ya wafungwa wakitoka gerezani wanarudia makosa yaleyale na kujikuta wakirejea tena vifungoni. Tunaamini kwa kuwafikia kwa neno la Mungu na kuwajenga kimaadili, kutawasaidia kufanya maamuzi sahihi wanaporejea uraiani,” amesema Shemkai.
Amesema lengo la mpango huo ni kuwahakikishia wafungwa kuwa Mungu yupo na anawapenda, ili baada ya kumaliza vifungo vyao waweze kurejea katika familia zao, kushiriki shughuli halali za kiuchumi na kuwa raia wema wenye mchango chanya kwa jamii, badala ya kurejea katika uhalifu.
Mbali na huduma za kiroho, Shemkai amesema umoja huo utaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha misaada inayotolewa inazingatia taratibu na inaleta tija kwa walengwa.
Waumini wakiwa katika bada ya Umoja wa Makanisa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani leo Jumamosi Desemba 27, 2025. Picha na Sanjito Msafiri
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mailimoja Kibaha, Aaron Chuma amesema kudumisha upendo na amani katika jamii kunahitaji viongozi wa dini kuwa karibu na makundi yaliyotengwa, wakiwamo wafungwa, badala ya kuwabagua kutokana na makosa au mapungufu yao ya awali.
“Kuna wakati baadhi ya viongozi wa dini wanakataa kutoa huduma kwa watu waliokuwa hawahudhurii kanisa kwa muda mrefu, hata pale wanapohitaji faraja au msaada. Hili ni jambo lisilo sahihi na linahitaji mabadiliko ya mtazamo,” amesema Chuma.
Ameongeza kuwa watu wote ni wa Mungu, hivyo viongozi wa kiroho wana wajibu wa kuwakumbatia waliotengwa, kusikiliza matatizo yao, kuwashauri na kuwaongoza katika kurejea kwenye maadili mema, huku wakiendeleza ujumbe wa amani, upendo na ushirikiano katika jamii.
Mmoja wa waumini waliohudhuria ibada hiyo, Nuru Samweli ameunga mkono mpango huo akisema utekelezaji wake utachangia kuimarisha upendo na amani nchini.
“Wafungwa muda mwingi huwa chini ya uangalizi wa askari magereza, lakini viongozi wa kiroho wanapowatembelea na kuwapa neno la Mungu, wanajisikia faraja na kurejeshewa utu wao,” amesema.
Umoja wa Makanisa unaojumuisha Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) na Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (TEC), ulianzishwa kwa lengo la kuyaunganisha makanisa kushirikiana katika masuala ya kiroho, kijamii na kitaifa.
Kupitia umoja huo, makanisa yameendelea kutoa mchango katika kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa, maadili na kusaidia makundi yenye uhitaji, hatua inayosaidia pia juhudi za Serikali katika kudumisha utulivu na maendeleo ya jamii.