Mungu akikupa baraka kuishi mwaka 2026 utamfanyia nini?

Bwana Yesu asifiwe mtu wa Mungu, ni matumaini yangu mmesherehekea Krismasi kwa amani na utulivu. Karibu katika tafakari ya neno la Mungu. Tumepewa somo linaloema “Kama Mungu akikupa kuishi mwaka 2026 utamfanyia nini?

Wengi wetu katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka tunaomba Mungu atuvushe salama na atupe nafasi ya kuuona mwaka mpya 2026. Yamkini lengo la maombi haya ni kwasababu tunahitaji kutekeleza mipango mizuri tuliyo nayo kwa mwaka 2026.Si watu wengi ambao tunafikiri kuanda mipango kwaajili ya kumzalia Mungu matunda.

Wako watu wengi ambao walitamani kuishi mwaka tunaomaliza 2025 lakini hawakupata hiyo nafasi kama mimi na wewe; lakini pamoja na nafasi tuliyopata inawezekana hatukumletea Mungu faida yoyote zaidi ya kuleta hasara katika dunia aliyotuweka tuitunze. Leo hii tunarudi kumuomba tena atupe mwaka mwingine 2026. Swali je kama akitupa kuishi 2026 tunawaza kumfanyia nini?

Nini matarajio ya Mungu kwetu

Ukisoma kitabu cha Luka 13:6-9 inaelezea habari ya mtini usiozaa matunda.

“Akanena mfano huu, mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu, akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate, Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu nisipate kitu, uukate mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia Bwana wake uuache mwaka huu nao hata niupalilie, niutilie samadi, Nao ukizaa matunda baadaye vema, La usipo zaa ndipo uukate.

Mambo matatu ya kutafakari katika hii mistari

Pamoja na mwonekano mzuri wa majani ya mtini lakini bado haukuwa na faida yoyote kwa mwenye shamba kwasababu lengo lake haikuwa kupata majani mazuri bali matunda. Ustawi wa nnje kimwili, kiafya, kiuchumi siyo kigezo cha Mungu kutuona tuna faida kwake na kwa dunia bali kuwa msaada kwa wengine ndio matarajio yake. Mungu hakutuleta duniani ili tustawi bila kumletea faida yoyote. Faida anayoitarajia Mungu ni kuona vitu anavyotubarikia vinakuwa chanzo cha furaha kwa wengine na si chanzo cha uharibifu.

Kama vile mwenye shamba la mizabibu alivyotarajia kuona matunda kutoka kwa mtini ndivyo na Mungu anavyotarajia kuona matunda kutoka kwetu. Mtini umewakilisha mwanadamu na matunda ni matokeo mema ambayo Mungu anatarajia kutoka kwa huyu mwanadamu. Mungu anatarajia kuona mwanadamu aliye muumba anakuwa ni chanzo cha upendo, furaha, haki, amani na utu wema kwa wandamu wengine ili wanadamu wengine wanaozaliwa waone duniani ni mahala salama pa kuishi. Tujiulize je kwa maisha tunayoishi na matendo tunayofanya tunamzalia Mungu matunda?

Mistari tulioisoma inaelezea jinsi Mtunza mtini alivyokuwa akienda shambani mfululizo kwa miaka mitatu akiangalia kama mtini utamzalia matunda lakini hakupata chochote. Baada ya hii miaka mitatu mwenye shamba alikosa uvumilivu na akaamuru ule mtini ukatwe. Kila mtu Mungu amempa muda wake wa kuishi hapa duniani na anatarajia kuona kwa muda aliotupa kuishi tunamzalia matunda yaani kutunza amani, upendo, haki na utu wema kwa ajili ya wanadamu wengine kuishi baada ya sisi kumaliza muda wetu.

Yamkini mimi na wewe tumeishi miaka mingi zaidi ya huu mtini ambao mwenye shamba aliamuru ukatwe baada ya miaka mitatu kupita bila kuzaa matunda. Mungu amekuwa akituvumilia matendo yetu kwa matarajio ya kwamba tutabadilika ili tumzalie matunda ya kumpendeza lakini kila anapotutazama haoni kinachobadilika zaidi ya kuendelea kuleta uharibifu.

Tunapoelekea mwisho wa mwaka 2025 na kukaribia mwaka 2026 ni vyema tukaomba toba na rehema mbele za Mungu ikiwa tulishindwa kumzalia Mungu matunda mema na badala yake tulichangia kuiharibu dunia kwa matendo yetu yasiyompendeza.

Mungu anatarajia kuona kila mmoja wetu anakuwa chanzo cha kutunza ufalme wake hapa duniani yaani tunaleta upendo, furaha, haki na amani katika dunia (Warumi 14:17). Ni ombi langu kwa Mungu kwamba mwaka 2026 Mungu aone kila mtu ni chanzo cha kumletea faida duniani na si hasara. Hivyo ili Mungu atubariki katika maisha yetu, anatarajia kwanza kuona matokeo kutoka kwetu. “Yohana 15:2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa na kila tawi lizaalo hulisafisha ili lizidi kuzaa.” Mungu akubariki msomaji wangu na niwatakie heri ya Mwaka Mpya ambapo tunatarajia kuukaribisha usiku wa Jumatano wiki hii.