Ni vitu vidogo lakini vina maana katika ndoa

Canada. Leo, tutaanza na maswali ya kichokozi. Ni maswali yanayoweza kuonekana ya kawaida,  ila yanabeba mengi kuhusiana na siha au ugonjwa wa ndoa.

Kuna vitu vinavyoweza kuonekana vidogo, visivyo vya maana hata kukera. Kama ukivichunguza uzuri, vina maana kubwa.

Kwa mfano, mnaenda dukani mkiwa mmeshakubaliana na mwenza wako nini cha kununua. Hata hivyo, baada ya kufika, mama au baba anakuuliza “nanunua hiki. Je wakionaje?” (Tabia hii wanayo kinamama japo hatujui kama kuna kinababa nao wanayo).

Kwa wasiojua lengo la swali kama hili, unaweza kuanza kujiuliza, kulaumu, hata kulalamika na kujisemea “sasa kama ushaamua kununua, unaniuliziani?”  

Wengine wanaweza wasijibu ili kuepusha shari au kujibu ovyo na kuiita shari bila ulazima.  Hivi, huwa unajisikiaje mwenzio anapofanya jambo bila kukushirikisha wakati ambao ulitaka ushirikishwe?

Ukitaka kujibu au kujua umuhimu wa changamoto na maswali hayo hapo juu ili upate jibu sahihi, jiulize. Ningekuwa mimi ndio nauliza swali kama hili, ningetegemea au kutaka kujibiwa nini?

Ni bahati mbaya. Si wengi wanajiuliza swali hili kabla ya kujibu au kutojibu. Kimsingi, binadamu hatuna uwezo wa kuingia kwenye vichwa vya wenzetu kujua kilichomo. Ingewezekana, hii makala isingekuwapo na kama ingekuwapo isingekuwa na maana.

Mfano mwingine, ni pale mnapopanga kutoka kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa au marafiki.Mara, unakuta mwenzio keshavaa nguo, ila unaambiwa “kati ya nguo hii na ile unataka nivae ipi?”

Kabla ya kujibu, kwa mara nyingine, jiulize. Ningekuwa mimi ningetaka au kutegemea jibu gani. Sasa kama hili hujui linasaidiaje, jibu utakavyo.

Mwambie mwenzio “vaa hii au ile.” Ajabu, ukimwambia hivyo, anaridhika. Lakini hebu badili jibu mfano useme “kwani wewe huna macho au unapenda ipi?” Tuamini  hiyo safari itaingia nyongo.

Mwenzio anajibu “wewe unataka nivae ipi?” Unashangaa na kujiuliza “je wavaa wewe au wanivalia mie?” Je, uliwahi kujiuliza, kwa wale wanaoulizwa au waliowahi kuuliza, ni kwanini mwenzio anakuuliza?

Je, ni wangapi wanavumilia, kuthamini na kujibu maswali haya yanayoweza kuonekana madogo hata ya ovyo japo ni muhimu? Kama hatakuuliza wewe, amuulize nani?

Kukutaka ushauri siyo kutojiamini au kutaka kukuchosha au kutokuwa na uwezo wa kuamua nini cha kuvaa au kununua. Ni kukuamini na kutaka muwe kwenye muktadha mmoja na ulio sawa. Pia, mfahamu kuwa acho mawili ni bora kuliko moja. Na isitoshe, huko muendako, wengi hawamwangalii kwa undani kama ufanyavyo wewe. Hebu jiulize. Unapotoka nyumbani kwenda mjini, unakutana na watu wangapi? Je huwa unawakambuka wangapi?

Unaweza kwenda sehemu ukatoka bila kujua yeyote kana kwamba ulikuwa peke yako. Kwa wale wanaosafiri wanajua hili. Hebu fikiria. Uko kwenye viwanja vikubwa vya ndege kama Chicago au Heathrow.

Ni watu wangapi wanakuwapo? Bila shaka ni maelfu.  Je, ukishachukua ndege yako na kuondoka, ukiachia wale wachache waliokuhudumia, wengine huwa unawakumbuka?

 Kwa taarifa ya msomaji wetu, watu wanaweza kuona kasoro haraka kuliko ubora. Kilichowazi, waone ubora au kasoro, nawe utahusika.

Mfano, mmoja wenu akienda harusini au sehemu akiwa amevaa nguo zisizostahili, utasikia watu wakisema “umeona mke au mume wa fulani alivyovaa leo?”

Akiwa au mkiwa mmependeza, pia, utawasikia wakisema “umeona mke au mume wa fulani alivyopiga vitu vya bei mbaya?”

 Hivyo, basi, sababu nyingine za kuuliza maswali hayo juu, mojawapo ni hii. Watu wanaowajua wanaona na kuwaeleza kama muwaonavyo au kuwaelezea.      

Yote tisa. Huwa, hasa kinababa unajisikiaje mkeo akikuuliza ‘leo tupike nini?” ilhali anayepika ni yeye? Ujue. Wakati akiuuliza hili, anaweza kuamua kuchagua chakula chochote akapika na mkala.

Ila kwa kutaka wote mpate mnachokitaka, mwenzio atakuuliza si kwa sababu hawezi kuamua kuchagua cha kupika. Ni ile hali ya kutaka wote mridhike.

 Tunashauri na kusihi wanandoa sana. Kabla ya kumhukumu mwenzio kwa lolote hata liwe dogo au kubwa kiasi gani, jiulize “ningekuwa mimi ningependa nipate jibu au ushauri gani?” Pia, ni vyema kukumbuka kuwa vichwa viwili ni bora kuliko kimoja.

Tufunge mwaka na kuwatakia heri ya mwaka mpya nyote.