Pazia la Mapinduzi Cup 2026 lafunguliwa na mambo mawili

KWA namna waandaaji wa Kombe la Mapinduzi 2026 walivyopanga ratiba ya ufunguzi ni wazi waliangalia mambo mawili.

Kwanza ushindani ndani ya uwanja, pili burudani kwa mashabiki watakaofika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Ushindani uwanjani na burudani unatokana na mechi ya kwanza itakayochezwa leo Jumapili, kisha ile ya pili saa 2:15 usiku.

Mabingwa mara mbili mfululizo 2023 na 2024, Mlandege itaikaribisha Singida Black Stars ambayo baada ya kocha Miguel Gamondi kuwa na jukumu la kuiongoza Taifa Stars katika AFCON 2025, mzigo ameachiwa David Ouma.

MAPI 04

Singida Black Stars inashiriki Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza, lakini Mlandege inakumbuka wakati inabeba ubingwa wa kwanza na wa pili katika michuano hii, ilizichapa timu za Tanzania Bara.

Mwaka 2023 ilianza kuifunga mabao 2-1 Singida Big Stars ambayo sasa inaitwa Fountain Gate, kisha 2024 ikawa zamu ya Simba kupigwa bao 1-0.

Singida Black Stars ambayo awali ilikuwa ikiitwa Ihefu, ushiriki wa mara ya kwanza katika michuano hiyo hauwezi kubezwa kwani imekuwa ikifanya vizuri ndani na kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Ikiwa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho ikianza kwa kufungwa kisha sare, Singida inajivunia taji la Kagame ililobeba Septemba, mwaka juu jijini Dar.

MAPI 03

Kushinda ubingwa huo na kucheza kwao makundi kimataifa, kunaifanya Singida Black Stars kutajwa miongoni mwa timu zinazopewa kipaumbele cha kubeba Kombe la Mapinduzi.

Kwa Mlandege, ukiachana na kutoanza vizuri Ligi Kuu Zanzibar msimu huu ikiwa bingwa mtetezi, lakini imepania kutetea tena Kombe la Mapinduzi ambalo sasa linachezwa kwa kushirikisha timu za klabu baada ya 2025 kuwa timu za taifa.

Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China, amesema: “Kama kawaida yetu tumejipanga kufanya vizuri, tunataka kuona ule ubingwa tuliouchukua mwaka 2023 na 2024, tunauchukua tena safari hii ili kuzidi kuonyesha  ubora wetu.”

Kwa upande wa Ouma, amesema: “Hakuna mashindano tunayoshiriki hatuyapi kipaumbele. Kwetu ni fursa nzuri kuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki Mapinduzi yatakayokuwa na timu nyingi shindani. Yatatusaidia kuiweka timu kwenye nafasi nzuri.”

MAPINDUZI Pict

Mabingwa wa kihistoria katika michuano hii, Azam FC itapepetuana na URA kutoka Uganda kuanzia saa 2:15 usiku.

Hii ni mechi ya mabingwa kwani timu zote zimelichukua Kombe la Mapinduzi kwa nyakati tofauti.

Azam ikiwa ndiyo imelibeba mara nyingi zaidi tangu 2007 ambazo ni tano, imelichukua 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

URA imelichukua mara moja pekee mwaka 2016.

Mbali na hilo, hii mechi itaturudisha nyuma hadi 2018, wakati Azam ikitwaa ubingwa wa nne, fainali iliichapa URA kwa penalti 4-3 baada ya dakika tisini ngoma kumalizika 0-0.

Kocha wa Azam, Florent Ibenge amesema: “Azam ni timu kubwa, hakuna shindano tunakwenda bila malengo ya kuchukua ubingwa…”