YANGA inapiga hesabu na kupambana kumsajili winga mmoja kutoka DR Congo, Ibrahim Matobo, ambaye kama akimalizana na mabingwa hao watakuwa wamelanda dume na kuimarisha kikosi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba, ripoti ya kocha Pedro Goncalves imeelekeza mabosi kuleta winga wa maana ili kukiongezea nguvu kikosi hicho kabla ya kurudi tena katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi B.
Mwanaspoti limedokezwa kuwa, mabosi wa Yanga wapo katika harakati za kusajili winga mpya na karata zimemuangukia Mkongomani Matobo anayekipiga Les Aigles du Congo, na tayari mazungumzo na klabu yake ya sasa yameshaanza.
Inadaiwa Pedro anamjua Matobo ambapo katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024), zilizofanyika Tanzania, Kenya na Uganda alikutana naye Angola aliyokuwa akiinoa na DR Congo zote zikiwa kundi moja zilizocheza mechi jijini Nairobi.
Katika michuano hiyo, Matobo alifunga bao moja dhidi ya Zambia akipokea mpira wa asisti kutoka kwa mshambuliaji Japhte Kitambala aliyepo Azam FC kwa sasa wakati DR Congo ikishinda 2-0.
Taarifa hizo zinasema mazungumzo yameanza na iwapo Yanga ikifanikiwa kumpata Matobo, itakuwa imeimarisha eneo la kushoto ambalo winga huyo akicheza huwa na balaa zaidi akisifika pia kwa kumwaga maji.
Ilisema mbali na kujua kutengeneza nafasi na kupangua mabeki, Matobo anajua kufunga kama akipata nafasi ya kufanya hivyo, kwani msimu huu tayari ameshafunga mabao sita na kutengeneza asisti tatu.
“Tumempa kocha yule winga Matobo, atatuambia kama atatufaa basi tutamalizana na klabu yake haraka, winga mzuri na umri wake sio mbaya bado ana nguvu,” mmoja wa vigogo wa Yanga aliliambia Mwanapoti na kuongeza:
“Tunataka kuiongezea timu nguvu kabla ya mechi zitakazoendelea. Kama mambo yatakwenda vizuri mnaweza hata kumuona katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoanza Jumapili (leo).
“Pale DR Congo mawinga wawili hatari wanaosifika kwa sasa ni Matobo na Joseph Kabwiti wa TP Mazembe ambao wanachuana vikali kwenye ligi ya huko.”
Ujio wa Matobo kma utafanikishwa, basi mawinga waliopo kwa sasa ndani ya timu hiyo akiwamo Maxi Nzengeli, Celestin Ecua, Fardi Mussa, Denis Nkane na Edmund John watakuwa na kazi ya kujipanga na hata baadhi yao kuchomolewa kikosini kipindi hiki cha dirisha dogo linalofunguliwa Januari 1-31, mwakani.
