Dar es Salaam. Wakati abiria wa treni ya kisasa (SGR) wakilalamika kusota kwa muda stesheni bila safari kuanza, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeeleza hali hiyo imesababishwa na changamoto za kiufundi zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu hali hiyo leo Desemba 28, 2025 saa 12:24 mchana, baada ya kuripotiwa kwa malalamiko ya abiria kusubiria kwa muda mrefu bila safari kuanza, katika stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema mvua zimesababisha hitilafu za kiufundi ambazo zinashughulikiwa na mafundi wa shirika hilo.
Ambapo kuanzia asubuhi ya leo mpaka muda anazungumza na Mwananchi hakukuwa na safari ya treni hiyo iliyofanyika, hivyo abiria waliokata tiketi kurundikana stesheni ya Magufuli wakisubiri usafiri. “Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, changamoto ya kiufundi imejitokeza na tunaifanyia kazi. Juhudi zinaendelea na muda si mrefu safari zitaanza. Tatizo hili liko nje ya uwezo wetu kwa kuwa mvua zimetuathiri,” amesema.
Masanja amesema athari kubwa zaidi zimeikumba reli ya zamani (MGR), ambayo baadhi ya miundombinu imeharibika, yakiwamo madaraja katika eneo la Gulwe, mkoani Dodoma na Kilosa, mkoani Morogoro.
Kwa upande wa treni ya SGR, amesema athari si kubwa na mafundi wanaendelea na ukaguzi wa kina ili kuhakikisha usalama kabla ya kuruhusu safari kuendelea.
“Hatuwezi kuruhusu treni kupita bila kujiridhisha kuwa njia ni salama. Tunafanya ukaguzi wa kina na kufikia hatua ya mwisho ya kuruhusu safari kuanza. Kikubwa tunawaomba abiria waendelee kutuamini, kwani lengo letu ni kutoa usafiri bora, wa uhakika na salama,” amesema.
Masanja amesema safari za SGR zitaendelea kama kawaida baada ya ukaguzi kukamilika, huku juhudi zikiendelea kurejesha huduma kwa haraka kwenye reli ya zamani iliyoathiriwa na mvua.