Myanmar yafanya uchaguzi, lakini… | Mwananchi

Dar es Salaam. Myanmar imefanya uchaguzi wake wa kwanza tangu jeshi lilipompindua madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Aung San Suu Kyi, mwaka 2021.

Ingawa uchaguzi huo unatazamwa kuwa hatua muhimu kwa amani ya taifa hilo, tayari umekumbwa na vikwazo lukuki ikiwemo vita vya ndani na tuhuma za kutokua huru na wa haki.

Uchaguzi huo, umeanza leo Jumapili, Desemba 28, 2025 na unafanyika katika takribani theluthi ya maeneo 330 ya kiutawala ya taifa hilo, huku mengi yakishindikana kufikika kutokana na mapigano kati ya jeshi na makundi ya upinzani.

Baada ya awamu ya kwanza, duru mbili nyingine za upigaji kura zinatarajiwa kufanyika Januari 11 na Januari 25, huku kura zikifutwa katika maeneo 65. Kwa maneno mengine asilimia 20 ya wananchi wamenyimwa haki ya kupiga kura katika hatua hiyo.

Kutokana na hali hiyo, kinachoangaliwa zaidi ni ushiriki wa wapigakura hasa katika miji mikubwa. Kwani tangu upigaji kura ulipoanza idadi ya kawaida ya wapigakura ilishuhudiwa.

Uchaguzi huo umekumbwa na ukosoaji mkubwa ikiwemo Umoja wa Mataifa, nchi za magharibi na mashirika ya haki za binadamu, yakiutaja kuwa si huru, si wa haki wala hauna uhalali, kwa kuwa vyama vinavyopinga utawala wa kijeshi havishiriki.

Aung San Suu Kyi, aliyeng’olewa madarakani miezi michache baada ya chama chake cha National League for Democracy (NLD) kushinda kwa kishindo uchaguzi wa 2020, bado anazuiliwa, huku chama chake kikivunjwa rasmi.

Dalili zinaonyesha chama kinachoungwa mkono na jeshi cha Union Solidarity and Development Party (USDP) kinatarajiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Jeshi, ambalo limeitawala Myanmar tangu mapinduzi ya 2021, linasema uchaguzi huo ni fursa ya mwanzo mpya wa kisiasa na kiuchumi kwa taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 55.

Kiongozi wa jeshi, Jenerali Mkuu Min Aung Hlaing, ameendelea kuutaja uchaguzi huo kama njia ya maridhiano ya kitaifa.

Akiwa amevalia nguo za kiraia, Min Aung Hlaing alipiga kura muda mfupi baada ya vituo kufunguliwa katika mji mkuu, Naypyidaw, kisha akaonyesha kidole chake kilichopakwa wino maalumu na kutabasamu mbele ya waandishi wa habari.

Baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa, uchaguzi huo ni huru na wa haki, na haujachafuliwa kwa sababu unasimamiwa na jeshi.

Gazeti la Serikali, Global New Light of Myanmar, liliandika maoni kuwa, uchaguzi huo utafungua ukurasa mpya na kuwa daraja kwa wananchi wa Myanmar kuelekea mustakabali wa ustawi.

Gazeti hilo pia liliripoti kuwa, waangalizi wa uchaguzi kutoka Russia, China, Belarus, Kazakhstan, Cambodia, Vietnam, Nicaragua na India, wamewasili nchini humo kabla ya upigaji kura.

Wakati mapigano yakiendelea katika maeneo mengi ya nchi, mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Tom Andrews, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuukataa uchaguzi huo unaoendeshwa na jeshi.

“Uchaguzi unaoandaliwa na jeshi linaloua raia, kuwafunga viongozi wa kisiasa na kuhalalisha ukandamizaji wa kila aina ya upinzani si uchaguzi, ni maigizo ya kisiasa yanayoendeshwa kwa mtutu wa bunduki,” amesema Andrews katika taarifa yake.

Amesema huo si mwelekeo wa kutatua mgogoro wa Myanmar, bali ni hila itakayodumisha ukandamizaji, migawanyiko na migogoro zaidi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochochewa na mapinduzi ya 2021 vimesababisha vifo vya takribani watu 90,000, kuwalazimisha zaidi ya milioni 3.5 kuyahama makazi yao na kuwaacha takribani watu milioni 22 wakihitaji msaada wa kibinadamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Assistance Association for Political Prisoners, zaidi ya watu 22,000 wanazuiliwa kwa makosa ya kisiasa.

Katika Jiji la Yangon, vituo vya kupigia kura vilikuwa vimezungushiwa vizuizi usiku kucha,   huku askari wenye silaha wakilinda makutano ya barabara.

Maofisa wa uchaguzi waliweka vifaa na mashine za kielektroniki za kupigia kura, ambazo zinatumika kwa mara ya kwanza nchini Myanmar. Mashine hizo haziruhusu kura batili wala majina ya wagombea wasio kwenye orodha.

Miongoni mwa wapigakura wa mapema alikuwa Swe Maw (45), aliyepuuza ukosoaji wa kimataifa akisema, “si jambo la muhimu sana. Ni kawaida kuwepo wanaopenda na wasiopenda.”

Lakini katika eneo la Mandalay, Moe Moe Myint (40) amesema haiwezekani kwa uchaguzi huo kuwa huru na wa haki.

“Tunawezaje kuunga mkono uchaguzi unaoendeshwa na jeshi hili lililoharibu maisha yetu? Tunaishi bila makazi, tunajificha misituni, tunaishi kati ya uhai na kifo,” amesema.

Duru ya pili ya upigaji kura itafanyika baada ya wiki mbili, kabla ya duru ya mwisho Januari 25. Hadi sasa, tarehe za kuhesabu kura na matokeo hazijatangazwa.

Wachambuzi wanasema jaribio la jeshi kuanzisha utawala thabiti wakati vita vikiendelea kote nchini humo,  lina hatari kubwa na kwamba uhalali wa kimataifa kwa serikali yoyote itakayodhibitiwa na jeshi ni mdogo.

Mchambuzi wa International Crisis Group, Richard Horsey, aliandika hivi karibuni kuwa, matokeo ya uchaguzi huo yako wazi, ushindi utaenda kwa USDP na kuendelea kwa utawala wa kijeshi uliojificha chini ya sura ya kiraia.

“Uchaguzi huu hautatatua mgogoro wa kisiasa wa Myanmar wala kupunguza msimamo wa upinzani wenye silaha. Badala yake, utaimarisha migawanyiko ya kisiasa na kuendeleza hali ya kuyumba kwa taifa,” aliandika.

Aliongeza Serikali mpya itakayochukua madaraka Aprili 2026 itakuwa na machaguo chache, uhalali mdogo na mkakati usioeleweka wa kuiondoa Myanmar katika mgogoro wa muda mrefu.