Moshi. Neno ‘ametekwa’ lilitumiwa kwa kiwango kikubwa mwaka 2025 na ndugu na marafiki kwa kila tukio la ukamataji, hali iliyokuwa ikizua taharuki.
Lakini swali linalojibiwa na mawakili ni kwa nini kila ukamataji ulihesabika kuwa ni utekaji.
Katika matukio hayo ya ukamataji, kwa wale ambao baadaye walipatikana wakiwa vituo vya polisi au kutoweka kabisa na hadi sasa hawajulikani walipo, inadaiwa walioendesha ukamataji huo walikuwa wamevaa kiraia, walikuwa na silaha za moto na walimiliki pingu.
Bahati mbaya, hata ndugu walipozunguka katika vituo mbalimbali vya Polisi, waliambiwa kuwa ndugu zao hawapo katika vituo hivyo, hali iliyowafanya kuamua kusambaza taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa ndugu yao ‘ametekwa’.
Mawakili waliozungumza na Mwananchi kuhusiana na hali hiyo, katika kipindi hiki tunachoelekea kuufunga mwaka, wamesema hali hiyo ilichangiwa na uwepo wa wimbi la utekaji watu, ambalo hadi leo Polisi hawajaweka wazi ni genge gani linalochukua watu kwa mtindo wa ukamataji na kisha kutoweka nao.
Watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, mwanaharakati Mdude Nyagali na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Deusdedit Soka.
Inaelezwa kuwa Soka alipigiwa simu na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na kumwita akachukue pikipiki yake kituo cha Polisi, lakini akiwa njiani, yeye na wenzake wawili walichukuliwa na watu waliohisiwa au kudhaniwa kuwa ni Polisi.
Wengine ambao hadi sasa hawajulikani kama walichukuliwa na Polisi au genge la watekaji ni pamoja na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Daniel Chonchorio, na aliyekuwa mtia nia udiwani Kata ya Ganyange mkoani Mara, Siza Mwita.
Kwa mujibu wa mawakili hao, ukamataji holela usiozingatia sheria, uliofanywa na askari wasio na sare, uliwafanya wananchi washindwe kutofautisha kati ya ukamataji wa polisi halisi na genge la watu wasiojulikana.
Akizungumzia sababu iliyofanya kila tukio la kukamatwa kudhaniwa kuwa ni utekaji, Wakili wa Mahakama Kuu, Gebra Kabole, amesema haikuwa rahisi kutofautisha kati ya ukamataji halali wa Jeshi la Polisi na ukamataji wa genge la watu wasiojulikana, kwa kuwa katika matukio mengi utaratibu wa kisheria haukufuatwa.
Amesema waliokuwa wakifanya ukamataji walijitambulisha kama polisi, hivyo suala la utambulisho halikusaidia kutenganisha uhalali wa hatua hizo, kwa sababu wote walivaa nguo za kiraia, walijitambulisha kuwa ni polisi na walikuwa na pingu pamoja na silaha za moto.
“Hata baadhi ya matukio yaliyohusisha Jeshi la Polisi, awali polisi walikana kuwakamata watu hao, lakini baadaye ilibainika kuwa waliwashikilia na hata kuwapatia dhamana,” amesema Kabole.
Ametoa mifano ya mwanaharakati Hilda Newton, ambaye alikamatwa na polisi lakini jeshi hilo lilikana awali kabla ya baadaye kumtoa, pamoja na John Heche, aliyekamatwa huku ikidaiwa kuwa ni Idara ya Uhamiaji, lakini baadaye ikabainika kuwa alikamatwa na polisi.
Kwa mujibu wa wakili huyo, ili tukio lisitafsiriwe kama utekaji, ni lazima sheria ifuatwe kikamilifu. Amesisitiza kuwa hata kama mtu amekamatwa na Jeshi la Polisi, endapo taratibu za kisheria hazikuzingatiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, ukamataji huo hugeuka kuwa utekaji.
Kabole amesema ni muhimu kufuatwa kwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20, kama ilivyorejewa mwaka 2023, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO), ili wananchi waweze kutofautisha kati ya utekaji na ukamataji halali wa polisi.
Amesema mtu anayekamatwa ana haki mbalimbali, ikiwamo kuambiwa kuwa yuko chini ya ulinzi, kumtambua anayemkamata, kuambiwa sababu ya kukamatwa kwake pamoja na haki ya kumjulisha wakili au ndugu.
Aidha, amesema mtuhumiwa ana haki ya kuambiwa kuwa ana haki ya kutotoa maelezo yoyote kwa polisi, haki ya kutolazimishwa kukiri kosa lolote na haki ya kudhaniwa kuwa hana hatia hadi Mahakama ithibitishe kosa analotuhumiwa.
Kwa upande wake, Wakili Peter Madeleka amesema Sheria ya CPA, Sura ya 20, imefafanua wazi maana ya ukamataji, namna unavyopaswa kufanyika na nani mwenye mamlaka ya kukamata, wakiwamo askari wa Jeshi la Polisi.
“Ili kubaini kama tukio ni la utekaji au ukamataji halali, lazima uangalie sheria. Ukikuta kinachodaiwa kuwa ni ukamataji kiko kinyume cha sheria, basi huo si ukamataji, hata kama aliyekamata ana mamlaka,” amesema Madeleka.
Amefafanua kuwa Kifungu cha 11 cha CPA kinaeleza kuwa ukamataji bila hati (arrest without warrant) unapaswa kufanyika pale mtuhumiwa anapofanya kosa mbele ya askari au mtendaji mwenye mamlaka.
Kwa mujibu wa Madeleka, polisi anapomkamata mtu ni lazima ajitambulishe, amweleze kosa analotuhumiwa na ampe haki ya kuwasiliana na ndugu au wakili wake, ingawa mara nyingi taratibu hizo hazifuatwi.
Ameongeza kuwa mtu anayekamatwa lazima apelekwe katika eneo sahihi, yaani kituo cha polisi, ndani ya muda unaotakiwa kisheria. Endapo masharti hayo hayatazingatiwa, amesema, tukio hilo haliwezi kuitwa ukamataji bali hugeuka kuwa utekaji.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kama sheria zingefuatwa katika ukamataji, nchi isingefikia hatua ambayo raia wake wanahusisha kila ukamataji na utekaji.
“Unakuta watu wanakamata watu bila kujitambulisha, sheria zinakataza kabisa kuvaa nguo za kiraia katika mazingira ambayo wangeweza kuvaa sare. Sheria inataka upitie kwa viongozi wa mitaa au vitongoji, lakini hazifuatwi,” amesema na kuongeza;
“Ukamataji mwingine unaofanywa na Polisi unapelekea hata wale watu ambao pengine wana nia mbaya kutumia fursa hiyo kuteka watu. Kama mnakumbuka alivyochukuliwa Ally Kibao, wale watu walijitambulisha kuwa ni polisi, baadaye tukasikia ameuawa.”
“Wakati mwingine ni vigumu kutofautisha utekaji na ukamataji wa Polisi. Ndiyo maana sisi tulisema, ili Jeshi la Polisi liepuke kuhisiwa ni watekaji, wasikamate watu bila sare na wasiende bila kuandamana na viongozi wa mtaa.
“Wanatakiwa wajitambulishe na kuwaambia ndugu wanampeleka kituo gani cha Polisi. Lakini yote haya hayazingatiwi na ndiyo yamechangia watu kupotea. Utekaji unahusisha sana aina hii ya ukamataji, ya kutofuata sheria zilizopo,” amesisitiza.
Amesema kama taifa lazima ifike mahali mifumo ifumuliwe; “twende kwenye Katiba mpya, turidhie mikataba ya kimataifa inayokataza utekaji na upoteaji wa watu. Mwaka huu (2025) matukio ya utekaji yamekuwa mengi sana.”
Ngurumwa amesema kwa mwaka 2025 pekee kuna matukio zaidi ya 100 ya utekaji na kupotea kwa watu, na kuitaka Serikali na Jeshi la Polisi kuweka wazi uchunguzi wao kuhusu waliowateka watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo.
Baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri George Simbachawene alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha ukamataji wa watuhumiwa unatekelezwa kwa kufuata misingi ya sheria na kwa kuzingatia staha.
Simbachawene alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, Desemba 8, 2025, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Alisema kuna aina ya ukamataji unaofanywa na askari wa Jeshi la Polisi nchini ambao haukubaliki na unapaswa kuachwa.
“Ukamataji, ukiwemo wa kuvaa mavazi ya kininja, kutovaa sare rasmi za polisi pamoja na kwenda kukamata watuhumiwa majumbani usiku, haukubaliki,” alisema waziri huyo.
Lakini Desemba 26, 2025, Waziri Simbachawene alinukuliwa tena akiweka wazi maagizo aliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, yakiwamo kuhakikisha uhusiano kati ya polisi na raia unakuwa mzuri na wananchi wawapende polisi.
“Leo hii polisi hata akipata shida unakuta watu wanashangilia. Tunataka hata polisi akipata ajali ya pikipiki, wananchi wampe pole. Ni lazima tufanye mabadiliko ya kimfumo na kiutashi. Mafunzo yetu ya Polisi lazima tuyaangalie,” alisema waziri huyo na kuongeza;
“Lazima tuzingalie, hivi tuna train (kufundisha) askari wanapokwenda kwa wananchi wakapambane na wananchi au tunawafundisha waende wakawalinde wananchi?”
Alisema lazima Jeshi la Polisi lifanyiwe mabadiliko makubwa.
