Arusha. Nani mmiliki halali wa hekari 30? Hili ndilo swali ambalo Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Arusha ilihoji kati ya Kijiji cha Slahhamo na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini.
Hata hivyo, Jaji Sylvester Kainda, katika hukumu yake, amelitamka Baraza la Wadhamini la KKKT Dayosisi ya Kaskazini kuwa wamiliki halali wa ardhi hiyo waliyogawiwa na kijiji hicho ili wajenge zahanati na chuo cha ufundi.
“Nimezingatia, miongoni mwa mambo mengine, historia ya mzozo, haja ya kudumisha amani na maelewano kati ya pande zote, hivyo nakataa kuamuru mdaiwa (kijiji) kulipa fidia ya uharibifu wowote wa jumla,” amesema Jaji.
Hukumu ya kesi ya ardhi namba 4833 ya mwaka 2024 ilitolewa Desemba 19, 2025, lakini ikapatikana katika tovuti ya mahakama (TanzLII) jana, Jumamosi Desemba 27, 2025, huku Jaji akiamuru kila upande kubeba gharama zake za kesi.
Jaji amesema kesi hiyo inatokana na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi ambao asili yake ni mabadiliko ya miundo ya utawala wa vijiji, sera ya Operesheni Vijiji ya mwaka 1970 na taratibu za kimila za ugawaji ardhi kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
“Lakini asili yake pia inahusisha ushiriki wa kihistoria wa taasisi za kidini katika kutoa huduma muhimu vijijini Tanzania,” amesema Jaji Kainda, ambapo kesi hiyo ilifunguliwa na Baraza la Wadhamini la KKKT dhidi ya halmashauri ya kijiji hicho.
“Mgogoro huu wa ardhi unaitaka mahakama hii kuzingatia kwa kina mwingiliano kati ya sheria ya ardhi, sheria za kimila, taratibu za utawala wa vijiji na ulinzi wa kikatiba wa haki za kumiliki mali,” amesema Jaji Kainda katika utangulizi wake.
Mdai katika shauri hilo ameeleza kuwa mwaka 1984 aligawiwa ardhi yenye ukubwa wa hekari 31.005 na kijiji hicho kwa ajili ya shughuli za kijamii, ikiwamo kujenga zahanati na chuo cha kutoa mafunzo ya ufundi stadi (vocational training).
Ameeleza kuwa alimiliki ardhi hiyo kwa amani kwa miaka 30 na kuiendeleza, na kwamba wadau wa jamii inayowazunguka, wakiwamo viongozi wa kijiji, walilitambua kanisa hilo la KKKT Dayosisi ya Kaskazini kuwa mmiliki halali.
Hata hivyo, mwanzoni mwa Aprili 2016 na pia mwaka 2021, kundi la wanakijiji na baadhi ya viongozi wa kijiji walivamia ardhi yao, kulima mazao kwenye sehemu ya ardhi hiyo, kukata miti 70, kuharibu majengo na kuvuruga uendeshaji wa chuo.
KKKT lilidai kuwa vitendo hivyo walivyovifanya vilikuwa ni kuingia kwa jinai na kuingilia mali za kanisa bila uhalali, licha ya kufahamu kuwa waliipata kihalali.
Wadaiwa katika shauri hilo, ambao ni halmashauri ya kijiji, walikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa ardhi hiyo inayobishaniwa ni mali ya kijiji, na kwamba KKKT Dayosisi ya Kaskazini walipewa hekari moja tu kwa ajili ya kujenga zahanati.
Hivyo, kujihusisha kwa kanisa katika ujenzi au maendeleo kulikuwa kama msimamizi (supervisor), na hakuwahi kumiliki eneo hilo, na kwamba hekari zote 31 ni mali ya kijiji tangu mwanzo na umiliki wake haukuwahi kuhamishwa kwa kanisa.
Katika usikilizwaji wa shauri hilo, mdai ambaye ni KKKT aliwakilishwa na wakili Emmanuel Safari, akisaidiana na wakili Geofrey Mollel, wakati wadaiwa waliwakilishwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Masunga Kamihanda.
Wakili huyo alisaidiana na mawakili wa Serikali, Leyani Mbise na Joseph Bundala.
Shahidi wa kwanza, ambaye ni Ofisa Sheria wa mdai, aliweka msingi wa madai ya mdai na kutoa vielelezo, ikiwamo makabidhiano ya ardhi ya mwaka 1984, na nyaraka hiyo ilikuwa na lakiri (seal) ya kijiji, majina ya viongozi na sahihi zao.
Alieleza kuwa ugawaji wa ardhi katika miaka ya 1980 haukufanyika kisasa kama ilivyo sasa, ambapo kunakuwa na hati ya umiliki, bali kupitia azimio la halmashauri ya kijiji na Kamati ya Maendeleo ya Kata husika.
Shahidi wa pili, ambaye aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO), alihudumu katika Kijiji cha Slahhamo kwa miaka 10, na katika kipindi chake cha uongozi, ardhi inayobishaniwa ilikuwa mali ya KKKT.
Alithibitisha pia kuwa hakuna mkutano wowote wa kijiji uliowahi kufuta ugawaji huo uliofanyika mwaka 1984 na kuwasilisha kielelezo P11, ambacho ni barua ya kijiji kwenda kwa kanisa wakiomba kukata miti, ikiwa ni kuthibitisha kuwa kanisa ndilo mmiliki.
Shahidi wa tatu, ambaye ni daktari mstaafu, alihusika katika mradi wa ujenzi wa zahanati na akaeleza kuwa alikuwapo wakati wa makabidhiano ya ardhi hiyo mwaka 1984, na aliwatambua saini yake aliyoiweka mwaka huo.
Alieleza kuwa ujenzi wa zahanati na chuo cha ufundi ulianza mwaka 1985 hadi 1990, ukifadhiliwa na wafadhili na jamii, na kwamba kwa miongo kadhaa hakuwahi kutokea mtu yeyote aliyepinga umiliki wa kanisa au uwepo wake.
Mashahidi wengine walikuwa ni waliowahi kuwa viongozi wa kijiji hicho, ambao walieleza namna kumbukumbu zinavyoonesha ardhi hiyo ni mali halali ya kanisa, huku mchungaji akieleza kuwa ardhi hiyo ipo katika kumbukumbu zao tangu miaka ya 1980.
Kijiji kilivyokwamia kortini
Shahidi wa kwanza wa mdaiwa, ambaye alikuwa Katibu wa Kijiji kati ya mwaka 1980 na 1988, alikana kuona nyaraka inayoonesha kanisa lilipewa ardhi hiyo na kusisitiza kuwa hakuwahi kusaini nyaraka, licha ya kukiri jina lake lipo.
Alipododoswa zaidi, alidai kuwa Desemba 11, 1984, siku mkutano mkuu wa kijiji ulipokaa, yeye hakuwepo kijijini, ingawa hakutoa ushahidi wowote wa kitabibu wala wa kiutawala kuthibitisha kuwa kweli siku hiyo hakuwepo.
Kwa mujibu wa Jaji, kuna wakati alieleza kuwa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) haikuwa na mamlaka ya kugawa ardhi, lakini baadaye akakiri kuwa mwaka 1984 vijiji vilikuwa vikitekeleza maamuzi ya maendeleo kutoka WDC.
Shahidi wa tatu, ambaye ni mzee wa kijijini, aliripoti kuwa wanakijiji walikabidhi ardhi hiyo kwa hiari kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kijamii mwaka 1980, na kuthibitisha kuwa wanakijiji walipewa ardhi mbadala walipotoa ardhi hiyo.
Alikubali kuwa zahanati na chuo cha ufundi vipo katika eneo lenye mgogoro, lakini alisisitiza kuwa ardhi hiyo ni mali ya kijiji. Hata hivyo, alipododoswa zaidi, alikubali kuwa hakuhudhuria kikao kilichogawa ardhi kwa KKKT, hivyo hajui maudhui yake.
Katika hukumu yake, Jaji Kainda amesema mashahidi wote wa mdai, kuanzia shahidi namba moja hadi nane, waliwasilisha ushahidi wa maelezo na nyaraka kuthibitisha eneo hilo ni mali yao tangu walipopewa mwaka 1984, na kwamba kuna majengo yao katika eneo hilo.
Jaji amesema mdaiwa, kwa upande wake, amesimama katika msimamo kuwa KKKT walikuwa wasimamizi tu, lakini madai hayo yanajikanganya na kielelezo P4 kinachoonesha kuwa wao ndio wenye mradi na wasimamizi.
Jaji amesema matendo ya mashahidi wa utetezi yanaonesha kutokuwa na msimamo (inconsistencies), jambo linalodhoofisha uaminifu wao, akitoa mfano wa shahidi wao wa kwanza kukana kielelezo P1 chenye jina lake.
Kwa ujumla wa ushahidi, Jaji amesema lalamiko la kuingia kwa jinai lililofanywa na mdaiwa mwaka 2016 na 2021 ni kuingilia haki ya mdai, na kwamba ushahidi wa mdai unashawishi zaidi kuliko ule wa mdaiwa, ambaye ni Serikali ya kijiji.
“Ushahidi wa mlalamikaji ni wa kina, thabiti, wenye msingi wa kihistoria na kuungwa mkono na vielelezo. Ushahidi wa mdaiwa hauendani, kwa kiasi kikubwa hauungwi mkono na nyaraka, na unapingana na uhalisia,” amesema Jaji.
Kutokana na uchambuzi huo, Jaji ametoa amri ya tamko kuwa Bodi ya Wadhamini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini ndiyo wamiliki halali wa ardhi hiyo inayojumuisha pia hekari 22, ambazo ni sehemu ya hekari 31.005 walizopewa mwaka 1984.
Pia, Jaji ametoa amri ya kuizuia Serikali ya kijiji hicho, mawakala wake, watumishi wake au mtu yeyote atakayekuwa ametumwa na mdaiwa, kuingia katika ardhi hiyo, kulima sehemu ya ardhi hiyo, kukata miti au kuondoa alama za mipaka.
Mbali na amri hiyo, Jaji ameamuru mdaiwa kutomsumbua mdai (KKKT) kwa namna yoyote katika umiliki halali wa ardhi hiyo, huku kila upande ukibeba gharama za shauri hilo.
