Mmoja afariki dunia, watatu wakipigwa na radi Tabora

Tabora. Kijana mmoja aitwaye Mwagala Malando (19),  mkazi wa kata ya Itambilo wilayani Kaliua mkoani Tabora, amefariki dunia na  wengine wawili wamejeruhiwa  kwa kupigwa na radi.

Akizungumza leo Desemba 28,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Tabora, Richard Abwao amesema watu hao wamepigwa na radi wakati wamejikinga na mvua kwenye baraza mbele ya nyumba yao.

“Walikua wamesimama mbele ya nyumba yao kuna baraza hivi iliyotengwa na mti  kwa muda wakati mvua kubwa inanyesha wakapigwa na  radi, mmoja akafariki wawili wakajeruhiwa.

Amesema waliojeruhiwa na radi hiyo ni Yohana Peter (18)  na George Deus  (18)  wote wakazi wa Kijiji cha Itambilo wilayani Kaliua, ambapo wameshapatiwa matibabu na kurejea nyumbani wakiuguza majeraha.

Kamanda Abwao amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ili kuepuka majanga kama hayo ikiwa ni pamoja na kuacha kusimama chini ya miti wakati mvua inanyesha na kuacha kutumia vitu vinavyoweza kusababishiwa shoti wakati radi inapiga.

Juma Makola mkazi wa Tabora amesema wakati mvua zikiwa kubwa Tabora kunakua na radi nyingi ambapo mara kadhaa hupiga mifugo na watu.
“Naiomba Serikali kama kuna elimu ya kujikinga na majanga ya radi wananchi wapewe ili kujikinga maana radi zinatokea mara nyingi   kila ifikapo mvua za masika Tabora lazima  baadhi ya watu au mifugo lazima  waumie na radi.”

“Yani tumeshajua kabisa ikifika masika tunaulizana safari hii atapigwa nani na radi maana Tabora radi zinaanguka sana, lakini tungejua kama kuna njia tunaweza kutumia tukaepukana na hayo majanga,kwa kweli tuelekezwe maana radi zinatuumiza sana,”amesema.

Mwajuma Seif mkazi wa Tabora, amesema kuna wakati mtu anaogopa hata kukinga maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwa sababu ya kuhofia kuumizwa  na radi,lakini pia hasara za vifaa mfano luninga zinaungua sana.

“Radi zikianza tu tunahangaika kuzima simu,kuzima tv na kila kitu tunachohisi huenda kikaleta shoti,kwa sababu tunaogopa na ndio hivyo tushaona wenzetu baadhi wamepigwa radi wameumia wengine wamefariki dunia wameacha familia zinahangaika”amesema Mwajuma.