Kiwango cha Che Malone chamuibua kocha Simba

KIWANGO cha beki wa zamani wa Simba, Fondoh Che Malone katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, imemuibua kocha aliyewahi kumnoa akiwa Msimbazi, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, aliyesema bila kuuma maneno kwamba Wekundu hao walizingua kumuacha.

Che Malone na Robertinho walifanya kazi pamoja msimu wa 2022-2023 ambapo iolishuhudia Simba ikapasuliwa mabao 5-1 na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu, kabla ya kila mmoja kuondoka kivyake, kocha akiondoka baada ya kipigo hicho cha Novemba 5, 2023 na beki huyo kuondoka msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho amesema beki huyo ameendelea kuonyesha kiwango bora kuanzia timu anayoichezea hadi sasa katika timu ya taifa ya Cameroon.

Robertinho mwenye uraia wa Brazili, amesema Che Malone ni beki wa daraja la juu ambaye bado alihitajika kulindwa ndani ya Simba ili aendelee kufanya vizuri.

“Che Malone amelinda hadhi yake hatua ya kutoka Simba na kuendeleza ubora akiwa Algeria na timu ya taifa hadi sasa ni beki bora kuliko mabeki wengine wote waliopo Simba kw sasa.

“Moja ya faida yake kubwa ni beki anayeweza kuwa kiongozi mzuri kwa wenzake makosa ya uwanjani ambayo Che Malone alikuwa akifanya bado hayaondoi ubora wake na hakuna mchezaji anayeweza kucheza kwa muendelezo mmoja duniani akisema hiyo ilikuwa kazi ya makocha kumrekebisha.”

Che Malone aliondoka Simba mwishoni msimu uliopita na kutimkia USM Alger ya Algeria amekuwa miongoni mwa mabeki wanaocheza kikosi cha kwanza kuanzia timu ya taifa mpaka hii ya sasa.

Katika mechi ya kwanza ya AFCON iliyozikutanisha Cameroon iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gabon, Malone alikiwasha mwanzo mwisho kwa dakika 90 kwa kiwango bora akishirikiana na wenzake.