Mvua ya siku mbili yaacha kilio, neema

Dar/Mikoani. Mvua iliyonyesha kwa takribani siku mbili maeneo kadhaa nchini, imesababisha uharibifu wa miundombinu, nyumba kuzingirwa maji na kuathiri safari za treni ya reli ya kisasa (SGR), lakini zikiwa neema kwa baadhi ya sekta.

Desemba 26,2025 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitoa angalizo kuhusu uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Morogoro, Lindi na Mtwara.

Vilevile, Desemba 27 na 28, mamlaka hiyo ilitoa tahadhari kuwa, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Kigoma, Katavi, Tabora, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja.

Kwa Desemba 29, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa kwa maeneo machache ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema wanaendelea kufuatilia na kufanya tathimini ya athari za mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha maeneo mengi wilayani humo usiku wa kuamkia leo Desemba 28.

Amesema hakuna taarifa za madhara ya kibinadamu licha ya nyumba kujaa na kuzingirwa na maji.

“Usiku wa kuamkia leo imenyesha mvua kubwa katika maeneo mengi ya Manispaa ya Morogoro, yakiwamo ya kata za Lukobe na Kihonda. Nafuatilia kujua kama kuna madhara ya kibinadamu,” amesema.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo, amesema: “Maeneo mengi ya Kihonda na Lukobe yalikuwa yamejaa maji, baadhi ya nyumba zilizingirwa na maji kwa muda mfupi baadaye maji yalipotea. Leo (Desemba 28) kama itanyesha kubwa kama ya jana usiku inaweza kuleta madhara kwa sababu ardhi itakuwa imeshiba maji.”

Mariamu Juma, ambaye nyumba yake imezingirwa na maji amesema mvua ilianza saa tisa usiku hadi alfajiri, hivyo maji yalijaa ndani na kuharibu vitu.

Amesema aliokoa watoto wake wawili waliokuwa wamelala chumba cha nje ambacho nacho kilijaa maji. Baada ya mvua kukata anaeleza maji yalipungua.

Aziz Habibu, mkazi wa Kihonda, amesema walilazimika kuwa macho hadi alfajili mvua ilipokatika.

“Nilishawahi kuathirika na mafuriko ya mwaka 2023 maji yalivunja ukuta na kuingia ndani, nilipoteza kila kitu kilichokuwapo ndani na nililazimika kuihama nyumba yangu. Mwaka huu niliamua kurejea, lakini kwa mvua iliyonyesha usiku nimeanza kupata wasiwasi na sasa naishi kwa tahadhari,” amesema.

Wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wananchi wanaendelea kurejebisha makazi yao baada ya kuathiriwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali Desemba 26, 2025.

Diwani wa Magole, Aziz Omary, amesema miundombinu ya umeme na maji iliyoharibiwa na mvua imeanza kurekebishwa, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Miundombinu ya barabara za mitaani imeharibika na bado mvua ndogondogo zimeendelea kunyesha,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, Desemba 27, alisema mvua imeathiri zaidi Tarafa ya Magole, kata za Dumila na Mgaole, ambako kwa tathmini ya awali zaidi ya nyumba 120 zimeathiriwa, ikiwamo kuezuliwa paa, kuporomoka kwa kuta na nyingine kubomoka kabisa.

Alisema hizo ni takwimu za awali na kwamba, kamati ya maafa ya wilaya inaendelea na tathmini ya kina ili kupata idadi sahihi ya nyumba na wananchi walioathirika, pamoja na kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa na maafa hayo.

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeeleza changamoto za kiufundi zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha ratiba ya safari kwa abiria wa reli ya kisasa (SGR) kuvurugika Desemba 28, 2025.

Akizungumza na Mwananchi saa 6:24 mchana wa Desemba 28, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema mvua zimesababisha hitilafu za kiufundi ambazo zinashughulikiwa na mafundi wa shirika hilo.

“Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, changamoto ya kiufundi imejitokeza na tunaifanyia kazi. Juhudi zinaendelea na muda si mrefu safari zitaanza. Tatizo hili liko nje ya uwezo wetu kwa kuwa mvua zimetuathiri,” amesema.

Masanja amesema athari kubwa zaidi zimeikumba reli ya zamani (MGR), ambayo baadhi ya miundombinu imeharibika, yakiwamo madaraja katika eneo la Gulwe, mkoani Dodoma na Kilosa, mkoani Morogoro.

Kwa upande wa treni ya SGR, amesema athari si kubwa na mafundi wanaendelea na ukaguzi wa kina ili kuhakikisha usalama kabla ya kuruhusu safari kuendelea.

“Hatuwezi kuruhusu treni kupita bila kujiridhisha kuwa njia ni salama. Tunafanya ukaguzi wa kina na kufikia hatua ya mwisho ya kuruhusu safari kuanza. Kikubwa tunawaomba abiria waendelee kutuamini, kwani lengo letu ni kutoa usafiri bora, wa uhakika na salama,” amesema.

Masanja amesema safari za SGR zitaendelea kama kawaida baada ya ukaguzi kukamilika, huku juhudi zikiendelea kurejesha huduma kwa haraka kwenye reli ya zamani iliyoathiriwa na mvua.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, amesema mvua zinazoendelea kunyesha nchini hazijasababisha changamoto kubwa ya utoaji wa huduma ya umeme.

Amesema mvua hizo ni neema kwa Tanesco, hususani kwa maeneo yanayozalisha nishati hiyo kwa kutumia maji kupitia mabwawa.

“Maji yanaendelea kutiririka vizuri kwenye mabwawa yetu, hivyo tunamshukuru Mungu kwa neema ya mvua. Tunaendelea kufuatilia hali hiyo na endapo kutajitokeza changamoto yoyote tutatoa taarifa kwa umma,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire, amesema kiwango cha maji katika vyanzo vinavyotegemewa kwa uzalishaji kimerudi katika hali yake ya kawaida.

Amesema kwa sasa Dawasa inaendelea na uzalishaji wa maji kama ilivyokuwa awali, akibainisha kuwa Desemba 29, uongozi wa mamlaka utafanya ziara katika vyanzo vya maji kujionea hali halisi.

Akijibu swali iwapo mgawo wa maji utaisha, Bwire amesema upatikanaji wa maji katika vyanzo ni jambo moja, huku kuwafikishia wananchi huduma hiyo ikiwa ni mchakato mwingine unaohusisha hatua mbalimbali.

“Suala la maji kuwepo mtoni ni jambo moja na kuwafikia wananchi huduma ya maji ni jambo lingine,” amesema.

Ameeleza baada ya maji kupatikana katika vyanzo, kuna hatua za kuyasafisha, kuyasafirisha na hatimaye kuyasambaza kwa wateja, mchakato unaohitaji muda na miundombinu.

Mkoani Manyara, sehemu ya daraja linalounganisha Shule ya Msingi Landanai wilayani Simanjiro na makazi ya jamii limeathiriwa na mvua. Daraja hilo linatumiwa na wanafunzi na walimu wa shule hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala ametoa tahadhari kwa wakazi wa eneo hilo kuwa waangalifu kipindi hiki cha mvua, akisema ameshatoa maagizo kwa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) kuchukua hatua za kutengeneza miundombinu uharibifu unapojitokeza.

Mkoani Iringa mvua imenyesha na kusababisha kuwapo utelezi, baadhi ya wananchi wakisema imesaidia kuondoa vumbi.

Mkoani Tabora, watu wanne akiwamo mjamzito walisombwa na maji katika Kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora wakiwa kwenye bajaji, kutokana na mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa tano usiku wa kuamkia Desemba 28.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Loshpay Laizer, amesema dereva alipuuza maji yanayotembea, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari.

“Maji yametuama maeneo mengi, lazima tuendelee kuchukua tahadhari ili tusiendelee kuwa na madhara kwa watu yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha,” amesema.

Dereva wa bajaji iliyosombwa, Abdurahmani Kipusi, amesema alijua maji siyo mengi lakini mwisho wa siku baada ya kuvuka barabara alisombwa alipokuwa akimpeleka hospitali mjamzito.

Mkoani Mbeya wakulima, akiwamo Witness Kamwela, amesema kunyesha mvua kunawapa nafasi ya kuanza kuandaa mashamba na kupanda mazao.

Kamati ya maafa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Shaka Hamdu Shaka, ikifanya tathmini ya athari za mvua kubwa iliyo ambatana na upepo mkali. Picha na Jackson John

Jijini Dar es Salaam, watumiaji wa barabara ya Kitunda hadi Msongola, Wilaya ya Ilala, wamelalamikia adha ya usafiri kutokana na madimbwi makubwa ya maji barabarani yaliyotokana na mvua zilizonyesha.

Dereva wa bodaboda, Paul Stephano amesema: “Changamoto hapa Kitunda ni kubwa, kuna madimbwi ya maji yanatutesa waendesha bodaboda, madimbwi ni mengi, watu wanakwama, wengine hawawezi hata kuvuka.”

Amesema wakati mvua baadhi ya watu hubebwa ili kuvuka madimbwi kwa kutozwa Sh500 kulingana na hali ya maji.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda na Devotha Kihwelo (Dar), Hamida Shariff na Jackson John (Morogoro), Christina Thobias (Iringa), Hawa Mathias (Mbeya), Joseph Lyimo (Simanjiro) na Hawa Kimwaga (Tabora)