Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imewaachia huru raia wawili wa Kenya, Titus Mutisya na Benard Musili, waliohukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Awali, walishtakiwa kwa makosa mawili ya kumiliki nyara ya Serikali kinyume cha sheria wakidaiwa kukutwa na meno ya tembo yenye uzito wa kilo 4.84 yenye thamani ya Dola za 2,904 za Marekani.
Kosa la pili walidaiwa kuingia katika hifadhi ya taifa kinyume cha sheria, ikielezwa Mei 30, 2022 walikutwa katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, eneo la Kimengelia, wilayani Rombo.
Hawakuridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama ya chini iliyowahukumu kifungo cha miaka 20 jela, hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu kuipinga.
Uamuzi wa rufaa umetolewa Desemba 23, 2025 na Jaji Lilian Mongella, aliyebatilisha hukumu hiyo akieleza upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi bila kucha shaka.
Amesema Jamhuri ilishindwa kumuita mpelelezi mkuu wa kesi hiyo kutoa ushahidi.
Katika mahakama ya chini, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo saba ili kuthibitisha kesi.
Ilidaiwa Mei 30, 2022 saa 10:00 jioni shahidi wa pili, Abraham Mbaga na wenzake wakiwa doria waliwaona washtakiwa (warufani) wakiwa wamebeba mabegi migongoni.
Alidai baada ya kuwakamata na kujitambulisha, waliowaomba nao wajitambulishe, kisha wakawapekua mbele ya shahidi wa tano na watu wengine wawili.
Katika upekuzi, alidai mrufani wa kwanza alikuwa na begi la rangi ya kahawia mgongoni, ambamo ndani kulikuwa na meno yaliyochongwa yaliyodhaniwa ni ya tembo.
Alidai yalikuwa yamechongwa kuwa na taswira ya mwanamume wa Kimasai na juu kulichongwa taswira za watu wawili waliokuwa wamekaa wakiwa wamebeba vyungu.
Ilidaiwa mrufani wa pili alikutwa na mfuko mweusi mgongoni ambao ndani kulikuwa na jino lililochongwa likihisiwa kuwa la tembo. Lilichongwa kwa taswira ya Mmasai aliyevaa hereni na picha ya watu wawili wakiwa wameketi kwenye vyungu.
Shahidi alidai aliwahoji iwapo wana vibali vya kumiliki nyara za Serikali, wakajibu hawakuwa navyo, hivyo akajaza cheti cha kukamatwa, ambacho alisaini yeye, warufani na mashahidi wengine kisha akawapeleka Kituo cha Polisi Tarakea, Rombo wakiwa meno hayo.
Shahidi alidai vielelezo hivyo alimkabidhi shahidi wa kwanza, Koplo Olias, ambaye aliviweka alama na namba ya kesi.
Mei 31, 2022 alifanya kazi kwa maagizo ya mpelelezi wa kesi hiyo, Koplo Dickson ambapo vielelezo hivyo vilikabidhiwa kwa shahidi wa tatu, Ismail Walale ili afanye utambuzi na uthamini.
Shahidi wa tatu alidai baada ya kufanya utambuzi, aliona sifa ambazo kwa kawaida hupatikana kwa meno ya tembo ikiwamo kimuundo, mifupa imara na rangi. Kwa kuzingatia uchunguzi huo, aliridhika kwamba ilikuwa ni meno ya tembo.
Alidai katika tathmini alibaini meno hayo yalikuwa na uzito wa kilo 4.84. Moja lililoandikwa K lilikuwa na uzito wa kilo 2.4 na lingine lenye alama K1 lilikuwa na uzito wa kilo 2.44.
Alidai thamani yake kwa siku hiyo ilikuwa Dola 600 kwa kilo moja, hivyo ikawa jumla ya Dola 2,904 (Sh6.75 milioni) kwa kilo zote 4.84.
Katika utetezi wao warufani (washtakiwa) walikana kutenda kosa hilo.
Titus alidai siku ya tukio akiwa njiani kutoka Nairobi kuelekea soko la Athiriver, alikutana na mrufani wa pili ambaye ni mfanyakazi wake.
Alidai walikwenda kituo cha mabasi na kupanda gari hadi eneo la Emali ambako walikutana na dalali aliyemweleza ana Sh180,000 za Kenya kwa ajili ya ununuzi wa vitunguu, kisha wakaelekea eneo la Kimana.
Alidai dalali aliwaeleza kuwa muuzaji wa vitunguu alikuwa sokoni, hivyo walikwenda mgahawani kunywa chai.
Wakiwa huko, dalali alilalamika kuhusu maumivu ya tumbo, hivyo akaondoka kwenda chooni alikokaa kwa takribani dakika 10 kisha akarudi.
Alidai aliporejea aliwaeleza muuzaji anakuja, baada ya muda gari dogo aina ya saloon lenye rangi ya bluu lilifika likiwa na watu watatu ndani. Dereva alimweleza haliwezi kubeba watu zaidi ya watano.
Alidai dalali alipanda pikipiki, wao na watu wengine watatu wakapanda gari wakaondoka. Dakika 10 baadaye walikutana na gari aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa limeegeshwa.
Alidai kulikuwa na watu wanne waliosimama nje ya gari hilo. Dereva wa gari walimokuwamo alisimama, mtu aliyekuwa ameketi mbele akafungua mlango na kuwaambia hiyo ndiyo ilikuwa biashara na walipaswa kushirikiana.
Alieleza namna walivyosafirishwa hadi Kituo cha Polisi Tarakea na baadaye Mkuu, Rombo na kufikishwa mahakamani kwa kupatikana na meno ya tembo yenye thamani ya Sh34.89 milioni na kuingia hifadhini bila kibali.
Warufani (washtakiwa) walikana mashtaka wakidai walikamatwa nchini Kenya na si Tanzania.
Februari 7, 2023 upande wa mashtaka ulieleza uchunguzi ulikuwa umekamilika na kuomba kubadili hati ya mashtaka.
Alidai walisomewa mashtaka mapya ya kupatikana na meno mawili ya tembo yaliyong’arishwa yenye uzito wa kilo 4.84 yenye thamani ya Dola 2,904 (Sh6.75 milioni) na kuingia hifadhini bila kibali.
Februari 14, 2023 alidai upande wa mashtaka ulifuta shtaka hilo na mahakama ikawaachilia huru, ila walikamatwa na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi na Februari 15, 2023, walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi walikofunguliwa mashtaka.
Baada ya mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, iliwatia hatiani na kuwahukumu kwa makosa yote mawili.
Katika kosa la kwanza walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kosa la pili kifungo cha miezi sita, adhabu ambazo zinatumikiwa kwa pamoja.
Katika rufaa, walikuwa na sababu 12 za kupinga kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo, akiwamo upande wa mashtaka kushindwa kuwaita au kuwaonyesha mashahidi muhimu zaidi katika kesi bila sababu za kutosha.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama Kuu ilibainisha kutoitwa mpelelezi wa kesi kuliacha maswali muhimu bila majibu, yakiwamo masuala ya kubadilishwa kwa shtaka, tofauti katika ushahidi wa mashahidi na mazingira halisi ya ukamataji na uthamini wa nyara hizo.
Mahakama imeeleza katika kesi nzito za jinai, hususani zinazohusu nyara za Serikali, mpelelezi ni shahidi wa msingi na ushahidi wake huwa muhimu ili kuondoa shaka inayoweza kujitokeza.
“Katika kesi warufani waliibua masuala kadhaa ambayo yanazua maswali yasiyo na majibu, ikiwamo ubadilishaji wa shtaka. Mwanzoni walishtakiwa kwa nyara za Serikali zenye thamani ya Sh34.89 milioni kisha Sh6.75 milioni. Utetezi wa warufani ulikuwa kwamba kesi hiyo ilikuwa ya uongo ndiyo maana upande wa mashtaka uliendelea kubadilisha maelezo ya kosa,” amesema na kuongeza:
“Zingatia nyara zinazozungumziwa kama kweli zilikuwa meno ya tembo yaliyochongwa kwa nakshi za Kimasai, ingawa zilielezwa na ofisa aliyefanya utambuzi na uthamini, mpelelezi aliyemtafuta ofisa huyo na anayedaiwa kuwepo wakati wa mchakato mzima alikuwa muhimu kuthibitisha ushahidi wa ofisa wa uthamini.”
Kutokana na upungufu huo, mahakama imesema kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa bila kuacha shaka, hivyo kuruhusu rufaa hiyo, kufuta hukumu na kuamuru warufani kuachiwa isipokuwa kama wameshikiliwa kwa sababu nyingine halali.
