Dar es Salaam. Mwaka 2025 umeweka wazi jeraha lisiloonekana, lakini lenye maumivu makali la afya ya akili miongoni mwa Watanzania.
Katika kipindi cha mwaka huu, kumeshuhudiwa ongezeko la matukio ya msongo wa mawazo, sonona, wasiwasi mkubwa na tabia za kujidhuru.
Makundi yaliyoathirika zaidi ni vijana na wanafunzi, wafanyakazi wa mijini, pamoja na wanawake wanaobeba mzigo mkubwa wa kiuchumi na kijamii.
Matumizi ya huduma za kidijitali za afya ya akili yaliongezeka, hasa miongoni mwa vijana na watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao walikuwa wakitafuta msaada kupitia majukwaa mbalimbali kwa sababu ya changamoto ya upatikanaji wa huduma za kawaida.
Watanzania wengi walikuwa wakishiriki uzoefu wa changamoto za afya ya akili kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram na TikTok, ikionyesha ongezeko la mjadala kuhusu msongo wa mawazo, wasiwasi na afya ya akili kwa ujumla.
Hii ilijumuisha maelezo ya walengwa kuhusu jinsi mitandao inavyowasababishia au kuwasaidia kutafuta msaada.
Hata hivyo, licha ya dalili kuongezeka ukimya na unyanyapaa uliendelea kuwafanya wengi kuficha hali zao kwa hofu ya kuitwa wagonjwa wa akili au dhaifu.
Kutokana na hali hiyo, imekuwapo changamoto ya watu kujiua, hasa miongoni mwa vijana na suala hili limekuwa likishutumiwa kuwa tatizo kubwa la afya ya akili.
Serikali ilitangaza kwamba kujiua imekuwa sababu kuu ya vifo miongoni mwa vijana wa umri wa 15–29 mwaka 2025. Kila kifo cha kujiua kuna majaribio mengi zaidi ya kujiua kati ya vijana wengine.
Julai, 2025 yaliripotiwa matukio mawili ya vijana kujiua mmoja akiwa mfanyabiashara na mwingine daktari wa watoto ambayo yote yalitokea mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Ronald Malisa (35) ambaye alikuwa mfanyabiashara Moshi na Dodoma alidaiwa kujiua kwa kujinyonga katika choo cha nyumba yake.
Ilielezwa tukio hili lilitokea Julai 10 chanzo ni msongo wa mawazo na mara kadhaa alishajaribu kutaka kujiua kwa kunywa sumu ila alikuwa akiokolewa na wanafamilia.
Siku hiyohiyo lilitokea tukio lingine ambapo Magreth Swai, aliyekuwa daktari bingwa wa watoto naye alijinyonga.
Ripoti za Wizara na wataalamu wa afya zilitaja sababu kadhaa zinazoendelea kuchangia tabia ya kujiua, ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo, migogoro ya kifamilia, ukosefu wa ajira, na unyanyasaji.
Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Jeshi la Polisi, unaonyesha vifo 1,141 vilivyotokana na kujiua vilitokea nchini kuanzia Januari 2024 hadi Juni 2025, huku wanaume wakiongoza kwa asilimia kubwa.
Akizungumza Septemba 10, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mirembe, Dk Paul Lawala alisema idadi hiyo ni kubwa na inazidi kuongezeka siku hadi siku, hivyo mamlaka zinazohusika zichukue hatua za haraka.
Dk Lawala alisema Hospitali ya Mirembe baada ya kuona idadi ya matukio ya watu kutaka kujiua, kutishia kujiua na kujiua yameongezeka waliamua kufanya utafiti kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kupata idadi hiyo ya watu kujiua katika kipindi cha miezi 18.
Alibainisha changamoto ya watu kujiua inashika nafasi ya tatu nchini kwa kusababisha vifo, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anajiweka mbali na visababishi vya kujitoa uhai ikiwamo ulevi kupindukia, sonona, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na magonjwa sugu.
Ripoti na simulizi za mwaka mzima zinaonyesha sababu kuu zinazoathiri afya ya akili, ni kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na uhakika wa kipato hasa kwa vijana.
Msongo wa kazi katika sekta ya umma na binafsi, pamoja na athari za mitandao ya kijamii, ikiwamo mashindano ya maisha na unyanyasaji wa mtandaoni. Haya yote yameunda mazingira ya shinikizo la kudumu, bila mifumo imara ya msaada.
Wataalamu wa afya walizungumzia hili kwa kina wakisema kulinda na kuboresha afya ya akili si jambo la hiari tena, bali ni hitaji la msingi kwa kila mtu.
Mtaalamu wa saikolojia tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Isaack Lema, alisema mtu anaweza kuchukua hatua mbalimbali katika maisha ya kila siku kulinda afya yake ya akili.
Alisema ni muhimu kila mtu kujiuliza namna anavyokabiliana na changamoto za kila siku, jinsi anavyotambua na kuonyesha hisia zake na kama ana uwezo wa kujizuia kutoa kauli hasi au kukasirika kwa wepesi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili (Mirembe), Dk Godfrey Mkama, anaongeza kuwa mtu anapaswa kuwa wazi kuhusu hisia zake, kupata usingizi wa kutosha, kula mlo kamili, kushughulisha mwili, kuishi kwa kuzingatia wakati uliopo na kufurahia kile kinachotokea katika maisha yake kwa sasa.
Anasisitiza kuwa kushirikiana na watu wenye mitazamo chanya, kujali wengine, kuboresha uhusiano wa kifamilia, kuondoa kinyongo na kujitolea ni njia muhimu za kuimarisha afya ya akili.
Mwaka 2025 umebainisha changamoto kubwa, upungufu wa wanasaikolojia na wanasaikatria, huduma kujikita katika hospitali chache, na afya ya akili kukosa bajeti na kipaumbele stahiki. Kwa wananchi wengi, huduma zimeendelea kuwa ghali, mbali na zisizoeleweka.
Pamoja na changamoto, hatua chanya zimejitokeza. Kampeni za uhamasishaji zimeongezeka, viongozi na watu maarufu wameanza kuzungumza wazi, na mashirika ya kiraia yameanzisha msaada wa kisaikolojia kwa vijana na wanawake.
Zaidi ya hayo, Wizara ya Afya imetenga bajeti ya Sh1.62 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 itakayosaidia pia huduma za afya ya akili kama sehemu ya vipaumbele vya sekta ya afya.
Katika hotuba ya bajeti iliyosomwa na marehemu Jenista Mhagama (aliyekuwa Waziri wa Afya) ilibainisha mojawapo ya vipaumbele ni kuimarisha huduma za afya ya akili, pamoja na huduma zingine maalumu za afya kwa makundi kama ya watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Hii ilionyesha kwamba bajeti imepangwa si tu kwa huduma za matibabu ya kawaida bali pia kwa huduma za msingi za afya ya akili zinazojumuishwa katika mfumo wa afya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, programu za kuimarisha huduma za afya ya akili zinahusishwa na mikakati ya jumla ya kuingiza huduma hizi katika ngazi za kiafya, ikilenga kutolewa pamoja na huduma nyingine za afya.
Afya ya akili mwaka 2025 imejitokeza kama kioo cha maisha ya Watanzania, shinikizo la kiuchumi, mabadiliko ya kijamii na mifumo dhaifu ya msaada.
Matukio yaliyoambatana na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 yameacha alama isiyofutika, yaliingiza baadhi kwenye msongo wa mawazo hasa kufuatia kuzimwa kwa intaneti na hata ilipowashwa tatizo liliongezeka zaidi miongoni mwao na wengi kupata kiwewe.
Wataalamu wengi walitumia nafasi hiyo kusaidia jamii wakiungana na vyombo vya habari ili kuwafikia kwa urahisi, hii ilionyesha kwamba kupuuza afya ya akili kuna gharama kubwa za kijamii na kibinadamu.
Wito unabaki wazi kuvunja ukimya, kupambana na unyanyapaa na kujenga mifumo imara ya huduma kabla majeraha yasiyoonekana hayajageuka majanga yanayoonekana.
