KLABU ya Namungo iko katika hatua za mwisho za kuachana na beki wa kati wa kikosi hicho, Mghana Daniel Amoah, baada ya kudaiwa benchi la ufundi la kikosi hicho haliko tayari kuendelea naye, kufuatia mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika.
Nyota huyo alijiunga na Namungo Desemba 15, 2024, akitokea Azam na kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine mmoja, japo taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza hatoongezewa na ataachwa dirisha hili dogo.
Mtoa taarifa huyo aliliambia Mwanaspoti Amoah ni miongoni mwa mabeki wazoefu katika Ligi Kuu Bara, japo kwa mwaka mmoja aliokitumikia kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, wamefikia makubaliano ya kuachana na hawatamuongezea mkataba mpya.
“Tumefikia makubaliano ya pande mbili ya kutomuongezea mkataba mpya ila, tunashukuru sana kwa mchango wake mkubwa ambao ameuonyesha kwetu na sisi tunamtakia pia kila la heri katika maisha yake mapya nje ya Namungo,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, amesema wanasubiri ripoti ya benchi la ufundi ndipo wafanye uamuzi wa mwisho wa kujua ni maboresho ya aina gani yanapaswa kufanyik.
Nyota huyo anayecheza beki wa kati na kulia kwa ufasaha, alitua nchini kwa mara ya kwanza na kujiunga na Azam, Agosti 5, 2016, baada ya mabosi wa matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam kuvutiwa naye uwezo wake akiwa na Medeama ya kwao Ghana.
Amoah aliyeitumikia Azam kwa misimu minane kuanzia Agosti 5, 2016 hadi Desemba 15, 2024, alijiunga na kikosi hicho baada ya kuonyesha kiwango bora, katika mechi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Yanga iliyopigwa, Julai 16, 2016.
Katika mechi hiyo ya makundi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliisha kwa sare ya 1-1, ambapo Yanga ilipata bao kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya pili tu, huku Medeama ikisawazisha dakika ya 17, lililofungwa na Bernard Ofori.
