Dodoma. Jeshi la Uhamiaji nchini limetangaza nafasi mpya za ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Desemba 29, 2025, kupitia kurasa rasmi za jeshi hilo, ajira hizo zinawalenga vijana wenye sifa kuanzia elimu ya kidato cha nne, stashahada, astashahada hadi shahada.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa waombaji watakaopata kipaumbele ni wale wenye elimu ya astashahada, stashahada ya juu na shahada, waliomaliza masomo katika vyuo vinavyotambulika na kuthibitishwa na Serikali kupitia mamlaka husika.
Ajira hizo zinahusisha fani mbalimbali zikiwemo lugha za kimataifa, uhusiano wa kimataifa, sheria, uchumi, saikolojia, ufundi umeme, ufundi wa viyoyozi (AC), ufundi wa magari, udereva pamoja na wenye ujuzi wa bendi ya muziki wa ala (brass band).
Taarifa hiyo imesainiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini, Dk Anna Makalala, kwa mujibu wa Kanuni Namba 11(1) ya Uendeshaji wa Uhamiaji ya mwaka 2018.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waombaji wa elimu ya kidato cha nne wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, wenye afya njema ya mwili na akili, wenye ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Tatu, wasiokuwa na kumbukumbu za uhalifu, wasiooa au kuolewa, na wenye umri kati ya miaka 18 hadi 22.
Masharti mengine ni kutokuwa na alama za kuchora mwilini (tattoo), kutotumia dawa za kulevya, kuwa tayari kuhudhuria hatua za awali za usaili, pamoja na kuwa na Kitambulisho cha Taifa au Namba ya Utambulisho iliyotolewa na kuthibitishwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kwa waombaji wa ngazi ya astashahada na shahada, wanatakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 25, huku waombaji wenye Shahada ya Juu wakitakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 30.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia Mfumo wa Ajira wa Jeshi la Uhamiaji, unaopatikana katika tovuti ya https://www.immigration.go.tz, kuanzia leo Jumatatu, Desemba 29, 2025 hadi Januari 11, 2026.
Waombaji wanatakiwa kuambatanisha barua ya maombi iliyoandikwa kwa mkono, barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa, kijiji au shehia. Kwa waombaji waliopo katika Makambi ya JKT au JKU, wanapaswa kuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwa Mkuu wa Kambi husika.
Aidha, waombaji wanapaswa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa, pamoja na namba za vyeti vya ufaulu wa Kidato cha nne na kidato cha sita.
Kwa waombaji wa ngazi ya stashahada, astashahada na shahada au shahada ya Juu, wanatakiwa kuwa na namba ya utambuzi inayotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), pamoja na vyeti vya usajili wa kitaaluma kwa fani zinazohitaji usajili wa bodi husika.
Jeshi la Uhamiaji limeonya kuwa litachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu katika mchakato huu wa ajira, na kuwakumbusha waombaji kuepuka watu wanaodai au kuomba rushwa wakiahidi kuwasaidia kupata ajira.