TRC yaongeza safari za SGR baada ya usumbufu kwa abiria

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanzisha safari za ziada za Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kuwahudumia abiria walioathirika na usumbufu wa safari uliotokea jana, Desemba 28, 2025.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelezo ya Wizara ya Uchukuzi kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha athari katika miundombinu ya SGR na barabara, hali iliyoathiri ratiba za usafiri na kutishia usalama wa wasafiri.

Taarifa ya wizara hiyo kwa umma ilitolewa jana wakati huduma za SGR tayari zilikuwa zimeathirika, baada ya baadhi ya abiria kushindwa kuanza safari zao kwa mujibu wa ratiba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, treni iliyopaswa kuondoka saa 12:00 asubuhi ilikwama katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, na hadi saa 6:24 mchana haikuwa bado imeanza safari.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa mvua zitaendelea kunyesha leo, Desemba 29, 2025, katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma leo, Desemba 29, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa TRC, Fredy Mwanjala, amesema kuanzishwa kwa safari za ziada ni hatua ya kupunguza usumbufu uliowakumba abiria na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

“Shirika linaomba radhi kwa abiria wote wanaotumia huduma za reli za MGR na SGR kufuatia usumbufu uliojitokeza jana. Ratiba ya treni za SGR leo Desemba 29, 2025 itaendelea kama ilivyopangwa, huku safari za ziada zikiongezwa kutokana na changamoto zilizojitokeza,” amesema Mwanjala.

Kwa mujibu wa Mwanjala amesema, safari za SGR kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam zitakuwa saa 11:15 alfajiri, saa 12:00 asubuhi (EMU), saa 8:15 mchana, saa 9:00 mchana (EMU), saa 11:15 jioni, saa 12:00 jioni (EMU) na saa 12:40 jioni.

Safari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma zitakuwa saa 12:00 asubuhi, saa 1:00 asubuhi, saa 2:00 asubuhi (EMU), saa 3:30 asubuhi, saa 4:30 asubuhi (EMU) na saa 12:55 jioni.

Pia, safari kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam itafanyika saa 3:50 asubuhi, huku safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikipangwa kuondoka saa 10:00 jioni.

Mwanjala amesema kuwa TRC itaendelea kuboresha huduma na kuchukua hatua stahiki ili kuzuia kujirudia kwa usumbufu kama huo siku zijazo.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa TRC, Machibya Masanja, amesema shirika hilo limeongeza safari za treni kwa siku ya leo pekee, ili kuwahudumia abiria waliokumbwa na changamoto ya kushindwa kusafiri jana.

Masanja amefafanua kuwa ratiba ya kawaida ya treni bado inaendelea, huku safari za ziada zikiongezwa ili kuongeza uwezo wa kubeba abiria.

“Imetulazimu kuongeza treni za ziada, zikiwemo baadhi kufungwa mabehewa mawili mawili, ili kubeba abiria wengi zaidi na kuwaondolea adha waliyoipata jana,” amesema.

Kwa upande wa abiria wa reli ya zamani ya MGR, Masanja amesema changamoto bado zinaendelea kushughulikiwa, huku sababu kubwa ikiwa ni uharibifu wa madaraja mawili. Ameeleza kuwa timu ya mafundi ipo maeneo husika ikiendelea na matengenezo.

“Tukikamilisha matengenezo tutatoa taarifa ya kurejesha huduma. Sehemu kubwa iliyoathirika ni madaraja, na kuyarekebisha kuna changamoto zake, lakini tayari tumeanza kazi ikiwemo daraja la Gulwe ambalo tathmini yake imekamilika na halitachukua muda mrefu,” amesema.

Amesisitiza kuwa lengo la TRC ni kuhakikisha reli zote zinafanya kazi kwa ufanisi, ili wananchi wasafiri kwa uhakika bila usumbufu.

Kutokana na changamoto kujirudia kila msimu wa mvua, Masanja amesema TRC imepanga kujenga mabwawa katika maeneo ambayo reli ya MGR inapita, hasa mabondeni na karibu na mito mikubwa.

 “Tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa. Lengo si kuzuia maji pekee, bali pia kuwawezesha wananchi kutumia maji hayo kwa shughuli za kilimo na uzalishaji,” amesema.

Ameongeza kuwa mabwawa hayo yatasaidia kupunguza athari za mafuriko na kuwawezesha wananchi kunufaika na kilimo cha umwagiliaji, ikiwemo katika Bonde la Kilosa.

“Tunataka wakulima walime mazao ya mboga na TRC tutawasaidia kuyasafirisha kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine. Sambamba na hilo, tutaanzisha programu ya utunzaji wa mazingira kwa kushirikiana na jamii ili kukabiliana na tatizo la mabonde kujaa mchanga,” amesema.