Dar es Salaam. Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Mahusiano kwa kushirikiana na Kampuni ya Kampuni ya Target Tours and Labour Surply Company Limited, imetangaza fursa za ajira kwa madereva wa pikipiki katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali leo Jumatatu Desemba 29, 2025, nafasi hizo ni kwa ajili ya vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki zikiwemo kuwa na umri kati ya miaka 20 hadi 37, pamoja na leseni ya udereva wa pikipiki katika madaraja ya A, A1 na A3.
Taarifa hiyo pia, inataja sifa zingine muhimu kwa waombaji wa fursa hiyo kuwa ni uzoefu usiopungua miaka miwili katika kazi ya uendeshaji pikipiki, mwenye elimu ya msingi au sekondari na awe na uwezo wa kuzungumza na kuandika lugha ya Kiingereza.
“Mwombaji anapaswa kuwa mwanaume mwenye leseni ya udereva wa pikipiki na hati ya kusafiria,” imeeleza taarifa hiyo.
Ajira hizo ambazo zitakuwa chini ya Tasisi yaVelo Logistics Delivery services LLC huko UAE, zimeelezwa kuwa zitatolewa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo na mshahara pia ukitolewa kwa sheria hizo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini jijini Dodoma, inaelekeza kuwa nafasi hizo za ajira zitakuwa za mkataba wa miaka miwili utakaohuishwa, hivyo kutoa nafasi ya kuendelea kwa kipindi kirefu.
Kuhusu masilahi kwa wafanyakazi, taarifa hiyo inafafanua kuwa watakaopata fursa hiyo mwajiri atawapatia gharama za matibabu kipindi chote cha ajira, usafiri wa kwenda na kurudi pamoja na gharama za chakula na malazi kwa miezi miwili ya mwanzo.
“Mwajiri atalipia gharama zote za usafiri wa kutoka nyumbani hadi kituo cha kazi kwa miezi miwili ya mwanzo wa ajira,” imesisitiza taarifa hiyo.
Kwa wenye uhitaji wa ajira hizo, tangazo la Serikali limefafanua kuwa waombaji wanatakiwa kutuma wasifu wao (CV) kwa nia ya mtandao kupitia https://www.targettours.co.tz [email protected] ikisisitizwa kuwa baada ya kutuma maombi hayo mwombaji atajisajili kupitia hpps://jobs.kazi.go.tz
Kuhusu hatua za usaili wa waombaji, imeelezwa kuwa utafanyika kwa tarehe tofauti katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kuanzia Januari 19 hadi 20, 2026 usaili utafanyika jijini Dar es Salaam, Kariakoo katika jengo la Tahmeed Lumumba, Ghorofa ya pili.
Awamu nyingine itakuwa kuanzia Desemba 24, 2026 ambapo usaili utafanyika jijini Mwanza katika jengo la Exim Bank ghorofa ya tatu.
Usaili huo utahitimishwa jijini Tanga ambapo kuanzia Januari 26 hadi 28, 2026, utafanyika katika jengo la Anjuman.