Pemba. Wakati Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikiendelea kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini kuepuka kubeba abiria kupita kiasi, wazazi na walezi pia wametakiwa kupunguza idadi ya watoto wanaosafiri nao ili kuimarisha usalama wao safarini.
Wito huo umetolewa leo, Desemba 29, 2025, na Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ibrahim Saleh Juma, wakati wa ziara maalumu aliyofanya katika Bandari ya Mkoani, ambapo alibaini meli ya Silink 2 ikiwa imebeba abiria zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa.
Amesema kuwa katika kipindi hiki kuna ongezeko la abiria wanaosafiri kati ya Unguja, Tanga na Dar es Salaam, hali inayochangiwa na kufungwa kwa shule, hivyo amesisitiza umuhimu wa vyombo vya usafiri kuzingatia idadi halali ya abiria ili kuepusha ajali na madhara yanayoweza kujitokeza.
Juma amewaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanapunguza idadi ya watoto wanaposafiri wakati wa mapumziko ya Desemba, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa usalama wao na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
‘’Tumefanya ziara ya kukagua eneo la usafiri kwenye Meli ya Silinki 2 tumebaini ongezeko la abiria, kipindi hichi cha Desemba, Januari na tukatoa angalizo kwa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanapakia abiria halali na sio kutumia kipindi hichi kwa kujaza abiria, kinyume na utaratibu waliowekewa kisheria,’’ amesema.
Amesema meli inaweza kuchukua abiria 1,500 inayotakiwa lakini utakuta kuna watoto wasiopungua 400 hali hiyo inaweza kuleta shida, vyombo vya usafiri vinapaswa kuwa makini katika kulinda usalama wa abiria wao.
“Vyombo vya usafiri vinapaswa kuchukua abiria kulinga na uwezo wa chombo inayotakiwa kama ni abiria 1,500 wasizidishe, wahakikishe wanafuata mifumo ya ununuzi wa tiketi bila ya kuongeza idadi ya abiria kwenye vyombo vya usafiri.
‘’Kwa sababu tu kipindi hiki idadi ya abiria wameongezeka, hivyo vyombo vya usafiri hutumia mwanya huo kwa kuuza tiketi bei ghali ambapo sio bei yake kihalali jambo linalopelekea malalamiko kwa abiria,’’ amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Meli ya Silink 2, Saleh Suleiman Saleh amesema wamekuwa wakijitahidi kufuata utaratibu kwa kupakia abiria wanaopaswa kulingana na uwezo wa meli, lakini alidai changamoto kubwa inayojitokeza ni wazazi kusafirisha watoto wengi kwa wakati mmoja.
Amesema na wakiingia kwenye boti watoto wote wanataka kukaa kwenye viti jambo hilo limekuwa ni gumu na kuomba wazazi na walezi kupunguza idadi ya watoto wakati wakisafiri.
‘’Tumekuwa tukijitahidi kupakia abiria wanaotakiwa lakini changamoto inakuja baadhi ya wazazi wamekuwa wakisafirisha watoto wengi wengine ambao hawalazimiki kakata tiketi , mzazi mmoja anakuja na watoto sita na wote anataka akae nao kwenye viti jambo hilo limekuwa likiwakwaza,’’ amesema.
Awali, Mratibu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kisiwani Pemba, Bakari Hamad Suleiman, amesema mamlaka hiyo imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha utaratibu unafuatwa ili abiria wasafiri wakiwa salama.
Suleiman amesema ingawa kipindi hiki ni changamoto kutokana na ongezeko la abiria, hususan wanafunzi wanaosafiri kwenda masomoni na wengine kurudi nyumbani, mamlaka inajitahidi kuhakikisha kila safari inafanyika kwa njia salama na ya kisheria.
