Soraga awataka vijana waepuke kuvuruga amani

Unguja. Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia, Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema kuna wimbi la wapinga maendeleo linalowatumia vijana kuvuruga amani kwa kisingizio cha kupinga uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Soraga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Desemba 29, 2025, wakati akihutubia katika kongamano la kitaifa la vijana, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Kuna kundi la wasiopenda maendeleo wanawatumia vijana kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha kupinga matokeo ya uchaguzi, hivyo hili msilikubali lindeni amani kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi,” amesema. 

Soraga, amewaomba vijana kuepuka kuhusika na makundi yanayovuruga amani, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ustawi wao, jambo lililosababisha kuundwa kwa wizara zinazowahusisha vijana.

Amesema vijana wasikubali kuungana na watu wenye nia ovu na kutokubali kuhusika katika harakati zinazoweza kuhatarisha amani. Serikali pia itaimarisha ushiriki wa vijana katika maendeleo yanayotekelezwa na viongozi wa nchi.

Soraga amesema kongamano hilo,  linadhihirisha kuwa vijana wapo tayari kulinda na kuyatetea Mapinduzi ya Zanzibar, jambo lilithibitishwa na hatua za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuunda wizara zinazolenga vijana.

Kongamano hilo pia litatoa fursa kwa vijana kujifunza wajibu wao katika kukuza uzalendo, kutambua fursa, na kutoa mapendekezo ya kuimarisha ustawi wao.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Salama Mabrouk Khatib, amesema kuanzishwa kwa wizara hiyo ni ishara ya mshikamano na umoja wa Taifa.

Vijana walioshiriki kongamano la Kitaifa na Vijana na Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lililofanyika New AmaanComplex, Mkoa wa Mjini Magharibi. Picha na Zuleikha Fatawi

Ameongeza kuwa wizara hiyo itahimiza ubunifu wa vijana na kuwa chombo cha kuwakutanisha, kutoa elimu, ajira, na vyeti vya ujuzi vitakavyowasaidia kukabiliana na changamoto za soko la ajira ndani na nje ya Zanzibar.

“Kongamano hilo litakuwa chachu ya kuimarisha ushiriki wa vijana kuyaenzi na kuyalinda kwa vitendo Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema. 

Naye, Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Rashid Ali Salum amesema wizara hiyo ipo kwa ajili kushughulikia changamoto za vijana hivyo wawe tayari kutoa ushirikiano.