Tunduma. Sio jambo la ajabu kwa dereva wa lori kutumia wiki au zaidi kuvuka katika mpaka wa Tanzania na Zambia, wilayani Tunduma, Mkoa wa Songwe.
Hali hii inatokana na kukithiri kwa msongamano wa malori, unaosababishwa na ufinyu wa barabara na uzembe wa baadhi ya watendaji wa mpaka.
Muda mrefu wa kuvuka ni changamoto moja. Madhara yanayowakumba madereva kutokana na siku wanazotumia mpakani ni simulizi ngumu ya maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), zaidi ya malori 1,000 hufika katika mpaka huo kila siku, lakini yanayofanikiwa kuvuka hayafiki nusu.
Mwananchi imefika katika eneo hilo na kupata simulizi za madereva mbalimbali, ambao wanasema ingawa haitabiriki ni siku ngapi zitachukuliwa kwenye msongamano, hakuna nyongeza ya posho wanayopewa na mabosi wao.
Akizungumzia hilo, mmoja wa madereva wa malori, Godwin Kinyaha anasema mabosi huwalipa posho kwa kuhesabu siku za safari kwenda na kurudi kutoka Zambia au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika hesabu ya siku hizo za safari, anasema hakuna anayetoa posho kufidia siku zinazotumika kwenye msongamano mpakani
Kwa mujibu wa Kinyaha, hatua hiyo inasababisha dereva atumie kiasi cha posho kilichopaswa kutumika anakokwenda na wakati mwingine fedha yote inaishia Tunduma.
Kinyaha anasisitiza kuwa licha ya siku kadhaa zilizotumika katika msongamano, hakuna malipo ya ziada ya posho au chakula, hivyo mara nyingine wanaishiwa kabisa.
“Hii inamaanisha inakula kwa dereva, ule muda unaokaa si unatumia fedha nyingi kula na mambo mengine. Kusingekuwa na msongamano ungeshafika DRC na kushusha mzigo, inatuumiza sana kiuchumi,” anasisitiza.
Hata hivyo, anaeleza kila kampuni ya lori ina utaratibu wake wa malipo kwa madereva, lakini zaidi kuna mabosi wachache wanaoongeza posho kwa dereva kutokana na msongamano, lakini wengi hawalipi na hawaelewi.
“Tangu nimefika Tunduma nina siku ya tano leo. Nimekaa siku nne, leo ya tano ndio naona dalili za kuvuka. Maegesho nilikaa siku nne, leo ya tano saa tano usiku ndio tumeitwa tuje kuvuka lakini imeshafika saa mbili asubuhi bado sijavuka,” anasema Kinyaha.
Anaeleza siku hizo alizotumia hadi kuvuka ni chache ukilinganisha na uhalisia wa msongamano katika eneo hilo, kwani zipo nyakati zinapita hadi wiki mbili dereva hajavuka mpakani hapo.
Alipoulizwa kuhusu kiini cha msongamano huo, Kinyaha anasema tatizo linaanzia kwenye ufinyu wa boda yenyewe, kwani ina barabara moja inayopitisha malori yanayovuka kwenda Zambia na moja inayopitisha mengine yanayorudi Tanzania.
“Zilitakiwa kuwa barabara mbili zinazoenda na mbili zinazorudi, hii foleni kidogo ingepungua,” anasema.
Kwa sababu ya wembamba huo wa barabara, anasema hata ikitokea lori moja limeharibikia boda, inalazimika shughuli zote zisimame kwani hakuna eneo la kuliegesha na mengine yapite.
“Kwenye eneo kama Milima ya Sogea gari ikiharibikia barabarani hakuna sehemu ya kuivuta wala kuegesha, inalazimika msubiri itengenezwe iwake ndio muendelee kuvuka, kwahiyo foleni inakuwepo,” anasema.
Kinyaha anaeleza suala la msongamano katika eneo hilo limeshakuwa kawaida kwa madereva, unafika wakati wanakaa zaidi ya wiki kusubiri kuvuka.
Dereva mwingine, Laiton Mwachange, anabainisha kuwa kutokana na msongamano na mara nyingi dereva kuwa mmoja ndani ya lori, analazimika kukesha.
Anaeleza ukishakuwa kwenye msongamano hakuna namna ya kutoka na utalazimika kuwa macho ili magari yakisogea nawe usogee kidogo, hivyo hawalali na kuhatarisha usalama wao barabarani.
“Serikali ituonee huruma imeshazidi, hata kama kuonewa imepitiliza. Na njia hii karibu kampuni zote zinakuja hapa kuna bosi ana gari 50 unamuweka kwenye msongamano siku tatu mwisho wa siku zinakutana na yeye anashindwa awalipe nini madereva,” anasema.
Kilio cha posho kimetolewa pia na Adam Msangi ambaye pia ni dereva wa lori anayesema kadiri wanavyokaa kwenye msongamano mpakani hapo na ndivyo wanavyotumia fedha walizopewa kutumia wanakokwenda.
“Ukikaa muda mrefu matumizi yanaongezeka, fedha uliyopewa kwa ajili ya kwenda kutumia Zambia au DRC, unalazimika kuitumia ukiwa Tunduma sasa unafanyaje,” anasema.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Wadogo wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaaban anasema hakuna biashara ambayo mmiliki wa lori anaifanya gari inapokwama kwenye foleni.
Kwa mazingira hayo, anasema hakuna faida wanayoingiza na hawana fedha wanayopata kulipa posho ya ziada kwa dereva zaidi ya hasara, ni vigumu kulipa.
“Sasa kwenye foleni tunafanya biashara? gari ikisimama maana yake hakuna biashara inayoendelea, nakulipaje wakati hakuna faida nayoingiza. Ni akili finyu. Tunatakiwa kupambana changamoto ya foleni iishe tunaumia wote sio kubebeshana mizigo,” anasema Shaaban.
Katika msisitizo wake, anasema anatambua baadhi ya madereva wanafanya starehe wanapokuwa eneo hilo, huku wakitambua foleni hiyo ni hasara kwa mabosi zao na hakuna posho ya ziada watakayolipwa.
“Ujue lori langu linapokaa kwenye msongamano napata hasara na wakati mwingine natakiwa kulipa fedha ya kuchelewesha kasha kwa ninayempelekea, sasa dereva anataka nimpe hela natoa wapi,” anaeleza.
Anasema wakati mwingine wamiliki hao wa malori wamekopa fedha benki na kadiri lori linapokaa kwenye msongamano riba inaongezeka, kwa hiyo ni hasara juu ya hasara.
Hata hivyo, anasema juzi walikuwa kwenye kikao na viongozi wa Serikali na walikutana baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuwa tayari na kujadili hatma ya msongamano huo.
Jawabu la kwanza, anasema wanataka kuanzia kwenye makutano ya barabara ya mpakani hapo iongezwe njia kwa kuwa gari ikiharibika nyingine haiwezi kupita.
“Upande wa Zambia scanner yao haikuwa inafanya kazi saa 24 na juzi tumekwenda wanasema wameshaweka nyingine ya saa 24 na ujenzi wake umefikia asilimia 99 na ndani ya mwezi huu itaanza,” anasema.
Anashauri ikiwezekana Serikali ifungue geti lingine la kisasa ili kuendana na idadi kubwa ya magari, kwani lililopo ni lile lilijengwa tangu enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zambia, hayati Kenneth Kaunda.
Mwachange anaona tatizo ni utaratibu unaotumika wa kukusanya malori yote kwenye maegesho, kisha yanatolewa na kuruhusiwa kwa mkupuo.
Anasema ungetumika utaratibu wa kila lori linalofika mpakani hapo, liruhusiwe kwenda kuvuka, angalau kusingekuwa na mrundikano.
Hata hivyo, anasema yote hayo yanasababishwa na utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji hasa upande wa Zambia, akifafanua wengi wanaondoka kazini mapema.
“Ukifika mchana hapa wa saa nane si ajabu kuambiwa maofisa wa ZRA (Mamlaka ya Mapato Zambia) wameondoka, sasa mtu anaondoka saa nane mchana anaipenda kazi yake huyo?” anahoji.
Anasisitiza umuhimu wa kila mamlaka kutimiza wajibu wake kupunguza msongamano huo.
Ongezeko la malori tatizo, uzembe
Kwa upande wake, Msangi anasema eneo hilo limezidiwa, kwani wakati mpaka huo unafunguliwa hakukuwa na msongamano, lakini kwa sasa ni tofauti.
“Gari zimeongezeka, miundombinu ni ile ile ya zamani. Kuna kero kubwa kwamba barabara ni moja. Walijenga boda hata mwaka haujaisha Waziri Mkuu (Dk Mwigulu Nchemba) kaja anawaambia wavunje ukuta watanue, sasa wapangaji wanafanya nini.
“Huo ni uharibifu wa fedha za umma, hawakujua kabla kwamba hapa kutahitaji barabara kubwa, kuna maana gani ya kuwa na wahandisi wasomi,” anasema.
Anaishauri Serikali iangalie utaratibu wa kuongeza njia angalau zifike nne, ili kurahisisha uvukaji. Pia anashauri scanner ili kwenda na kasi sawa.
Anaeleza baadhi ya watendaji wamekuwa wazembe, badala ya kutoa huduma, wanachezea simu na hivyo kuwasubirisha madereva.
Kiongozi wa madereva wa malori, Ramadhan Seleman anasema kuna haja ya kutanuliwa kwa barabara ili kuruhusu magari mengi kupita, zaidi ya sasa kila barabara inapitisha lori moja.
Hilo, anasema liambatane na kuoanisha huduma upande wa Zambia uende na kasi sawa na Zambia ili kuwe na mtiririko mzuri wa uvushaji, badala ya mkwamo.
“Zambia wanaishia saa 3 usiku huku sisi (Tanzania), tunafanya hadi saa 24. Pamoja na kwamba Tanzania tuna magari mengi, lakini wakati mwingine foleni inasababishwa na wenzetu wa Zambia,” anasema.
Ni maumivu, neema kwa wengine
Dereva Bodaboda katika eneo la Kilimanjaro, Tunduma ulipo mpaka huo, Ambakisye Tuntufye anasema nao wanaathirika kwa kuwa inawalazimu wapenye jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na abiria wanaowapakia.
“Kuna siku inatokea barabara zinafungwa tunashindwa kupita lakini kwa sisi bodaboda sio tatizo sana kwa sababu tuna njia za mkato, lakini ni tatizo kubwa,” anasema.
Kwa upande wa Loveness Kibinga muuzaji wa Kongoro katika eneo hilo, msongamano huo kwake ni neema.
Anasema madereva wanapokuwa kwenye msongamano wanalazimika kununua supu ya kongoro na vitafunwa kutoka kwake, hivyo anafaidika.
“Mimi foleni hii inaninufaisha, hawa madereva ni wateja wangu, wananunua na napata hela kwa hiyo nanufaika kwa kile ninachokipata,” anasema.
Hata hivyo, Loveness anasema msongamano huo kwa upande mwingine ni maumivu kwake, kwani kuna wakati analazimika kutumia muda mwingi kurudi nyumbani.
“Kuna siku nashindwa kupita kuwahi kurudi nyumbani, kwa sababu ya msongamano huu. Lakini kwa kuwa nauza kongoro sioni shida sana, ingawa kwa wengine ni kero,” anasema.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori Afrika kwa upande wa Tanzania, John Siaba anasema msongamano umesababisha Serikali iruhusu barabara ya Sumbawanga ndio itumike na malori.
Katika barabara hiyo, anasema wakati wa msongamano, madereva huvamiwa na vibaka na majambazi na kuibiwa walivyonavyo kwa kuwa hakuna uhakika wa usalama.
Anasema wanalazimika kupita katika barabara hiyo ya Sumbawanga baada ya barabara ya Mbeya kuwa finyu, ukizingatia malori mengi hivyo inahelemewa.
“Lori zikipanga foleni katika barabara ya Mbeya, zinaweza kufika hadi Vwawa kutokana na ufinyu wa barabara. Sasa Serikali ikaona tupite Sumbawanga, lakini tunachoomba usalama wa madereva uzingatiwe,” anasema.
Kuhusu changamoto ya posho, anasema ingawa suala la malipo kwa madereva wa malori linamuhusu bosi na mfanyakazi wake, kuna haja ya Serikali kuingilia kati ili angalau madereva walipwe kinachostahili.
Katika maelezo yake, Siaba anasema Desemba 12, mwaka huu walikutana na Jeshi la Polisi, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkuu wa Mkoa, Wilaya na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Katika kikao hicho, anasema walijadiliana kuhusu kuelemewa kwa mpaka huo, kutokana na wingi wa malori na ufinyu wa barabara na wakakubaliana umuhimu wa kuwepo kuongeza miundombinu.
Katika mazungumzo yake kuhusu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame anasema wanatambua kwamba changamoto hiyo inasababishwa na ufinyu wa barabara.
Changamoto zote kuhusu eneo hilo, walizibaini baada ya kuwasikiliza wadau wa usafirishaji, katika kikao walichoketi nao mapema Desemba mwaka huu.
Baada ya kikao hicho, Makame anasema Tanroads wameshaelekezwa kuangalia uwezekano wa kuitanua barabara katika mpaka huo.
Mbali na kilichoelezwa na Makame, katika ziara yake ya Desemba 12, mwaka huu, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alimwelekeza Mkurugenzi wa Tanroads, Mohamed Besta atafute fedha za dharura kufanya tathmini na utanuzi wa barabara hiyo.
“Zitajengwa barabara za njia tatu. Zitafutwe fedha za dharura kutengeneza mzani Iboya na magari yote yanayotoka Tunduma yakapime huko na sio Mpemba,” anasema.
Anataka barabara za michepuko katika eneo hilo, zifanyiwe kazi haraka na kuepusha migogoro kati ya madereva na Serikali.
