WANANCHI HAI, FUONI , KATA TANO KUPIGA KURA KUCHAGUA WABUNGE NA MADIWANI KESHO

 

Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele leo Desemba 29,2025 amesoma
risala maalum kuhusu uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Siha lililopo
Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania Bara na Jimbo la
Fuoni lililopo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Tanzania
Zanzibar unaotaraji kufanyika Desemba 30,2025.
 
Jaji Mwambegele amesema,
uchaguzi mdogo huo utahusisha pia, kata tano za Tanzania Bara. Kata hizo ni;            Chamwino iliyopo katika Halmashauri
ya Manispaa ya Morogoro, Mkoa wa Morogoro; Mbagala Kuu iliyopo Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam; na Nyakasungwa iliyopo katika Halmashauri
ya Wilaya ya Buchosa, Mkoa wa Mwanza.
 
Nyingine ni Kata ya Masoko
iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mkoa wa Mbeya; na kata ya Ndono
iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora.
 
Aidha, amesema jumla
ya wagombea 33 kutoka katika vyama vya siasa 17 wanawania nafasi wazi za ubunge
na udiwani katika maeneo niliyoyataja. Kati ya wagombea 33, wagombea 21 sawa na
asilimia 63.64 ni wanaume na wagombea 12 sawa na asilimia 36.36 ni wanawake.
Kwa namna ya pekee, Tume inavipongeza vyama vilivyoshiriki na wagombea
waliojitokeza kushiriki.
 
Jaji Mwambegele amesema,
jumla ya Wapiga Kura 218,024 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura watashiriki katika uchaguzi huo na jumla ya vituo 556 vya Kupigia Kura
vitatumika.
 
“Natumia fursa hii
kuvikumbusha Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho tarehe 30 Desemba,
2025 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya zoezi la kupiga,
kuhesabu na kujumlishia kura. Wasimamizi wa uchaguzi katika Majimbo na Kata
husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa
vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
 
Amesema, mawakala
hao, wanawajibika katika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo,
wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume
katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.