Yanga yafuata straika Angola | Mwanaspoti

YANGA inaendelea kujifua kwa mazoezi makali kambini, huku ikijiandaa kufunga safari kwenda visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, lakini kuna kitu kinaendelea kufanywa na mabosi wa klabu hiyo kimya kimya katika kuimarisha kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Mreno, Pedro Goncalves.

Katika kufanyia kazi pendekezo la kocha Pedro la kutaka kuletewa straika mpya anayejua kufunga mabao, mabosi wa Yanga wamehamia kwa nyota wa timu ya taifa ya Angola, Gelson Dala anayekipiga kwa sasa katika klabu ya Al-Wakrah ya Qatar, ili kama mambo yataenda sawa jamaa atue dirisha dogo kuitumikia timu hiyo ya Jangwani.

Mshambuliaji huyo wa kati anayetumia mguu wa kulia mwenye umri wa miaka 29 amebakiza miezi sita na Al-Wakrah baada ya kujiunga nayo Julai Mosi, 2022 kwa muda wa miaka minne kabla ya kutolewa kwa mkopo wa muda mfupi kwa Rio Ave FC ya Ureno ambayo ndio iliyowauzia Waarabu hao nyota huyo aliyewahi kupita pia  Sporting.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli Yanga ipo katika mchakato wa kutafuta mshambuliaji baada ya ripoti ya kocha Pedro kuhitaji mchezaji wa eneo hilo na kuna nyota wanatupiwa macho na kwa sasa dira zimeelekezwa kwa Dala mwenye bao moja katika AFCON 2025 (kabla ya mechi za jana).

“Kuhusu Dala ni miongoni mwa majina yanayotajwa eneo la ushambuliaji, lakini dili bado halijakamilika ispokuwa uongozi umefanya mazungumzo kwa ukaribu na mchezaji huyo ambaye pia ameonyesha nia ya kutafuta changamoto nje ya nchi aliyopo sasa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Bado tunaendelea kumtupia macho sio mshambuliaji mbaya hasa kwa dirisha hili dogo ambalo ni ngumu kupata mchezaji bora ambaye hana mkataba na timu nyingine. Kwa Dala kuna unafuu kidogo kwani mkataba alionao Qatar unaelekea ukingoni.”

Chanzo hicho kilisema kutokana na nyota huyo kuwa katika kikosi cha timu ya taifa kinachoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) uongozi umempa jina kocha ili aweze kumfuatilia kwa ukaribu kama ataridhishwa na uwezo wake basi jambo hilo watalikamilisha haraka.

Katika mechi ya kwanza waliyopasuka mabao 2-1 mbele ya Afrika Kusini, Dala alitumika kwa dakika 76 na ile iliyoisha kwa sare dhidi ya Zimbabwe alicheza kwa dakika 80 na kufunga bao la utangulizi kabla ya wapinzani wao kuchomoa karibu na mapumziko.

“Kocha anamtazama na si mchezaji huyo tu kuna wengine wawili ambao majina yao sijayapata bado, ila nao wapo pia katika fainali hizo na wanatazamwa, atakayemvutia zaidi kocha basi atamalizana na uongozi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Uzuri kiongozi wetu yupo nchini humo hatutakuwa na wakati mgumu kufunga safari kwa ajili ya kumalizana na mmoja wa wachezaji hao ambao wanatazamwa kuja kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji ambao kwa sasa linaongozwa na Prince Dube.”

Mshambuliaji aliyeanza kufahamika kupitia klabu ya CD 1 de Agosto ya Angola kabla ya kutua Ureno na kuchezea klabu mbalimbali anafahamiana vyema na Pedro aliyewahi kuinoa timu hiyo ya taifa ya Angola na kuipeleka katika fainali hizo za 35 zinazoendelea Morocco wakati kocha huyo akija kujiunga na Yanga hivi karibuni.