Faili la Fei Toto latua mezani kwa MO Dewji, kocha mpya aachiwa msala

KOCHA mkuu wa Simba, Steve Barker jana Jumatatu alikuwa na kikao kizito na benchi la ufundi sambamba na mabosi kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya klabu ikiwamo ishu ya usajili, lakini kuna mtu mmoja ametuma ujumbe maalumu kwa Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji kuhusu Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Kiungo mshambuliaji huyo wa Azam FC kwa sasa yupo katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 akiwa na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachomalizia mechi ya mwisho ya Kundi C leo dhidi ya Tunisia ikisaka rekodi mpya ya kushinda na kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano inayofanyika Morocco.

Katika dirisha kubwa lililopita la msimu huu, Simba ilihusishwa kumtaka Fei Toto kutokana na pendekezo lililotolewa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, lakini ilikwama kumpata kutokana na mkataba aliokuwa nao Azam na dau lililowekwa na mabosi wa Chamazi ambao waliomuongezea mkataba mpya hadi 2027.

Hata hivyo, licha ya kiungo huyo kuwa na mkataba mrefu na Azam, kuna shabiki mmoja lialia wa klabu hiyo, aliyeamua kutuma ujumbe kwa MO Dewji akimtaka kufanya kila linalowezekana kumshusha jamaa ili kuimarisha eneo la mbele ya kikosi hicho kwa kuamini Fei Toto anaendana na soka la Msimbazi.

Aliyetoa ombi hilo ni msanii wa vichekesho, Aman Nzala ‘Anko Nzala’ aliyeliambia Mwanaspoti limfikishie ujumbe Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Simba, MO Dewji kumshauri amsajili namba 10 mzawa ili kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji.

Anko Nzala amesema kiungo mshambuliaji huyo wa Azam, anayemuona ni mtu sahihi na anatamani kumuona akivaa jezi ya Simba na kumsisitiza Mo Dewji kama akiamua linawezekana kabisa kumshusha fundi huyo wa mpira na kurejesha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo.

“Mimi ni shabiki wa Simba lialia, najua Mo Dewji anazikubali kazi zangu na aliwahi kuziposti katika mtandao wa Instagram, ninachotamani kumwambia atusajilie Fei Toto najua lipo ndani ya uwezo wake kama ataamua,” amesema Anko Nzala na kuongeza;

“Kinachotakiwa kwa Simba ni wachezaji wenye uwezo wa juu sina maana waliopo ni wabaya, ila mchezaji kama Fei ana uwezo wa kufunga mipira ya chenga, ya kutenga, mashuti ya mbali pia ni fundi wa kutengeneza asisti, hivyo akijiunga Simba kuna kitu kikubwa atakiongeza katika safu ya ushambuliaji.”

Fei msimu uliopita alimaliza na asisti 13 na mabao manne, wakati kwa msimu huu amefunga mabao mawili na asisti moja, pia ni mshkaji wa Anko Nzala aliyefichua wakianza kutaniana anamwambia kuna siku atavaa jezi ya Wanamsimbazi.

“Japo tukikutana huwa namtania na kumwambia kuna siku tajiri Mo Dewji akiamua atakusajili, tukiweka ushabiki pembeni Fei Toto ni mchezaji aliye na kipaji kikubwa,” amesema Nzala.

Alipoulizwa ni mchezaji gani wa Yanga anayetamani achezee Simba? Alijibu:”Japo nina washikaji zangu ninaowakubali kama Djigui Diarra, Maxi Nzengeli, Dickson Job na wengine wengi ila hakuna hata mmoja ninayetamani aje kuichezea Simba, Yanga ndio inayotamani wachezaji kutoka wa Simba.”

Kabla ya kutua Azam FC, Fei Toto aliitumikia Yanga kwa misimu karibu mitano baada ya kusajiliwa kutoka JKU ya Zanzibar japo alipita kidogo Singida United.