Taifa Stars ‘do or die’ Morocco

HAKUNA namna. Taifa Stars ina dakika 90 ngumu usiku wa leo mbele ya Tunisia. Ni ushindi pekee ndio unaweza kuifanya timu hiyo isalie Morocco ama ifungashe virago kurudi nyumbani kama ilivyokuwa kwa Botswana, Gabon na Guinea ya Ikweta zilizoaga mapema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya Kundi C kwa Nigeria, kisha kulazimishwa sare ya 1-1 na Uganda, Taifa Stars imeingia mtegoni, kwani inahitaji ushindi wa aina yoyote usiku wa leo ili kujiweka katika nafasi ya kusonga mbele katika fainali hizo.

Licha ya kwamba ushindi huo mbele ya Tunisia katika mechi hiyo ya mwisho ya makundi itaiweka Stars katika nafasi nzuri ya kutinga 16 Bora, pia itakuwa ni rekodi kwa timu hiyo  inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya nne tangu mwaka 1980.

STA 01

Katika ushiriki wa fainali tatu za awali za mwaka 1980, 2019 na 2023, timu hiyo ya taifa ya Tanzania haijawahi kupata ushindi wowote zaidi ya kuambulia sare au vipigio kutoka kwa wapinzani.

Fainali za kwanza za 1980 kule Nigeria, Stars ilipoteza mechi mbili kwa vipigo vya 3-1 kutoka kwa Nigeria na 2-1 kutoka Misri, kisha ikatoka sare ya 1-1 na Ivory Coast, wakati fainali za 2019 ilipoteza zote mbele ya Senegal (2-0), Kenya (3-2) na Algeria (3-0) na zile zilizopita za Ivory Coast ilipoteza 3-0 kwa Morocco, kisha kutoka sare ya 1-1 na Zambia na kutoka sululu na DR Congo na kote kukwamia hatua hiyo ya makundi.

Katika msimu huu kwa sasa katika kundi ililopo, Nigeria tayari imeshakata tiketi ya kucheza 16 Bora ikizifuata Misri na Algeria zilizotinga mapema kila moja ikikusanya pointi sita, huku Tunisia ikiwa ni ya pili katika msimamo kwa pointi tatu, kisha Tanzania na Uganda zikifuata zikiwa na pointi moja na kutofautiana mabao tu.

STA 02

Stars inavaana na Tunisia kwenye Uwanja wa Olympic wa Rabat kuanzia saa 1:00 usiku muda ambao pia Nigeria na Uganda zitapepetana kwenye Uwanja wa Fez, ili kuamua timu moja ya kuifuata Nigeria na ile itakayopenya kupitia kapu ya mshindwa bora (best looser) kutinga hatua ya 16 Bora.

Hii ni mechi ya kufa au kupona kwa Tanzania kwani ikipoteza au kutoka sare itakuwa imehitimisha ushiriki wake wa fainali hizo za 35 tangu zilipoasisiwa kwa michuano mwaka 1957.

Ni mechi ambayo kocha Muargentina Miguel Gamondi anapaswa kuingia uwanjani kwa mbinu  na mipango madhubuti kama kweli anataka kuivusha Stars hatua inayofuata na kuwa kocha wa kwanza kufanya hivyo katika AFCON akiwa na timu hiyo ya Tanzania. Stars inatakiwa kucheza kwa nidhamu na utulivu mkubwa na kuepuka makosa kama yaliyojitokeza katika mechi mbili zilizopita ambazo ziliigharimu timu hiyo mbele ya Nigeria na Uganda.

Tunisia ni timu inayocheza soka kwa nidhamu kubwa ya kiulinzi, mpangilio mzuri wa kati na mashambulizi ya kushtukiza. Wanajua kulinda matokeo na wamezoea mechi za presha. Kwa Stars, changamoto kubwa itakuwa kuvunja ukuta wao bila kupoteza umakini nyuma, kwani katika mechi zote mbili zilizopita imeruhusu mabao.

STA 03

Ilipoteza kwa mabao 2-1 kwa Nigeria baada ya kusawazisha bao mara baada ya kipindi cha pili, lakini hata katika mechi ya Uganda licha ya kutangulia kupata bao la penalti mapema kipindi cha pili iliruhusu bao la kusawazisha kwa wapinzani wao katika dk80 kisha ikanusurika kipigo baada ya Uganda kupoteza penalti dakika za majeruhi.

Ingawa Tunisia ilianza michuano kwa ushindi mnono wa mabao 3-1, ni timu inayofungika kwani katika mechi ya pili dhidi ya Nigeria ilikubali kulala mabao 3-2 na kuifanya iwe moja ya timu zilizoruhusu mabao mengi kundini, ikifungwa manne kama ilivyo kwa Uganda, wakati Tanzania imefungwa matatu kama ilivyo kwa Nigeria.

Huenda kukawa na mabadiliko kidogo kwa kikosi kilichocheza na Uganda, ambapo dhidi ya Tunisia langoni anaweza kusimama Zuberi Foba, huku Shomary Kapombe anaweza kurejea kikosini kucheza beki wa pembeni na Mohammed Hussein, huku Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto wakasimama beki ya kati na viungo wakiwa ni Alphonce Mabula, Dismas Novatus na Feisal Salum, huku Mbwana Samatta akitarajiwa kurudi katika nafasi yake ya mshambuliaji kinara akisaidiwa na Simon Msuva na Tarryn Allarakhia.

Hata hivyo, kocha Gamondi ana nyota wengine ambao anaweza pia kuanza nao kama ataamua kufanya mabadiliko zaidi akiwamo Idd Seleman ‘Nado’, Seleman Mwalimu, Charles M’Mombwa na Yusuf Kagoma kwa eneo la kiungo, mbali na wachezaji wengine akiwamo Kelvin John na Haji Mnoga.

STA 04

Mabeki wa Stars wanapaswa kuwa makini na washambuliaji Elias Achouri mwenye mabao mawili hadi sasa, Hazem Mastouri na Sebastian Tounekti ambao ni wasumbufu na wanaocheza kwa kasi, mbali na viungo na mabeki wanaopandisha mashambuli kama Montassar Talbi na Ali Abdi wenye bao moja kila mmoja.

Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara mbili tangu 2020 zilipokuwa katika kundi moja la mechi za kufuzu AFCON ambapo Tunisia ilishinda mechi ya nyumbani kwa bao 1-0 na kulazimisha sare ya 1-1 ugenini, kuonyesha kuwa ni timu zisizochekana sana, japo kwa viwango vya soka vya FIFA Tunisia ipo juu zaidi.

Mapema kocha Gamondi amesema mechi ya leo ni ngumu kutokana na ubora wa Tunisia, lakini watashuka uwanjani kupambana kuhakikisha wanamaliza vyema mechi za makundi, huku akionyesha kusononeshwa na matokeo ya sare dhidi ya Uganda kwa vile timu ilionekana ilikuwa ikiandika historia ya kupata ushindi wa kwanza katika AFCON.

Mfungaji kinara wa michuano ya AFCON kwa Tanzania, Simon Msuva amesema imani yake ni kwamba AFCON kwao bado haijaisha hadi pambano hilo liiishe dhidi ya Tunisia akiwataka Watanzania waiombee dua njema wakati wakiwaombea pia wapinzani wao Uganda wachemshe katika mechi yao dhidi ya vinara, Nigeria.