Kocha Fufuni macho yote kwa Simba

JANA Jumatatu kuanzia saa 10:15 jioni, vinara wa Ligi Kuu Zanzibar, Fufuni walikuwa uwanjani kucheza dhidi ya Muembe Makumbi City katika Kombe la Mapinduzi 2026, lakini kocha wa kikosi hicho, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ alikuwa ameitolea macho Simba.

Fufuni kutoka kisiwani Pemba, imepanda daraja Ligi Kuu Zanzibar msimu huu 2025-2026, na kupata nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja ikipangwa Kundi C sambamba na Muembe Makumbi City na Simba.

Baada ya jana kumalizana na Muembe Makumbi City, Fufuni itamaliza hatua ya makundi Januari 5, 2026 kucheza dhidi ya Simba ambayo mechi ya kwanza itacheza Januari Mosi 2026 dhidi ya Muembe Makumbi City.

Akizungumzia namna anavyoiona nafasi ya Fufuni kutinga nusu fainali kutokea kundi hilo linalotoa timu moja pekee, kocha huyo amesema wataonyeshana umwamba na Simba kuamua nani mbabe kati yao.

Man Gamera au Govinda kama mwenyewe anavyopenda kuitwa majina hayo, amesema hakuna cha kuhofia kukutana na timu yoyote, kikubwa anachofahamu Simba ni wababe wa Tanzania Bara na Fufuni wameitawala Zanzibar, hivyo wanakwenda kukutana wababe wawili kusaka mshindi.

“Mtawala wa Tanzania Bara ni Simba, lakini mtawala wa Unguja ni Fufuni, tukikutana ndani ya uwanja itaamuliwa nani mtawala wa jumla.

“Haya ni mashindano makubwa, hatuwezi kuja kinyonge,” amesema.

 “Fufuni tuna malengo ya kufika fainali na kwenda kuchukua ubingwa ardhi ya nyumbani kule Pemba.

“Mimi kwetu Unguja, lakini timu inatokea Pemba na fainali ya Mapinduzi itachezwa Pemba. Ukiangalia katika ligi tumechukua pointi takribani 15 hapa Unguja, hivyo nimeshazoea kushinda nikiwa hapa.

“Kama nilivyojitambulisha naitwa Suleiman Mohamed a.k.a Man Gamera, mwisho unaweza kumalizia Govinda. Unajua Govinda ni ‘sterling’ wa Kihindi ambaye hafi mpaka mwisho wa mchezo, kwa hiyo nimejiandaa kupambana hadi mwisho, kwangu ni suala la kawaida,” amesema