Dar es Salaam. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema kati ya Januari na Desemba 2025, matukio ya moto 3,091 yaliripotiwa, yakisababisha vifo vya watu 114 na majeruhi 295.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Desemba 24, 2025, jeshi hilo limesema mikoa iliyoathirika zaidi ni Dar es Salaam, Mbeya, Pwani, Ruvuma, Njombe, Dodoma na Manyara.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha jeshi hilo imesema maeneo yaliyoathirika zaidi ni nyumba za makazi yakiwamo matukio 1,422, magari 94, ofisi 132 na stoo 117.
Mbali na hayo, jeshi hilo limesema kuanzia Januari hadi Desemba 2025, jumla ya matukio ya moto 3,091 yalifanyiwa uchunguzi.
“Tulibaini kuwa vyanzo vinavyoongoza kwa matukio ya moto ni hitilafu katika mifumo ya umeme, yakiwa matukio 781,” imesema taarifa hiyo.
Vyanzo vingine ni watoto kuchezea viberiti yakiwa matukio 215 na uchomaji wa takataka pamoja na maandalizi ya mashamba yakiwa matukio 479.
Miongoni mwa matukio hayo, liliripotiwa Julai 15, 2025, kwamba mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka mitatu hadi minne alifariki dunia kwa ajali ya moto uliotokea ndani ya chumba kimojawapo katika ghorofa eneo la Magomeni Kota, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi Jacob Chacha, alikaririwa na Mwananchi akieleza uchunguzi wa awali ulibaini chanzo cha ajali ni mtoto huyo aliyekuwa ndani ya chumba akichezea njiti za kiberiti bila uangalizi wa mtu yeyote.
Katika kudhibiti na kuzuia majanga ya moto, jeshi hilo limesema linaendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga katika vyombo vya usafiri na usafirishaji, pamoja na majengo, kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalamu na kuimarisha kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto katika ujenzi.
Imeelezwa maeneo 69,594 yalikaguliwa na michoro ya ramani 2,356 ilipitishwa.
Vilevile, jeshi hilo limeendelea kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto, ikielezwa maeneo 22,062 yalifikiwa moja kwa moja.
Kupitia vyombo vya habari, imeelezwa vipindi 1,039 vya kuelimisha umma, vikiwamo 978 vya redio na 61 vya runinga, vilifanyika vikilenga kuhamasisha jamii kuhusu usalama wa moto na uokoaji.
Mbali na hayo, limeeleza linaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza majanga ya moto, ikiwemo kuimarisha utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari kwa kutembelea maeneo, kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuongeza vituo vya zimamoto na uokoaji.
Pia, linaongeza idadi ya watumishi na kuimarisha vitendeakazi, ikiwamo mitambo ya kuzima moto na uokoaji, magari ya kubeba wagonjwa, helikopta ya kuzima moto na uokoaji, boti za uokoaji na vifaa vingine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, amesema si kila hitilafu ya umeme inayojitokeza katika nyumba za wananchi husababishwa na shirika hilo.
Twange amesema miundombinu ya umeme katika nyumba hugawanyika katika sehemu mbili; upande wa mmiliki wa nyumba na mkandarasi wake, pamoja na upande wa Tanesco.
“Nyumba ya mtu umeme una pande mbili. Kuna sehemu ya mwenye nyumba na mkandarasi wake kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umeme. Baada ya kukamilisha, Tanesco tunaitwa kupeleka huduma ya umeme,” amesema.
Amefafanua kuwa matumizi ya kila siku ya umeme ndani ya nyumba ni jukumu la mtumiaji mwenyewe, na shughuli au matumizi yasiyo sahihi yanaweza kusababisha hitilafu za umeme.
Twange amesema uchunguzi hufanyika kubaini chanzo cha tatizo iwapo hitilafu imesababishwa na miundombinu ya Tanesco au matumizi ya mtumiaji.
“Si kila hitilafu ya umeme inapaswa kulaumiwa Tanesco. Pale mwenye nyumba anaporipoti, Tanesco tunaenda kufanya uchunguzi. Tukibaini ni tatizo la Tanesco tutakiri, lakini kama ni mtumiaji, tutamuelimisha namna sahihi ya kutumia umeme ili kuepuka ajali,” amesema.
Ameeleza kuwa elimu kwa watumiaji wa umeme ni muhimu ili kuhakikisha usalama na matumizi sahihi ya nishati hiyo majumbani, na wamekuwa wakiitoa mara kwa mara.
Wakati Tanesco ikieleza hayo, ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi hivi karibuni baada ya kuibuka matukio ya moto Kariakoo, Dar es Salaam, uliibua hoja kutoka kwa wadau kuhusu baadhi ya watu kubana matumizi katika ujenzi wa mfumo wa umeme, ikiwamo utandazaji wa nyaya na ununuzi wa vifaa.
Hali hiyo ilielezwa haijitokezi katika ujenzi wa majengo mapya pekee, bali hata yanapobadilishwa matumizi yale ya zamani, mfano kutoka makazi kwenda ofisi au biashara. Licha ya ongezeko la matumizi, miundombinu ya umeme hubaki ileile ya awali, hivyo kuelemewa.
Vilevile, kuliibuliwa hoja ya matumizi ya mafundi wasio na viwango ili kukwepa gharama.
Mbao na bidhaa zake zinazotengenezwa kwenye maghala ni miongoni mwa vitu vinavyowaka kwa kasi zaidi, hali inayosababisha ongezeko la matukio ya moto.
Usiku wa kuamkia Desemba 5, 2025, moto uliteketeza ghala ambalo samani hutengenezwa eneo la Boko Msikitini, jijini Dar es Salaam.
Tukio lingine la aina hiyo lilitokea kwenye ghala na maduka ya samani eneo la Keko Novemba 24, 2025, chanzo kikitajwa kuwa hitilafu ya umeme.
Ndani ya juma moja Julai 2025, maeneo ya biashara katika masoko yaliyopo mikoa ya Iringa, Tabora na Singida yaliteketea kwa moto.
Wakati soko maarufu la Mashine Tatu, lililopo Manispaa ya Iringa, likiteketea kwa moto usiku wa kuamkia Julai 12, 2025, tukio lingine liliteketeza maduka matano katika eneo la Salmini, Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, usiku wa kuamkia Julai 7.
Vilevile, vibanda 13 vilivyomo ndani ya Soko Kuu la Singida usiku wa kuamkia Jumamosi Julai 5, 2025 viliteketea kwa moto.
Kuhusu shughuli za uokoaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema limefanya uokoaji katika maeneo 1,127, yakiwamo migodini, mashimo ya vyoo, ajali za barabarani, mafuriko, mito, mabwawa na baharini.
Matukio hayo imeelezwa yalisababisha vifo 130 na majeruhi 1,726, huku mikoa iliyoathirika kwa matukio ya uokoaji ikiwa ni Morogoro, Katavi, Dodoma na Mbeya.
“Jeshi linawakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi cha mvua za vuli na masika kwa kuepuka kuishi au kukaa katika maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mafuriko,” imeeleza taarifa hiyo.
Wananchi pia wametakiwa kuhakikisha watoto wanalindwa na kuepuka kucheza kwenye mito, mabwawa na visima vilivyo wazi, pamoja na kuweka na kutumia vifaa vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.
