RC Mara aonya gharama kubwa  vipimo vya afya kwa wanafunzi

Tarime. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ametoa muda wa saa 48 kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime kukutana na wakuu wa shule zote za sekondari za umma wilayani Tarime na kuandaa fomu ya aina moja ya vipimo vya hospitali, kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza hivi karibuni.

Kanali Mtambi ametoa agizo hilo Desemba 29,2025 wilayani Tarime alipofanya ziara ya  kukagua miundombinu ya shule ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi, ambapo pamoja na mambo mengine alibaini uwepo wa gharama kubwa kwa ajili ya vipimo hivyo.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Dk Amos Manya amesema vipimo hivyo vinagharimu zaidi ya Sh50,000 kulingana na vipimo viliainishwa na shule husika katika fomu.

“Kuna shule unakuta wameandika watoto wapimwe figo, ini na vipimo vingine ambavyo mtaalamu analazimika kutumia X –Ray, vya maabara na kawaida kwa hiyo gharama inatokana na idadi ya vipimo pamoja na aina ya kipimo,” amesema.

Kutokana na maelezo hayo, Mkuu huyo wa mkoa amesema gharama hizo ni kubwa na ni mzigo kwa wazazi, hivyo ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuandaa fomu maalumu itakayokuwa na gharama nafuu .

“Serikali inataka kila mtoto wa Kitanzania apate elimu na kwa sasa elimu ya lazima ni kuanzia awali hadi kidato cha nne na ili kufikia lengo hilo imeamua kutoa elimu bila malipo, kwa hiyo haiwezekani kukawa na vikwazo vitakavyosababisha wazazi washindwe kupeleka watoto shule,” amesema.

Amefafanua kiasi cha Sh50,000 ni kikubwa hivyo ni lazima utaratibu ufanyike ili kupunguza gharama hiyo kuruhusu wazazi waweze kuendelea na maandalizi mengine, kwa ajili ya watoto kuanza masomo shule zitakapofunguliwa Januari mwakani.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza leo Desemba 30, 2025 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya elimu wilayani Tarime.  Picha na Beldina Nyakeke

“Kuna vipimo ambavyo sidhani kama ni lazima kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, yaani nyie mnapima hadi figo utadhani mtoto anataka kuwa komando wa jeshi, hakuna haja ya kumpa mzazi gharama kubwa kiasi hicho, andaeni fomu yenye vipimo muhimu ambavyo vitakuwa na bei rafiki,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kanali Mtambi, amewaagiza wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kuwa miundombinu yote ya shule kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza masomo mkoani humo inakuwa tayari kabla shule kufunguliwa Januari mwakani.

Agizo hilo limetolewa kufuatia ziara aliyofanya Februari mwaka huu wilayani Tarime, ambapo alibaini baadhi ya wanafunzi kulazimika kukalia matofali, mawe, au kuleta viti kutoka nyumbani shuleni kutokana na upungufu wa madawati, jambo ambalo amesema kwa sasa hali hiyo haikubaliki.

Amesema kuwa mwaka huu Serikali imetoa zaidi ya Sh4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya saba za sekondari, huku halmashauri pia zikitenga fedha kutoka mapato ya ndani kwaajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine ya shule.

“Niwaagize pia  wataalamu kuanza kupitia miradi yote na kukagua kama ujenzi umezingatia viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa BoQ, pia kama suala zima la thamani ya fedha limezingatiwa,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amesema kufuatia maandalizi yanayoendelea wilaya hiyo itakuwa na ziada ya madarasa na madawati ingawa hakutoa takwimu.

“Kesho nakwenda kupokea madawati yenye thamani ya zaidi ya Sh324 milioni na kwa jinsi maandalizi yetu yalivyo tunakwenda kuwa na ziada ya madawati na madarasa kwa mwaka wa masomo 2026,” amesema Meja Gowele

Baadhi ya wazazi wamemshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa maagizo aliyoyatoa hususan kuhusu vipimo vya afya kwa ajili ya wanafunzi.

“Juzi kuna mtoto alikwenda kupima katika kituo cha afya Sirari akatakiwa kulipa Sh34,000 lakini akawa ana Sh20,000 wakamkatalia na akarudi nyumbani bila kupima,” amesema Otaigo Waitara.