Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewafutia kesi na kuwaachia huru washtakiwa wawili kati ya sita waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia katika jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Waliofutiwa mashtaka na kuachiwa huru ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Zenabu Islam(61) ambaye ni mkazi wa Kariakoo na mshtakiwa wa tatu, Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.
Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Leondela Mdete(49) mkazi wa Mbezi Beach, pamoja na wenzake watatu ambao ni Soster Nziku(55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe(59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku(28) mkazi wa Mbezi Beach, wao hawajafutiwa mashtaka yao na DPP, hivyo wanaendelea na kesi hiyo.
Uamuzi huo wa kuwafutia kesi washtakiwa hao wawili, umetolewa leo Jumanne Desemba 30, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Godfrey Mhini, anayesikiliza kesi hiyo.
Hakimu Mhini amesema Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo, baada ya DPP kuwasilisha hati mahakamani hapo ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Awali, wakili wa Serikali Christopher Olembelle akisaidiana na Neema Kibodya, aliileleza Mahakama hiyo kuwa DPP amewasilisha hati ya kutokuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa wawili, chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.
Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii
