Ushirikiano duni kwenye kilimo, chanzo migogoro ya familia

Iringa. Dawati la jinsia Mkoa wa Iringa limesisitiza kuwa kuimarisha ushirikiano wa kifamilia ni njia madhubuti ya kupunguza migogoro na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii za wakulima.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Desemba 30, 2025, na Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai.

Swai alikuwa akizungumza na wakulima kwenye mdahalo wa mafunzo ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU),  uliolenga kujadili masuala ya ukatili wa kijinsia na stadi za maisha.

Swai amesema migogoro mingi ya kifamilia huanzia katika shughuli za kilimo pale majukumu na uamuzi unapobaki upande mmoja wa familia, hali inayochochea kutokuelewana na kuzua migawanyiko.

“Familia nyingi huanza msimu wa kilimo kwa mshikamano, lakini changamoto hujitokeza baada ya mavuno, hususan kwenye matumizi ya mapato ndipo migogoro huanza,” amesema Swai.

Amesema Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto, linapokea idadi kubwa ya kesi kutoka maeneo ya vijijini zinazohusiana na migogoro ya kifamilia inayotokana na shughuli za kilimo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia mkoani Iringa, Elizabeth Swai akizungumza na Wakulima katika ukumbi wa mikutano wa Chuo huria leo Desemba 30, 2025 wakati wa mdahalo wa mafunzo ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa humo (IFCU).picha na Christina Thobias

Kutokana na hali hiyo, amesema IFCU imeamua kuandaa mdahalo wa mafunzo kwa wanachama wake ikilenga kujadili kwa kina masuala ya ukatili wa kijinsia na stadi za maisha, kama sehemu ya juhudi za kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wakulima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU), Tumaini Lupola amewataka wakulima kuacha migogoro isiyo ya lazima na badala yake, waelekeze nguvu zao katika kufanya kilimo chenye tija kwa ajili ya maendeleo ya familia zao na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika mdahalo huo, Lupola amesema migogoro ya kifamilia hasa inayohusiana na umiliki wa mashamba na matumizi ya mapato ya kilimo, imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya wakulima wengi mkoani Iringa.

Naye Ofisa Miradi wa IFCU, William Seme amesema mdahalo huo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wakulima kwa kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa kifamilia katika kuongeza uzalishaji na ustawi wa kaya.

“Mradi huu unalenga kupunguza mzigo wa kazi unaoangukia upande mmoja wa jinsia na kuhakikisha wanafamilia wote wanashiriki katika maamuzi ya kilimo na matumizi ya mapato,” amesema Seme.

Amesema mdahalo huo umefanyika chini ya mradi wa kukuza maisha bora, endelevu na shirikishi kupitia mkulima ndani ya ushirika, unaofadhiliwa na shirika la We Effect.

Nao baadhi ya wakulima walioshiriki mdahalo huo wamesema ukosefu wa ushirikiano wa kifamilia husababisha matatizo mengi, yakiwamo ya migogoro ya ndoa, kushuka kwa kipato na athari kwa watoto katika malezi.

“Unapofanya kazi shambani peke yako na maamuzi ya mapato yasifanywe kwa pamoja, migogoro haiwezi kuepukika,” amesema Festo N’gasi, mmoja wa wakulima walioshiriki mdahalo huo.