Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) uliojengwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Mamlaka hiyo pindi utakapoanza kutumika.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza na wataalam wa ndani ya TRA walioshiriki kujenga mfumo huo tarehe 29.12.2025 jijini Dar es Salaam amesema mfumo wa IDRAS utarahisisha sana ukusanyaji wa mapato na kuokoa muda wa walipakodi.
Amesema kupitia mfumo wa IDRAS TRA itaweza kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi na kuzuia ukwepaji kodi kwa kupata taarifa sahihi za walipakodi wote hali ambayo itaongeza mapato ya Serikali.
Kupitia IDRAS Kamishna Mkuu Mwenda amesema watawezesha biashara zaidi kwa kuhakikisha walipakodi wanapatiwa makadirio kulingana na taarifa zao zilizopo kwenye mfumo na kuepuka madai yasiyokuwa sahihi ambayo yamekuwa yakiletwa na baadhi ya Walipakodi wasiokuwa waaminifu.
“Mfumo wa IDRAS unakwenda kutekeleza matakwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kutaka mifumo ya Taasisi za Serikali isomane ili kuongeza uwazi na uwajibikaji pia kurahisisha utendaji kazi” amesema Bw. Mwenda.






