SIKU ya kwanza baada ya kutoka mapumziko Yanga imefanya mazoezi chini ya kocha msaidizi Patrick Mabedi, kujifua na maandalizi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza kuchezwa Desemba 28 Visiwani Zanzibar.
Jumatatu mastaa wa Yanga walifanya mazoezi ya gym za Gymkhana ya kurejesha ufiti wa mwili na jana jioni walitarajia kuungana na kocha mkuu, Pedro Goncalves ili kuendelea kujifua katika Uwanja wa KMC Complex.
Taarifa za ndani kutoka kwa mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara, zilisema siku mbili hizo za mazoezi wachezaji walikuwa wanatokea nyumbani wakisubiri ratiba ya kuingia kambini kisha kujiandaa na safari ya kwenda Zanzibar kwa ajili ya Mapinduzi.
“Mazoezi ya mwanzo wachezaji walikuwa wanatokea nyumbani, lakini tunasubiri maelekezo ya kocha ambaye anaweza akaungana na timu mazoezi ya jioni (jana Jumanne), ndipo tutajua kama wachezaji wataingia kambini ama nini kitafanyika,” kilisema chanzo hicho.
Katika mazoezi hayo mshambuliaji mpya Emmanuel Mwanengo aliyetokea TRA alijiunga na wenzake kwa ajili ya kuanza kuitumikia klabu hiyo.
“Mwanengo ameishaanza mazoezi na wenzake, hilo litamsaidia kuanza kuyazoea mazingira ya Yanga yapoje na kuuona ushindani halisi ambao utampa taswira ya kupambana zaidi,” kilisema chanzo hicho.
Kwa Bara zinatoka timu nne ambazo ni Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars ambayo tayari imecheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Mlandege mabingwa mara mbili mfululizo 2023 na 2024, iliyofungwa kwa mabao 3-1. Yanga kwenye michuano ya Mapinduzi imepangwa Kundi C ambapo ipo pamoja na KVZ na TRA.
