CCM yashinda ubunge Fuoni | Mwananchi

Unguja. Chama Cha Mapinduzi kimeibuka na ushindi katika uchaguzi mdogo wa mbunge Fuoni Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo usiku huu Desemba 30, 2025 katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Wilaya ya Magharibi B, Msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, Miraji Mwadini Haji amemtangaza Asha Hussein Saleh kuibuka mshindi.

Katika matokeo hayo, Asha amepata kura 9,861 akifuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo, Khamis Shaib Mussa ambaye amapeta kura 503 ya kura zote zilizopigwa.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 14,130, waliopiga kura ni 11,024, kura halali 10,930 na zilizoharibika ni 94.

“Kwa mantiki hiyo namtangaza Asha Hussein Saleh wa CCM kuwa mshindi wa jimbo la Fuoni,” amesema Miraji.

Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi B, Miraji Mwadini Haji (kushoto) akimkabidhi cheti cha ushindi Asha Hussein Saleh (CCM) baada ya kutangazwa mshindi wa ubunge Fuoni katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Wilaya ya Magharib B Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Licha ya ACT kupata nafasi ya pili, lakini chama hicho kimesema hakikushiriki katika uchaguzi huo badala yake Tume imetumia mgombea yuleyule aliyekuwa katika orodha ya wagombea waliokuwapo katika orodha ya uchaguzi mkuu, kabla ya kuahirishwa.

Uchaguzi wa mbunge wa Fuoni umekuja kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Ali Mwinyi ambaye ni kaka yake mkubwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Kifo cha Abbas Mwinyi kilitokea Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Lumumba, Zanzibar.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Asha amewashukuru wananchi waliompigia kura akiahidi kushirikiana nao kuwaletea maendeleo katika jimbo hilo.

“Nawashukuru wananchi wa Fuoni kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi niwe mbunge wao, ninachowaomba tena ni kunipa ushirikiano ili tukaijenge Fuoni kwa maendeleo,” amesema Asha

Baadhi ya waliokuwa wagombea kupitia vyama vvya DP na CUF, wamesema wapo tayari kushirikiana na aliyeshinda kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.

“Uchaguzi umeisha aliyeshinda kashinda, tunampongeza kwa ushindi huo Ila anatakiwa atoe ushirikiano kwa kila mmoja bila kujali chama kwa masilahi ya jimbo letu,” amesema Magirwa Peter Agathon aliyekuwa mgombea kupitia chama cha DP

Naye Ali Fikirini Liwali aliyekuwa mgombea wa CUF, amesema hawana shaka na ushindi alioupata mwenzao, hivyo wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa masilahi ya wananchi.