Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amefanya mabadiliko ya wenyeviti wa bodi wa mashirika mbalimbali.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Desemba 30, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, mhandisi Zena Ahmed Said, imesema uteuzi huo unaanza leo.
Taarifa imesema Makame Hasnuu Makame ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), ambapo awali aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA).
Naye, Sultan Said Suleiman ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), kabla ya mabadiliko hayo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).
Aidha, Dk Mwinyi amemteua tena Dk Abdulhamid Yahya Mzee kuwa Mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC).
Rais Mwinyi amefanya mabadiliko hayo baada ya kupita siku tisa tangu ateue wenyeviti wa bodi ya wakurugenzi Desemba 22,2025.
Katika uteuzi uliofanywa Desemba 22, 2025 Dk Mwinyi aliteua wenyeviti watano kati yao wawili wamefanyiwa mabadiliko na watatu wamesalia kwenye nafasi zao.
Wenyeviti waliosalia kwenye nafasi zao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhani Mohamed, Dk Maudline Cyrus Castico na Dk Idrissa Muslim Hija.
