Mkinga. Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe Tanga iliyopo Kijiji cha Gombero, wilayani Mkinga inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Septemba na Oktoba, 2026.
Hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo na miundombinu mingine.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema hayo jana Desemba 30, 2025 alipotoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Katima, alipofanya ziara kukagua maendeleo ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa kampasi hiyo unaotarajiwa kukamilika Machi, 2026.
Amesema ujenzi wa kampasi hiyo unatekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), uliopatiwa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB) unaotekelezwa katika vyuo vikuu vya umma.
Amesema ujenzi wa kampasi hiyo unatarajiwa kugharimu Sh12 bilioni kwa ajili ya kujenga jengo la taaluma, madarasa sita yatakayohudumia wanafunzi 360, maktaba ndogo itakayokuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 48, duka la vitabu na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 300.
Majengo mengine ni maabara mbili zenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 80 kila moja, ofisi 36 kwa ajili ya watumishi 72, hosteli za wanafunzi wa kike 180 na wa kiume 180 na bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 450.
Pia, kituo cha afya kitakachowahudumia wanachuo na wakazi wa vijiji vya jirani kikiwa na wodi za kulaza wanaume wanane na wanawake wanane, nyumba nne za watumishi kwa kiwango cha familia, mifumo ya majitaka na taka ngumu pamoja na tanki la majisafi lenye ujazo wa lita 400,000.
“Hadi sasa mradi huu umefikia asilimia 85 kilichobaki ni umaliziaji. Kwa mujibu wa mkandarasi ujenzi utakamilika Machi, 2026 ili michakato ya kuomba ithibati na kudahili wanafunzi ianze hatimaye Oktoba tuanze kufundisha rasmi,” amesema.
Kwa upande wake, mshauri elekezi wa usanifu na usimamizi wa mradi huo, Dk Moses Mkoni, amesema ujenzi wa kampasi hiyo unatekelezwa na kampuni ya ukandarasi ya Dimetoclasa Realhope Limited kwa kushirikiana na Mponela Construction Company Limited.
“Ujenzi ulitarajiwa kukamilika Novemba 30, 2025 lakini kutokana na changamoto za upatikanaji wa vifaa, kunyesha kwa mvua na mabadiliko ya kiufundi ikiwamo kuhamisha miundombinu ya majitaka muda umeongezwa hadi Machi, 2026,” amesema.
Msaidizi Mahsusi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Aloyce Gervas amesema miongoni mwa changamoto zinazoukabili mradi huo ni miundombinu mibovu ya barabara yenye urefu wa kilomita 2.4 ya kuingia chuoni, akieleza zinahitajika Sh82 milioni kuitengeneza.
Nyingine ni umeme ambao zinahitajika Sh158 milioni, huduma ya maji inayohitaji Sh1.96 bilioni na eneo la jirani kupangwa ili kuwa rasmi.
Akijibu changamoto hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Katima amesema suala la barabara atalifikisha kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ili iingizwe kwenye bajeti.
Kuhusu changamoto za umeme na maji, amesema atawasiliana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) ili kuhakikisha huduma hizo zinafikishwa haraka.
“Kuhusu upangaji wa eneo jirani na chuo, tayari idara ya ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga imeanza kupima na kuweka michoro,” amesema.
