ALIYEFARIKI DUNIA KWA TUKIO LA KUCHOMWA KISU TUMBONI, FAMILIA YAKE YASEMA IMEAMUA KUMUACHIA MUNGU

Na Mwandish wetu, DAR ES SALAAM

FAMILIA ya marehemu Salehe Iddy Kitambulio iliyopo Zavala, Chanika Manispaa ya Ilala, imesema pamoja na ndugu yao kupokwa uhai wake kwa tukio la mtu kumvamia nyumbani kwake na kumchoma kitu chenye ncha kali tumboni, yenyewe imeamua kumuachia Mungu.

Kauli hiyo imetolewa Disemba 30, 2025 baada ya ndugu kukutana kwa pamoja nyumbani kwa marehemu kwa lengo la kuzungumza na vyombo vya habari hasa kuhusu minong’ono na kauli zisizo rasmi juu ya kifo cha ndugu yao.

“Pamoja na yote yaliyotokea, sisi kama familia na ndugu wa marehemu tunasema tumechagua kumuachia Mungu ili maisha mengine yaendelee,” amesema Ally Athuman mpwa wa marehemu Kitambulio.

Kwa mujibu wa Athuman, tukio la kifo cha Kitambulio lilitokea Disemba 4, 2025 muda mfupi baada ya kuvamiwa nyumbani kwake muda wa alfajiri na mtu aliyejitambulisha kuwa ameelekezwa kuwa Kitambulio ni mganga wa kienyeji hivyo amekuja ili ampatie tiba.

“Kwanza tunaishukuru serikali hasa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, amefika hapa nyumbani kutufariji, pia ameagiza waliofanya tukio hili wasakwe na wakamatwe, sisi tunaamini serikali itafanya kazi yake,” amesema Athuman

Kauli ya Athumani kwamba wanamuachia Mungu, inaungwa mkono na dada wa marehemu, Bi. Asha Kitambulio (78) naye akidai familia haina namna zaidi ya kukubalina na yote yaliyotokea.

Hata hivyo, amesema kitendo cha kaka yake kufariki dunia ghafla bila hata kuugua kimemuuma na kwamba siku alipopewa taarifa za kifo alihisi kuchanganyikiwa lakini hakuna namna zaidi ya kumshukuru Mungu.

“Sisi familia hatuna la kusema kuhusu kifo cha ndugu yetu, yaliyotokea yametokea, tumekubalina na yote japo ni hali isiyoelezeka kirahisi kwani hatukuitegemea,” amesema Asha.

Mpwa mwingine wa marehemu Bi. Zakia Athumani anayeishi Kinyamwezi kwa Mbiki, Ilala, akisimulia namna tukio lilivyokuwa amesema siku ya tukio mtoto wa Kitambulio aliyekuwa amelala ndani alisikia mtu akibisha hodi mlangoni, baba yake akatoka chumbani na kwenda kufungua mlango wa nje ili kumsikiliza.

Anasema kuwa wakati mtoto huyo akiwa ndani amelala alisikia maongezi yote ambapo aliyebisha hodi alimueleza Kitambulio kuwa ameelekezwa kuwa kwenye nyumba hiyo kuna mganga wa kienyeji hivyo anahitaji tiba. Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto, Kitambulio alimueleza muuaji kuwa yeye si mganga wa kienyeji hivyo huenda ameelekezwa vibaya.

Hata hivyo, muuaji aliendelea kushinikiza kuwa hajakosea na yuko sahihi lakini baada ya muda mfupi wa majibizano mtoto akasikia kelele za baba yake nje akilalamika kuvamiwa na kwamba alivyotoka nje akamkuta anagalagala huku utumbo ukiwa nje na damu zinavuja na kutapakaa chini.

“Majirani waliowahi kwenye tukio, wakamuwahisha kituo cha afya cha Nguvukazi, pale walifanya jitihada kuokoa maisha yake, ikashindikana, madaktari wakashauri apelekwe hospitali ya Amana, wakiwa njiani kwenda Amana umauiti ukamkuta,” amesema Zakia.