Dar es Salaam. Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo), limehuzunishwa na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la taasisi hiyo, Bashir Mrindoko, likisema atakumbukwa kwa umahiri na ubunifu katika kuendeleza taasisi na Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo amesema taasisi hiyo inaungana na familia, ndugu na jamaa wa marehemu katika kipindi hiki kigumu, akiomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu.
Mrindoko, aliyewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini zikiwamo za Naibu Katibu Mkuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika awamu ya nne ya Serikali, alifariki dunia Desemba 30, 2025 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumatano Desemba 31, 2025, Profesa Mtambo amesema Mrindoko aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa baraza hilo mwaka 2022 na Oktoba, 2024 aliteuliwa kwa awamu nyingine kutokana na utendaji wake.
“Alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyefuatilia utekelezaji na kusisitiza mipango ikamilike kwa wakati. Kifo chake ni pigo kwetu kama taasisi na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesema alikuwa mtu mwenye upendo, mchapakazi na kiungo muhimu cha kuunganisha taasisi, alipatikana wakati wowote alipohitajika licha ya umri wake.
Profesa Mtambo, amesema taasisi imepata pigo kutokana na kupoteza mchango wa Mrindoko katika sekta ya nishati safi na mbadala.
Amesema alisaidia kuanzisha ushirikiano na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) katika uzalishaji wa mkaa bora unaotokana na makaa ya mawe unaosaidia kupunguza ukataji miti na kulinda mazingira.
Profesa Mtambo amesema alisaidia taasisi kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa) katika miradi ya nishati mbadala.
Ameeleza Mrindoko alisisitiza uwekezaji wa viwanda kwa kubainisha maeneo sahihi ya kanda za viwanda.
“Kupitia juhudi zake, tumekamilisha uainishaji wa kanda za viwanda katika mikoa tisa. Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam na Morogoro) imeshakamilika, Kanda ya Kaskazini (Tanga na Kilimanjaro) na sasa tunakamilisha Arusha, Manyara, Shinyanga na Mwanza,” amesema.
Amesema Mrindoko alisaidia kuimarisha mfumo wa utambuzi wa viwanda nchini kwa kukusanya na kuhifadhi kanzidata ya viwanda, ambayo imesajiliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na tayari viwanda vya mikoa tisa vimeingizwa kwenye mfumo huo, hatua inayorahisisha ufuatiliaji wa maendeleo ya viwanda.
Kuhusu madini ya kimkakati, Profesa Mtambo amesema Mrindoko alianza kuweka mikakati na kusaidia upatikanaji wa fedha za utafiti kwa kushirikiana na Stamico katika mikoa ya Kagera na Singida, ambako maeneo ya madini hayo yameshaanza kuainishwa.
Vilevile, amesaidia taasisi kuimarisha maabara ya nishati ya chakula kwa kupata vifaa vya kisasa, hatua itakayoiwezesha kuhudumia wateja wa kimataifa kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Profesa Mtambo, mwili wa Mrindoko umeagwa leo Desemba 31, 2025 jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kusafirishwa kwenda Usangi, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro ambako mazishi yatafanyika kesho, Januari Mosi, 2026.
Mrindoko pia amewahi kuwa kamishna wa nishati na mafuta ya petroli katika Wizara ya Nishati na Madini.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema katika kipindi cha uongozi wake, Mrindoko alitoa mchango katika kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa.
Amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ni kuundwa Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Taarifa za Viwanda (NIIMS), unaosaidia kuongeza uwezo wa ufuatiliaji wa maendeleo ya viwanda na uwekezaji nchini.
“Uundaji wa mfumo wa NIIMS ni mojawapo ya kazi zilizofanyika kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wake,” amesema.
Pia, alifanya ukaguzi wa vifaa vya uhandisi kwa kutumia mbinu za kisasa (NDT), katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, jijini Dodoma, pamoja na kufanya tathmini ya athari za mazingira katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), unaoendelea kwa awamu ya pili.
Kapinga amesema wizara itaendelea kumkumbuka Mrindoko kama kiongozi mahiri aliyejitolea muda wake mwingi kufuatilia na kutatua changamoto za ndani ya Tirdo kwa masilahi ya Taifa.
