Polisi Tanga wajipanga kulinda usalama mkesha wa mwaka mpya

Tanga. Jeshi la Polisi limewashukuru wakazi wa Mkoa wa Tanga kwa kumaliza mwaka 2025 kwa amani na utulivu, jambo linalowavutia wawekezaji na watalii.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema hayo leo Desemba 31, 2025 alipokuwa akiwasilisha salamu za kuuga mwaka 2025 kupitia waandishi wa habari.

Amesema mwaka 2025, Mkoa wa Tanga umekuwa amani na utulivu uliotokana na wakazi wake wakiwamo vijana kuamua kujiepusha na matendo ya vurugu.

“Niwashukuru wakazi wa Mkoa wa Tanga kwa kumaliza mwaka 2025 kwa amani na utulivu wa hali ya juu…niwaombe waendeleze kwa mwaka ujao,” amesema Mchunguzi.

Amesema katika kuelekea sikukuu za kuukaribisha mwaka mpya, Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha usalama kwenye maeneo yote kwa kufanya doria katika maeneo ya fukwe pamoja na mitaa ya katikati na pembezoni mwa jiji

“Ni marufuku kwa mtu yeyote kupiga fataki bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika…hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka,” amesema Mchunguzi.

Kuhusu usalama barabarani, Kamanda huyo amewataka watembea kwa miguu na waendesha vyombo vya moto kufuata sheria na taratibu za usalama ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Watu waliozungumza na Mwananchi kuhusiana na salamu hizo za Kamanda Mchunguzi wamesema zinatokana na Tanga kuwa miongoni mwa mikoa ambayo havikutokea vitendo vya maandamano wala uvunjifu wa amani.

“Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo vijana na wananchi wake walijiepusha na maandamano na uvunjifu wa amani…hii imeujengea sifa ya kuwa ni eneo lenye utulivu,” amesema Kiama Mwaimu.