Kelvin Kijili kuibukia TRA United

TRA United imetuma ofa Singida Black Stars ya kumtaka beki wa kulia, Kelvin Kijili, ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya raundi ya pili msimu huu.

Kijili aliyeitumikia Simba msimu uliopita alirejea Singida msimu huu na kusaini mkataba wa miaka miwili ambao utamalizika mwakani.

Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa TRA amesema Kijili amekuwa chaguo la kocha Etienne Ndayiragije kwani aliwahi kufanya naye kazi KMC.

Amesema tayari wameshatuma ofa Singida Black Stars ili kuangalia uwezekano wa timu hizo kukaa mezani na kufanya mazungumzo kwani bado mchezaji ana mkataba wa mwaka mmoja na miezi sita na klabu hiyo.

“Tumetuma ofa kwa Singida kumtaka Kijili, lakini bado dili halijakamilika, kwani wameomba muda kufikiria kwa kina na hili limetokea kwa sababu ya hii taarifa ya kufungiwa kusajili.

“Singida kwa sasa wanataka kuona hilo linamalizika kwanza, ila kwa upande wetu tunatimiza matakwa ya kocha kwani ndiye alimhitaji. Kama tutafanikiwa basi tutaweka kila kitu wazi kwani Kijili sio mchezaji mbaya ana kiwango kizuri na anaweza kuisaidia timu.” amesema.

Kwa upande wa Singida Black Stars taarifa za ndani zilidai: “Singida itakunjua mikono kwa TRA kwa sababu tayari imeshashusha beki mwingine kutoka KMC Abdallah Said ‘Lanso’.”

Kijili ambaye aliwahi kuichezea KMC na Fountain Gate ambako aliwaka  na kuwashawishi mabosi wa Simba kumvuta Msimbazi msimu uliopita ambako alicheza msimu mmoja na kutimkia Singida Black Stars.

TRA iliyopo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea Zanziabr hadi sasa imecheza mechi saba za Ligi Kuu Bara ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza miwili, ikiwa na pointi tisa ikishika nafasi ya 10 katika msimamo wa michuano hiyo inayotarajiwa kurejea viwanjani kuanzia Januari 21 baada ya kusimama kupisha fainali za Afcon 25.