WAKATI kipa namba mbili wa klabu ya Simba Yacoub Seleman, akipelekwa hospitali iliyoko nchini Morocco kwa matibabu, hatma ya kipa mpya imeachwa mikononi mwa kocha Steven Barker.
Rasmi Simba imempeleka Yacoub kupata matibabu kwenye hospitali ileile ambayo kipa namba moja Moussa Camara alitibiwa, huku Wekundu hao wakisimamia matibabu yake licha ya kwamba aliumia kwenye majukumu ya timu ya taifa.
Ikumbukwe kuwa huyo anakuwa kipa wa pili ndani ya msimu mmoja kupata majeraha ya goti kwa upande wa Simba, huku matatizo hayo yakiwakumba wakiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa.
Huku Simba sasa imeanza harakati za kusaka kipa mpya na maswali ni kama atakuwa mzawa au mgeni, kutokana na uwepo wa Camara, lakini kwa upande wa Wekundu hao wanachozingatia zaidi ni ubora pekee.
Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa, Simba imemwachia kocha hatma ya kipa mpya, huku ikisuka mipango kama ile iliyofanya kwa Ayoub Lakred msimu uliopita kama mambo yatakuwa magumu.
“Simba kwa sasa inasubiri kocha atoe uamuzi kulingana na hali ya Camara kwa sababu macho yote yapo kwenye hizi mechi muhimu zitakazochezwa Januari za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance de Tunis, kama ataridhishwa na viwango vya wazawa basi watasajili, lakini ikishindikana itatumika mbinu nyingine.
“Ila asiporidhishwa navyo itabidi wasake mgeni halafu Camara watazungumza naye wamuondoe kwenye usajili ili kumpisha kipa mgeni ambaye ataisaidia timu katika michuano ya kimataifa.”
Ikumbukwe kuwa, Camara amesalia na mkataba wa miezi sita tu ndani ya Simba, huku ripoti ya majeraha yake ikimtaka akae nje kwa wiki 10 ambazo zitamalizika Februari mwishoni mpaka Machi mwanzoni.
Kutokana na changamoto ya majeraha ya makipa
Simba imeendelea kufanya mazungumzo na makipa wawili wazawa, ingawa asilimia kubwa inaonekana kuweka nguvu kwa Yona Amos wa Pamba aliyemaliza msimu uliyopita na cleansheets 11.
Kipa mwingine ambaye wameanza mazungumzo naye ni wa Mashujaa, Patrick Munthari aliyemaliza na cleansheets 12 msimu uliyopita na amebakiza miezi sita na timu hiyo.
Chanzo cha ndani kinasema: “Viongozi wanaangalia uwezekano mkubwa wa kumpata Amos, lakini ikishindikana basi chaguo la pili ni la Munthari wa Mashujaa.”
