Rais Samia atoa zawadi za mwaka mpya kwa wenye mahitaji maalumu Moshi

Moshi. Zikiwa zimesalia saa chache kuukaribisha mwaka mpya 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa watoto 190 wenye ulemavu pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu.

Msaada huo ni mchele kilo 100, ngano kilo 50, mbuzi wawili, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, sukari kilo 25 na vinywaji, vimekabidhiwa leo Desemba 31 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga kwa niaba ya Rais, katika kituo cha The Creator Share Foundation kilichopo Kata ya Kirua Vunjo kusini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Nderiananga ametoa wito kwa jamii kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia makundi ya wenye mahitaji maalumu ili kukuza umoja na mshikamano katika Jamii.

Nderiananga amesema, ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais  ameendelea kuleta faraja, upendo, tumaini na umoja kwa Watanzania huku akisema kuwa kitendo hicho ni ishara ya upendo   kwa wananchi bila kujali hali zao.

“Naomba nitumie fursa hii kuwatakia kheri ya sikukuu ya mwaka mpya wa 2026 twende tukasherehekee kwa amani na tukiwa na faraja kwa sababu Rais ametukumbuka sisi ni watoto wake, hivyo tudumishe upendo huu miongoni mwetu kila mmoja amuone mwenzake ni wa muhimu katika jamii,” amesema Nderiananga.

Nderiananga ametoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa kuwahudumia na kuwasaidia watoto na watu wenye mahitaji maalumu ili kuwapa faraja na kuwaonyesha upendo katika jamii.

“Kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia watoto na watu wenye mahitaji maalum katika jamii, siyo tu kwa siku za sikukuu, bali kwa muda wote ili kuwapa faraja na huo ndio upendo tunaotakiwa kuwaonesha,”amesema Nderiananga

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava ameitaka jamii kuwakumbuka na kuwaonyesha upendo wa hali na mali wenye uhitaji maalumu katika jamii ili kuwafanya nao wajione kama watu wengine.

“Ili kuwa na ustawi wa maisha ya kijamii ni lazima kuwajali watu wenye uhitaji katika jamii zetu   ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku,”amesema DC Mnzava

Akizungumza, Diwani wa Tarafa ya Vunjo Magharaibi, Pamela Chuwa amemshukuru Rais Samia kwa kuwafikia watu wenye ulemavu hatua inayowafanya kujisikia kuwa ni sehemu ya jamii inayowazunguka.

Kwa upande wake, mmoja wa viongozi kutoka kituo hicho, Judith Shio amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa upendo na kuwajali watu wenye mahitaji maalumu, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitolea ili kuendelezwa moyo wa upendo na faraja kwa makundi hayo.