UONGOZI wa Singida Black Stars una mpango wa kumtoa kwa mkopo nahodha wa timu hiyo, Kennedy Juma kwenda Mashujaa ambako umemng’oa Abdulmalik Zakaria.
Zakaria anayecheza beki wa kati tayari ameshaanza kazi akiitumikia timu hiyo katika michuno ya Kombe la Mapinduzi 2026 akiwa sambamba na Abdallah Kheri ‘Sebo’ waliojiunga na timu hiyo dirisha dogo la usajili lililofunguliwa leo, Alhamisi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji wengi watapunguzwa kupisha usajili mpya kutokana na ripoti ya kocha.
“Ni kweli jina la Keneddy ni miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa kutolewa kwa mkopo dirisha hili, hivyo mambo bado hayajakamilika yakienda kama yalivyopangwa atatua Mashujaa.
“Mashujaa iliomba mpango huo ufanyike baada ya kumnasa beki wao Zakaria. Mazungumzo baina yetu na klabu yameenda vizuri, bado mchezaji mwenyewe kuamua maana atapewa nafasi ya kuchagua nafasi ya kucheza,” kilisema.
Chanzo hicho kilisema nafasi ya kucheza kwa Kennedy itakuwa ngumu chini ya kocha Gamondi kutokana na mchakato wake alioupanga, hivyo ametoa nafasi ya kuzungumza na wachezaji hao waweze kutolewa kwa mkopo.
“Keneddy anafahamu hili suala kwani uongozi mara baada ya kupokea ripoti ulifanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao wamewekwa kwenye ripoti kupisha usajili mpya.”
