TRC yasitisha safari za SGR Morogoro–Dodoma kwa muda, yataja sababu

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kusitisha kwa muda safari za treni ya reli ya kisasa (SGR) kati ya Morogoro na Dodoma kuanzia leo Desemba 31, 2025, kufuatia uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua kubwa.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, Desemba 31, 2025, na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imesema, mvua hizo zimesababisha athari katika maeneo ya Kidete wilayani Kilosa mkoani Morogoro na Godegode wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, hali iliyolazimu shirika hilo kuchukua hatua ya kusimamisha safari hizo kwa ajili ya usalama wa abiria.

Kutokana na hali hiyo, TRC imesema kuwa kwa sasa safari zote za SGR zitahudumia njia ya Dar es Salaam–Morogoro na Morogoro–Dar es Salaam pekee hadi pale matengenezo yatakapokamilika na usalama kuthibitishwa.

“Tunawaomba abiria wetu kubadili ratiba za safari zao kulingana na mabadiliko haya ya muda,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Oktoba 23, 2025 TRC ilisitisha safari za SGR kwa muda baada ya  treni ya Electric Multiple Unit (EMU) maarufu kama treni ya mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma  kupata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.

Hatua hiyo, ilisababisha abiria wanaotumia usafiri huo kulazimika kusubiri kwa muda usiojulikana.

Desemba 28, 2025 TRC ililazimika kuongeza safari za treni ya SGR ili kuwahudumia abiria waliopata usumbufu uliojitokeza kutokana na mvua zilizonyesha na kuathiri miundombinu ya reli hiyo na sambamba na ratiba ya SGR.

Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, wakati huduma hizo zikiwa zimeathirika, baada ya  baadhi ya abiria kushindwa kuanza safari zao kulingana na ratiba iliyopangw