Dar es Salaam. Serikali katika kuuanza mwaka 2026, imejipanga kujenga umoja wa kitaifa nchini.
Rais Samia Suluhu Hassan, amesema hayo katika hotuba kwa ajili ya kuuaga mwaka 2025 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2026, aliyoitoa leo Desemba 31, 2025 akiwa Tunguu, Zanzibar.
Kauli hiyo ameitoa akirejea yaliyotokea Oktoba, 2025, ambapo Tanzania ilipitia nyakati ngumu alizosema zilihitaji subira, mshikamano na uzalendo.
Oktoba 29, 2025 wakati wa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais ziliibuka vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali.
“Hatua za kuunda tume ya maridhiano zimeanza kuchukuliwa. Serikali itashirikiana na wadau wote katika kukubaliana kuhusu muundo wa tume, aina ya wajumbe, majukumu yao na muda wa kazi wa tume hiyo,” amesema.
Ametoa rai kwa Watanzania akieleza wanapoendelea kulijenga Taifa, wasikubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo ziwagawe na kuwapotezea malengo ya maendeleo na ustawi wa Taifa.
“Sote tunafahamu kuwa, tofauti ni sehemu ya demokrasia, lakini zisitumike kuligawa Taifa la Tanzania,” amesema na kuongeza:
“Narudia kusema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu; ndani ya Jamhuri hiyo kuna Watanzania, ambao wamejengwa na itikadi ya kuamini kwamba amani, umoja na mshikamano hujenga uzalendo na ndiyo virutubisho vinavyotuletea maendeleo endelevu na ustawi wa Watanzania.”
Akirejea yaliyotokea mwaka 2025, Rais Samia amesema kiungo kingine cha maendeleo ni uwepo wa utulivu wa kisiasa na hali ya amani na usalama nchini.
Amesema mwaka 2025, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, Taifa lilipitia pia changamoto na mitihani iliyowagusa wote.
“Itakumbukwa kuwa Oktoba, mwaka huu, tulipitia nyakati ngumu zilizohitaji subira, mshikamano na uzalendo,” amesema na kuongeza:
“Kwa dhati kabisa, ninavishukuru vyombo vyetu vya ulinzi na usalama nchini na wananchi wote kwa ujumla, kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu. Tumeweza kuuthibitishia ulimwengu kwamba Tanzania ni Taifa imara, himilivu na lenye kujitahidi kushughulikia changamoto zake.”
Rais Samia, Novemba 14, 2025 akilifungua rasmi Bunge la 13 jijini Dodoma, ikiwa ni siku 17 baada ya vurugu zilizotokea, alieleza hatua ambazo Serikali ilikuwa imechukua ili kudumisha umoja wa kitaifa.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuunda tume kuchunguza vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 ili kubaini kiini cha tatizo, kuwezesha kufanyika mazungumzo ya kuleta maelewano na amani.
Mbali ya hayo, alitangaza msamaha kwa vijana waliofikishwa mahakamani kwa kesi za uhaini kwa kufuata mkumbo wa kushiriki kwenye vurugu.
Kutokana na matukio hayo, Novemba 18, 2025 Rais Samia aliunda tume kuchunguza matukio hayo inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande ambayo aliizindua Novemba 20 na sasa inaendelea na kazi.
Samia amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwamo utekelezaji wa ahadi za siku 100 zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Serikali itatoa taarifa kwa umma baada ya kutimia siku 100 Februari, 2026,” amesema.
Miongoni mwa ahadi hizo ni kuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba na kuunda Tume ya Usuluhishi na Maelewano.
Katika hotuba ya kulifungua Bunge, Rais Samia alisema ingawa dhamira yake ya maridhiano wakati wa muhula wake wa kwanza wa uongozi ilikatishwa na baadhi ya wadau, katika awamu hii hatachoka kunyoosha tena mkono wa kufanikisha hilo.
Samia amesema kwa ujumla, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uchumi wa Taifa, ikiwamo kudhibiti mfumuko wa bei hasa za chakula.
Kwa mwaka 2025, amesema wastani wa mfumuko wa bei nchini ni asilimia 3.4, huku pato la Taifa likiendelea kukua kufikia asilimia 5.8 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ya mwaka uliopita 2024.
“Vilevile, deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu. Serikali inaendelea na mipango ya kulipa kwa haraka mikopo ya zamani yenye riba kubwa, na kurefusha muda wa kulipa mikopo, hatua itakayosaidia kupunguza kiasi cha riba iliyokuwa ikilipwa na kutoa ahueni kwa Serikali katika kulipa mikopo hiyo,” amesema.
Amesema ukuaji wa uchumi umetokana na uwekezaji wa Serikali katika miradi ya kimkakati ya miundombinu, pamoja na mchango mkubwa wa sekta za madini, kilimo, ujenzi na sekta ya fedha na huduma, ikiwamo utalii.
Rais Samia amesema akiba za fedha za kigeni imeendelea kuimarika na kufikia Dola bilioni 6.6 za Marekani, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano.
Amesema mwaka 2026 utaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050, ambapo Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa muda wa kati wa miaka mitatu (2025/2026 – 2027/2028) wa kuongeza mapato ya Serikali kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, kufanya malipo na kuongeza umakini katika usimamizi wa fedha na rasilimali za umma.
Amesema kufanya kazi kwa bidii, mshikamano na uzalendo, pamoja na kutimizwa kwa malengo huleta uendelevu wa maendeleo.
“Hivyo basi, Serikali itachukua hatua za kimkakati kuweka mazingira rafiki ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayoongeza fursa za biashara, uwekezaji na fursa nyingine za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Watanzania wote,” amesema.
Wakati huohuo, amesema wataendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi bila kusahau wajibu wa kulinda rasilimali za nchi ili zitumike kwa manufaa ya Taifa.
Katika kipindi cha miezi saba kuanzia Mei hadi Oktoba, 2025 amesema kulikuwa na uhaba wa mvua, hali iliyoleta ukame na kupungua kwa vyanzo vya maji.
“Nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine yote ambayo kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama,” amesema.
Katika kukabiliana na hali hiyo, hususani kwa Dar es Salaam, amesema Serikali ilihakikisha kuwa vyanzo vyote vya maji vilivyo karibu vinaelekeza maji jijini humo, pamoja na kufufua visima vilivyokuwa havifanyi kazi.
“Tunamshukuru Mungu kwamba mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya Desemba zinaongeza kina cha maji kwenye vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini na zinarejesha hali nzuri ya upatikanaji wa maji,” amesema.
Vilevile, amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa maji wa Kimbiji Mpera ili kuondoa kabisa shida ya maji mkoani Dar es Salaam na mikoa jirani, hata katika hali ya ukame.
“Hata hivyo, katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka (Novemba na Desemba), maeneo mengine ya nchi yameshuhudia mvua na upepo mkali ulioleta hasara na kubomoka kwa nyumba na kupoteza maisha. Kwa masikitiko makubwa tunatoa pole kwa wote waliofikwa na kadhia hiyo,” amesema.
Ameagiza kamati za maafa za wilaya kuchukua hatua stahiki ili kuwasaidia wananchi hao, akisema ni vyema kwa mikoa iliyopata mavuno mazuri, kuweka akiba ya chakula ili kifae katika siku za usoni.
Wajibu kikanda, kimataifa
Samia amesema katika mwaka 2025, Serikali imetimiza majukumu yake nchini, kikanda na kimataifa.
Amesema ilitimiza kikamilifu wajibu wa uanachama katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola, Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na Umoja wa Mataifa (UN).
“Tumetimiza wajibu wetu wa kulipa ada za uanachama, kushiriki mikutano, kujenga haiba na kuilinda heshima ya Taifa letu na kutoa mchango wetu kwenye shughuli za kimaendeleo, mazingira, siasa, ulinzi na usalama duniani,” amesema.
Amesema mwaka 2026 Tanzania itaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda.
Vilevile, itaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kujenga ustawi wa watu wake, sambamba na kusimamia ulinzi wa Taifa na mchango wake katika amani na usalama barani Afrika na duniani kwa ujumla.
