Nangu: Kuna tofauti kubwa kati ya Simba na JKT Tanzania

BEKI wa kati wa Simba aliyepo katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars, Wilson Nangu amesema kuna utofauti kubwa ya kimaisha na kisoka kati ya timu aliyotoka JKT Tanzania na kule alioko kwa sasa Msimbazi, huku akianika kinachombeba awapo uwanjani.

Simba ilimsajili Nangu kwa mkataba wa miaka mitatu, baada ya kufanya vizuri msimu uliyopita akiwa na JKT Tanzania ambapo alifunga mabao mawili na asisti mbili.

Katika stori za hapa na pale na Mwanaspoti, alipulizwa ni utofauti upi anauona akiwa mtaani kwa sasa anapokutana na mashabiki akitofautisha na alipokuwa JKT Tanzania? Alijibu: “Simba ni klabu kubwa yenye mashabiki wengi, lazima utofauti utakuwepo.

“Japo kinachofanya nisione mabadiliko makubwa washikaji wangu ni wale wale tangu nipo JKT Tanzania na sasa Simba pia nikitoka kufanya mazoezi napenda kupumzika ili kuupa mwili nguvu ya kupambana.

“Kama unavyojua kazi yetu bila kufanya mazoezi kwa bidii ni ngumu, hivyo inahitaji kupumzika baada ya mazoezi, nadhani nimekujibu kwa kifupi sitaki kuzungumza sana, ila hiki ndicho kinachonibeba uwanjani.”

Nyota wa TRA United (zamani Tabora United), Ramadhan Salum Chobwedo amemzungumzia Nangu aliyedai ni mshkaji wake wa karibu kwamba, ni mchezaji mpambanaji na mwenye kujituma kwa bidii katika kufanya mazoezi.

“Nangu ni mwanangu, anajituma naamini katika bidii yake ipo siku itamlipa, kama unavyojua mpira wa miguu lazima uwe na nidhamu na mazoezi,” amesema Chebwedo aliyepo na TRA katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea visiwani Zanziba ikiwa Kundi C sambama na KVZ na Yanga.