Steve Barker aanza na gia kubwa Simba

KIKOSI cha Simba tayari kipo visiwani Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya kuondoka jijini Dar es Salaam asubuhi ya jana, huku ikibainika kuwa kocha mpya wa Simba, Steve Barker ameanza na gia kubwa kwa kubadilisha baadhi ya mambo ndani ya kambi ya timu hiyo.

Simba imepangwa Kundi B katika michuano ya Mapinduzi na inatarajiwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Muembe Makumbi kabla ya kumalizana na Fufuni, lakini kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam kocha huyo aliyetua hivi karibuni akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini amefanya mabadiliko kadhaa ndani ya kikosi hicho.

Michuano hiyo ya Mapinduzi inayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja ndio kipimo cha kwanza kwa kocha Barker, huku Simba ikiwa na rekodi tamu ya michuano hiyo ikicheza fainali 10 na kutwaa ubingwa mara nne ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara Azam yenye mataji matano tangu mwaka 2007.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Simba haijampa presha kubwa kocha huyo katika michuano hiyo kutokana na ukweli haijafanya maandalizi ya kutosha kwa vile wachezaji waliokuwa kambini ni wachache baada ya wengine kuwa katika timu za taifa zinazoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea huko Morocco.

Lakini kocha Barker ametakiwa kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho ambayo kwa misimu minne mfululizo inashikiliwa na Yanga, pia kufika angalau nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikiwa Kundi D na kwa sasa inaburuza mkia baada ya kupoteza mechi mbili za awali dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali na sasa inakabiliwa na kibarua mbele ya Zamalek ya Misri mwezi huu.

Simba itacheza mechi mbili mfululizo na Zamalek inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa katika msimamo wa kundi hilo nyuma ya Petro na Malien zenye alama nne kila mmoja, wakati Wekundu wa Msimbazi wakiburuza mkia bila pointi wataanzia ugenini Januari 23 na kurudiana nao jijini Dar es Salaam Januari 30.

Baada ya mechi hizo mbili, itaifuata Petro kurudiana nao Februari 6 na kumalizia mechi za makundi ikiwa nyumbani dhidi ya Stade Malien wiki moja baada kufunga hesabu ili kuona kama itavuka kwenda robo fainali au la.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya Simba, kocha Barker ametakiwa pia kuhakikisha anatimiza malengo ili kuendana na matarajio ya klabu hiyo, lakini mwenyewe ameshaanza na mabadiliko katika utaratibu wa kikosi hicho, akitaka wachezaji wakae kambini kwa muda mrefu, pia sasa mazoezi ni mara mbili hadi tatu kwa siku.

MASTA 01

“Huyu kocha ndio anaanza kutengeneza benchi lake, lakini anaonekana kuwa na misimamo mikali na moja ya mambo ambayo ameshawaambia wachezaji wake ni kwamba anafanya kazi na mchezaji mwenye nidhamu, anayesikiliza na kujituma mazoezini,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.

“Amesema kwa sasa ambapo timu ipo Mapinduzi na hata ikirudi Dar itakaa muda mwingi kambini tofauti na ilivyokuwa kipindi cha Dimitar Pantev ambaye timu ilikuwa inaingia kambini siku mbili kabla ya mechi, lakini hata mazoezi yatakuwa mara mbili kwa siku hadi tatu,” kiliongeza chanzo hicho kilichosisitiza;

“Amesema pia kutakuwa na mazoezi ya asubuhi, jioni na wakati mwingine wachezaji wataanzia kwenye mazoezi ya Gym asubuhi au jioni ndipo waende katika mazoezi ya uwanjani. Kuna vitu vingi kabadilisha, kuna hata suala la chakula kuna jinsi anavyotaka wachezaji wakiwa kambini wale, naona kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye kipindi chake tofauti na watangulizi wake.”

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, kabla hajajiunga na Simba alikuwa kocha mkuu wa Stellenbosch inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambayo ilikutana na Simba katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kutupwa nje kwa jumla ya bao 1-0. Simba katika fainali ilishindwa kutamba mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1 ikianza na kipigo cha 2-0 ugenini kisha kutoka sre ya 1-1 Zanzibar.

Simba inatafuta ubingwa wa kwanza baada ya kupita misimu minne mfululizo iliyopita ambapo watani wao, Yanga wamebeba mara zote katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, lakini inataka kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo kwa misimu sita tofauti iliyopita imefika hatua ya robo fainali.

MASTA 02

Hadi timu inaondoka jijini Dar es Salaam kuna mastaa watatu hawajajiunga na timu hiyo na kumfanya Barker awachie mabosi wa klabu hiyo ujumbe kwamba wawasiliane na wachezaji hao kuwaambia ndani ya siku tatu wawe wamewasili Unguja.

Wachezaji ambao hawajawasili mpaka sasa kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji Jonathan Sowah, viungo Ellie Mpanzu na Jean Charles Ahoua ambao wametoa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, Barker hajakubali utetezi huo bali amewataka wachezaji hao haraka kambini akitaka kufuatilia ubora wao kabla ya kuanza hesabu zake za kutengeneza kikosi chake.

Bosi mmoja wa Simba ameliambia Mwanaspoti, tayari simu zao zimeshawafikia wachezaji hao kuwajulisha kwamba wakatishe wanayoyafanya kutokana na tamko la kocha wao huyo raia wa Afrika Kusini.

“Kila mmoja alikuwa na udhuru yake, lakini kwa agizo hili la kocha lazima litekelezwe hatutaki kumkwamisha, anachotaka (Barker) ni kuwafahamu wachezaji wote kwa haraka,” amesema bosi huyo.

“Wachezaji pekee ambao wanakuwa salama kwenye agizo hili ni wale ambao wako AFCON 2025 kwa mfano kama Mukwala (Steve) ambaye ameshatoka kuna siku chache tu atapewa na baada ya hapo atatakiwa hapa haraka.

“Hawa wengine ambao wako Stars anawafuatilia kwa karibu sana kuna vitu anafuatilia kila mchezaji wetu anavyopata nafasi.”

Pigo la kwanza kwa Barker ni kwamba hesabu zake za kutaka kumleta kocha wake msaidizi wa kwanza Maahier Fadlu zimekwama baada ya Msauzi huyo kushindwa kuafikiana na Wekundu hao.

Maahier ambaye ni mdogo wa Fadlu Davids uwezekano wa kuja nchini kuungana na Barker utakuwa mgumu na kutokana na hatua hiyo, sasa atabaki na Seleman Matola kama msaidizi wa kwanza.

Aidha, aliyekuwa kocha wa mazoezi ya viungo Riedoh Berdien amekubaliana kuachana na wekundu hao hatua ambayo Simba inapiga hesabu za kumbakisha kocha Mohammed Mrishona ‘Xavi’ kufanya kazi na Sibusiso Makhula aliyekuja na Barker.