Himid Mao atoboa siri ya ubora wake

KIUNGO wa Azam FC, Himid Mao ametoboa siri ya ubora wake akisema unachangiwa na namna ambavyo anayapokea majukumu kutoka kwa kocha na kuyatimiza inavyotakiwa.

Mao amebainisha hayo baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi ya Kundi A katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 wakati wakitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, Desemba 31, 2025.

Michuano hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, Azam inapambana kuhakikisha inabeba ubingwa wa sita na kuzidi kuwa timu yenye mataji mengi ya Mapinduzi.

“Kikubwa nafikiri ni kutimiza majukumu kwa asilimia kubwa ambayo huwa napewa niyafanye katika kila mechi ikiwamo kufika kwa wakati kwenye maeneo kuwadhibiti wapinzani. Lakini kama unaweza kutimiza majukumu bila ya ushirikiano mzuri na wenzako sidhani kama inaweza kutokea hivyo. Napenda kusema ubora wangu unachangiwa pia na wachezaji wenzangu ninaoshirikiana nao ndani ya uwanja,” amesema Mao.

Kwa sasa Mao ndiye nahodha wa kikosi cha Azam katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 akichukua mikoba ya Lusajo Mwaikenda ambaye yupo Morocco na kikosi cha Taifa Stars kinachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Africa (AFCON 2025).

Mao anayecheza eneo la kiungo mkabaji, ni lejendi wa Azam, amekuwa na kikosi hicho kuanzia timu za vijana tangu 2009 hadi 2018 alipoenda Misri kucheza soka la kulipwa.

Huko Misri amekaa kwa kipindi cha miaka saba akizichezea timu za Petro Jet (2018-2019), ENPPI (2019-2021), El Mahalla (2021-2023) na Talaea El Gaish (2023-2025), kisha Julai 2025 amerejea Azam.