Ujenzi wa viwanda vya nguo, dawa za binadamu kupunguza gharama za uagizaji Zanzibar

Unguja. Ujenzi wa viwanda vya nguo na dawa za binadamu katika eneo la viwanda Dunga Zuze, Mkoa wa Kusini Unguja, umetajwa kuwa suluhisho la kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi na kuhakikisha upatikanaji wa haraka na wa bei nafuu kwa wananchi wa Zanzibar.

Hayo yamebainika leo, Januari 2, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi wa viwanda vya nguo vya Mama Africa Textile Co Ltd na vya dawa za binadamu vya Africa Bio Chem Co Ltd, miradi inayogharimu jumla ya Sh205 bilioni na inayotarajiwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 600.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff, amesema sekta ya viwanda ni mhimili muhimu wa uchumi kwa kuwa bidhaa zake ndizo zinazouzwa na kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine.

“Tunakusudia kupunguza utegemezi wa bidhaa za viwandani kutoka nje ya nchi. Ndiyo maana Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia wawekezaji zaidi,” amesema Shariff.

Hata hivyo, ameitaka Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kuwachukulia hatua wawekezaji waliopatiwa maeneo, lakini wameshindwa kuyaendeleza kwa muda mrefu.

“Serikali haipo tayari kuchezewa. Wote waliokabidhiwa maeneo na kushindwa kuyaendeleza wachukuliwe hatua na wanyang’anywe maeneo hayo ili wapewe wawekezaji wenye nia ya dhati,” amesema.

Amesisitiza pia utekelezaji wa Sheria ya Uwekezaji Namba 10 ya mwaka 2023 inayotaka asilimia 90 ya ajira zitolewe kwa wazawa, huku asilimia 10 pekee zikibaki kwa wageni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dk Habiba Hassan Omar amesema eneo la viwanda Dunga Zuze, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, lina ukubwa wa ekari 61.83 na ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika mpango wa kuendeleza sekta ya viwanda Zanzibar.

Amesema Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilometa 7.83, mradi uliotekelezwa na Kampuni ya CCECC ya China kwa gharama ya Sh23.367 bilioni.

Meneja wa kiwanda cha Mama Africa Textile Co Ltd, Rashid Salim akimuonyesha Waziri wa Kazi na Uwekezaji bidhaa za nguo itakayozalishwa katika kiwanda hicho wakati wa hafla ya kuweka mawe ya msingi katika eneo la Viwanda, Zuze Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Ameongeza kuwa miradi mingine iliyokamilika ni pamoja na ujenzi wa tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, uchimbaji wa visima vitatu pamoja na usambazaji wa mabomba ya maji katika eneo lote la viwanda, kwa gharama ya Sh3.467 bilioni.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, amesema wizara imepanga kuendeleza zaidi eneo hilo kwa ujenzi wa ukuta na mabanda ya viwanda, mradi ambao tayari mkataba wake umeshasainiwa na Kampuni ya CCECC kwa gharama ya Sh32.748 bilioni.

Dk Habiba amesema jumla ya wawekezaji 12 wamepatiwa maeneo katika eneo hilo, kati yao watano wameshapewa mikataba ya ukodishwaji huku wengine saba wakipewa barua za dhamira.

“Kukamilika kwa miradi hii kunatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 600 kwa wananchi wa Zanzibar,” amesema.

Bidhaa zitakazozalishwa ni pamoja na vifaa vya umeme, vifaa vya ujenzi, nguo, dawa za binadamu, vyuma, plastiki, alumini, mbao na chuma.

Amesema hadi sasa viwanda sita vimeanza ujenzi, vitatu vimewekewa mawe ya msingi na vingine viko katika hatua za awali, huku jumla ya uwekezaji ukiwa Sh205 bilioni.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa wizara imebadilisha mfumo wa ukodishwaji wa maeneo kwa kuwataka wawekezaji kufikia angalau asilimia 20 ya uwekezaji ndani ya miezi mitatu kabla ya kupewa mkataba kamili, vinginevyo maeneo hayo yananyang’anywa.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Mama Africa Textile Co Ltd, Rashid Salim, amesema ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini umeongeza ari ya kuwekeza Zanzibar.

Amesema kiwanda hicho kitajihusisha na uzalishaji wa kanga na batiki, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, ameomba serikali kuboresha taratibu za usafirishaji wa bidhaa kwenda Tanzania Bara, Afrika Mashariki na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Bidhaa zikikaguliwa kwa haraka zitafika sokoni mapema na kuongeza mnyororo wa thamani,” amesema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Africa Bio Chem Co Ltd, Du Gongming, amesema Afrika kwa sasa inaagiza kati ya asilimia 90 hadi 99 ya dawa kutoka nje ya bara hilo, hali inayofanya dawa kuwa ghali na kuchelewa kufika kwa wagonjwa.

“Kwa kuzalisha dawa hapa Zanzibar, tutaongeza upatikanaji wa dawa muhimu na kuokoa maisha, kwani ucheleweshaji wa dawa mara nyingine husababisha vifo,” amesema.

Amesema uzalishaji wa ndani utapunguza gharama za dawa kwa takribani asilimia 30 kutokana na kuondoa gharama za usafirishaji na ushuru wa uagizaji.

Ameeleza kuwa uamuzi wa kuwekeza Zanzibar umetokana na miundombinu bora iliyowekwa na Serikali, ikiwemo barabara za lami na mifumo ya kisasa ya usambazaji wa maji.

“Miundombinu hii inatuwezesha kuleta teknolojia ya kisasa ya kibayoteki, na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uvumbuzi wa matibabu Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema.